Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuwadia kwa mwezi mtukufu wa Muharram na siku za maombolezo ya Imam Abu Abdillah Al-Hussein (as), katika mji wa Khulna, Bangladesh, zilifanyika shughuli za siku kumi zilizojumuisha majlisi za maombolezo, mihadhara ya kidini na ibada mbalimbali za kuomboleza, programu hizo zilifanyika kuanzia tarehe mosi hadi tarehe kumi Muharram, kwa ushiriki mkubwa wa wapenzi wa Ahlul-Bayt (as) pamoja na makundi mbalimbali ya wananchi.
Katika shughuli hizo, Hujjatul-Islam Sayyid Ibrahim Khalil Rizvi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Imamiyya Bangladesh, alielezea falsafa ya harakati ya Ashura na ujumbe wa kudumu wa mapinduzi ya Imam Hussein (as), akirejelea tukio lenye kuhuzunisha la Karbala alisema: Takribani karne kumi na nne zilizopita, Imam Hussein (as), mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saww), pamoja na maswahaba wake waaminifu sabini na wawili, walijitoa mhanga katika ardhi ya Karbala kwa ajili ya kuhuisha haki, uadilifu na kupambana na dhuluma pamoja na upotovu, na hivyo wakawa wameacha mfano wa milele kwa watu wote huru duniani.
Ashura; alama ya mapambano kati ya haki na batili
Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Imamiyya Bangladesh alisisitiza: Tukio la Karbala ni somo kubwa kwa Umma wa Kiislamu, na ujumbe wa Ashura ni kwamba Waislamu kamwe hawapaswi kujisalimisha mbele ya dhuluma, batili na upotovu. Harakati ya Imam Hussein (as) haikuwa mapambano ya kisiasa wala ya kutafuta madaraka, bali ilikuwa ni dhihirisho la mapambano ya milele kati ya haki na batili, na mapambano ya mnyonge dhidi ya dhalimu, Imam Hussein (as) aliwafundisha Waislamu kwamba hata kwa kuyatoa mhanga maisha yao, wanapaswa kusimama imara dhidi ya uonevu.
Mwanazuoni huyo wa Bangladesh pia alisema: Licha ya kupita karne nyingi tangu tukio la Ashura, utukufu na athari za harakati hiyo si tu kwamba hazijapungua, bali kila mwaka utamaduni na ujumbe wa Imam Hussein (as) unaenea zaidi katika sehemu mbalimbali za dunia, na mataifa mengi zaidi ya watu huru yanapata msukumo kutoka kwake.
Hujjatul-Islam Ibrahim Khalil Rizvi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia uhalifu wa utawala wa Kizayuni huko Ghaza alisema: Leo Ghaza imegeuka kuwa Karbala ya zama hizi, uhalifu unaofanywa dhidi ya watoto, wanawake na wananchi wanyonge wa Palestina unakumbusha ukatili na dhuluma za majeshi ya Yazid huko Karbala, wale wanaojiona kuwa ni wafuasi wa madhehebu ya Imam Hussein (as) wana wajibu wa kusimama pamoja na wananchi wanyonge wa Ghaza na kutonyamaza mbele ya uvamizi na uhalifu wa utawala wa Kizayuni.
Kusisitiza umoja wa Umma wa Kiislamu
Katika hafla hiyo pia, Shafiq-ul-Islam Mona, Mwenyekiti wa tawi la mji wa Chama cha Nationalist cha Bangladesh, alisema katika hotuba yake kwamba; Ashura ni ujumbe wa umoja na mshikamano kwa Umma wa Kiislamu, alisema: Ikiwa Waislamu wataweka kando tofauti zao na maslahi madogo madogo na wakaungana, hakuna nguvu yoyote ya kidhalimu itakayoweza kuwatawala.
Maandamano makubwa ya maombolezo yafanyika Khulna
Katika siku ya mwisho ya shughuli hizo, sambamba na kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Imam Hussein (as), maandamano makubwa ya maombolezo yalifanyika katika mji wa Khulna, idadi kubwa ya wanawake na wanaume wa Kishia walishiriki katika maandamano hayo, na kwa kusoma nauha na kupaza kaulimbiu za kidini, walihuisha kumbukumbu ya mashahidi wa Karbala.
Waandaaji wa shughuli hizo walitangaza kuwa; lengo la kuandaa programu hizo ni kuendeleza utamaduni wa Ashura, kueneza roho ya kupambana na dhuluma, na kuimarisha umoja wa Kiislamu katika jamii.
Maoni yako