Alhamisi 11 Juni 2026 - 19:15
Mchambuzi wa Kipalestina: Mwamko wa Kisiasa katika Nchi za Ghuba Umeanza

Hawza/ Abdul Bari Atwan, mchambuzi na mwandishi mashuhuri wa Kipalestina huku akirejelea upinzani wa Saudi Arabia dhidi ya matumizi ya anga yake na Marekani kwa ajili ya kushambulia Iran, alisema kuwa; viongozi wa nchi za Ghuba wamefikia hitimisho kwamba; Marekani na Israel hawawezi kuhakikisha usalama wa eneo hilo, na kwamba zama za kujitolea mhanga kwa ajili ya maslahi ya Tel Aviv zimefikia mwisho.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Islami Analysis, Abdul Bari Atwan alitangaza kwamba; vitisho vya Trump vya kusema: “Ikiwa hamtasawazisha uhusiano wenu na Israel, Iran itaendelea kuwa tishio juu yenu,” vimesababisha aina fulani ya mwamko wa kisiasa katika nchi za Ghuba ya Uajemi.

Atwan, akichambua matamshi ya Trump yaliyoelekezwa kwa nchi za Kiarabu za Ghuba, hususan Saudi Arabia na Qatar, alisema kuwa; Washington inajaribu kuzishinikiza nchi hizi ili, kwa malipo ya kufikia makubaliano na Iran, zirejee tena kwenye mchakato wa kusawazisha mahusiano na Israel na kile kinachoitwa “Makubaliano ya Abraham.”

Alielezea mtazamo huo kuwa ni “wa kiburi, wa kijinga na mfano usio na kifani wa upungufu wa busara za kisiasa,” na akaongeza kwamba; mkakati wa Marekani wa kuzitishia nchi za Ghuba kwa kutumia Iran na kuzielekeza kuelekea Israel hauna tena ufanisi wake wa zamani.

Katika mahojiano na kanali ya YouTube ya Sawt, Atwan alirejelea tukio la kihistoria ili kufafanua mtazamo unaofaa kwa nchi za Ghuba na kusema kwamba; baada ya vikosi vya muqawama nchini Somalia kuwashambulia wanajeshi wa Marekani na miili ya baadhi yao kuvutwa mitaani, Marekani iliamua kujiondoa Somalia.

Katika kipindi hicho, Washington ilimtaka Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan kuongeza shinikizo dhidi ya Iran kuhusu visiwa vya Abu Musa, Tunb Kubwa na Tunb Ndogo, na hata kuvuruga njia za meli za Iran.

Kwa mujibu wa Atwan, Sheikh Zayed alijibu pendekezo hilo kwa kusema: "Nyinyi hata hamkuweza kukabiliana na makundi ya muqawama nchini Somalia, na mara tu ndege yenu ilipoanguka na rubani wenu kuuawa, mliondoka eneo hilo, sasa mnataka kutuingiza katika mgogoro na nchi kubwa na jirani kama Iran, kuna dhamana gani kwamba kesho hamtatuacha peke yetu na kuondoka katika eneo hili?"

Atwan anaamini kwamba viongozi wa sasa wa nchi za Ghuba pia taratibu wameanza kufikia hitimisho kwamba; kuutegemea “mwavuli wa ulinzi wa Marekani” si dhamana ya usalama wao.

Mchambuzi huyu wa Kipalestina aliendelea kusema kwamba; Marekani na Israel zina historia ndefu ya kuwaacha washirika wao, na hata makundi yaliyokuwa yanapinga Iran na kuhamasishwa na Washington pamoja na Tel Aviv mwishowe hayakupata msaada wa maana.

Aliongeza kwamba; Benjamin Netanyahu mara nyingi aliwataka wananchi wa Iran wachukue hatua dhidi ya mfumo wa kisiasa wa nchi yao na kuwaahidi msaada, lakini ahadi hizo hazikuwahi kubadilika kuwa hatua za vitendo.

Atwan pia alisisitiza kwamba; licha ya kuwepo kwa makumi ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba, si kambi hizo wala serikali washirika wa Washington hazijawahi kupata usalama kamili. Kwa mujibu wake, tishio kuu kwa uthabiti wa eneo hilo ni sera za nguvu za kigeni.

Atwan alitaja moja ya ishara muhimu za “mwamko huu wa kimkakati” kuwa ni msimamo wa hivi karibuni wa Saudi Arabia. Alisema kwamba Riyadh imetangaza rasmi na waziwazi kuwa haitaruhusu ndege za Marekani kutumia anga yake kwa ajili ya kushambulia Iran, na kwamba msimamo huo umeakisiwa hata katika vyombo rasmi vya habari vya Saudi Arabia.

Atwan alihitimisha uchambuzi wake kwa kusema: "Miongoni mwa viongozi wa nchi za Ghuba, aina fulani ya busara na uelewa wa kisiasa inaibuka, wamegundua kwamba Marekani imekuwa ikiwatumia zaidi kuliko kuwapatia usalama, na pia wameelewa kwamba si Marekani wala Israel hawawezi kutimiza malengo yao dhidi ya Iran."

Aliongeza kwamba kutokana na mabadiliko haya, mawasiliano, mikutano na uratibu wa kisiasa kati ya Riyadh na Iran vimeongezeka, na kwamba pande hizo mbili zinarejea kwenye mahusiano yanayojengwa juu ya ujirani mwema na maslahi ya pamoja.

Atwan alimalizia kwa kusema: "Nchi za Ghuba haziko tayari tena kujitoa mhanga kwa ajili ya Israel, zama za kutegemea nguvu za bandia zimefikia mwisho."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha