Jumatano 3 Juni 2026 - 10:10
Wafuasi wa madhehebu ya Ghadir wapo mstari wa mbele katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa / Muqawama wa leo wa Umma wa Kiislamu ni matunda ya mafundisho ya madhehebu ya Ghadir

Hawza/ Ayatullah Makarim Shirazi katika ujumbe wake kuelekea Kongamano la Kimataifa la Ghadir na Muqawama, huku akisisitiza kwamba Muqawama wa leo wa Umma wa Kiislamu ni matunda ya mafundisho ya madhehebu ya Ghadir, alieleza: Wafuasi wa madhehebu haya nchini Iran, Iraq, Lebanon, Yemen na nchi nyingine za Kiislamu, kwa kufuata viongozi wa dini, wamesimama mstari wa mbele katika kupambana na ubeberu wa kimataifa, na kwa kusimama imara dhidi ya njama na mashinikizo ya maadui, wanatetea heshima, utambulisho na maadili ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Ayatullah Nasser Makarim Shirazi, jana Jumanne tarehe 2 June, katika ujumbe wake kuelekea Kongamano la Pili la Kimataifa la Ghadir na Muqawama ambalo linaendelea kufanyika katika eneo la kaburi la Imamzade Yahya bin Zayd mjini Miyami, Mashhad, alieleza kwamba; kusimama imara kwa Umma wa Kiislamu dhidi ya dhulma na ubeberu ni matunda ya mafundisho ya madhehebu ya Ghadir.

Matini ya ujumbe wake ni kama ifuatavyo:

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

يَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّکُمْ تُفْلِحُونَ
 (Surat Aal Imran, Aya ya 200)

Mwanzoni mwa hotuba hii, ninatoa pongezi na hongera kwa Waislamu wote na Mashia duniani kwa kufika kwa Idi tukufu na yenye nuru ya Ghadir, hasa kwenu nyote mliopo hapa, na ninatoa shukrani zangu za dhati kwa waandaaji, wahusika na washiriki wa kongamano hili. Ninatarajia juhudi hizi zenye thamani ziwe chanzo cha athari nyingi njema na baraka nyingi katika kueneza na kukuza maarifa ya Ahlul-Bayt (as).

Mafundisho ya madhehebu ya Ghadir, kinyume na wanavyodhani baadhi ya watu wenye mtazamo finyu, yanaweza kuwa mojawapo ya mihimili muhimu zaidi ya mkusanyiko, mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu. Mtume Mtukufu wa Uislamu (saww), kwa kuitangaza Wilayah na Uimamu wa Amirul Muuminin Ali (as) na kusisitiza mapenzi pamoja na kumfuata yeye, alifungua njia ya kuendelea na kudumu kwa Uislamu halisi kwa wanadamu. Maarifa haya ya Mwenyezi Mungu katika historia yote yamehifadhi njia iliyo wazi ya Uislamu wa asili na kuzuia kupotoka na kusahaulika kwake.

Miongoni mwa sifa mashuhuri za madhehebu haya ni nafasi ya Imam Maasumu (as) na mafaqihi wa Umma kama manaibu wa watukufu hao katika kuongoza na kuielekeza jamii ya Kiislamu; watu ambao daima wamekuwa wabeba bendera ya kusimama imara dhidi ya dhulma na ubeberu na wamezuia kuyumba na kupotoka kunakotokana na unafiki, ujinga na kutafuta maslahi ya kidunia.

Historia inashuhudia kwa uwazi kwamba; kushindwa na kubaki nyuma kwa Umma wa Kiislamu mara nyingi ni matokeo ya matendo ya watawala wasio na imani au dhaifu ambao kwa shinikizo dogo tu au kwa kushawishiwa, waliweka mbele maslahi yao binafsi na starehe zao badala ya maslahi ya Umma wa Kiislamu, au kwa kueneza hali ya kukata tamaa na udhaifu walizisukuma jamii za Kiislamu kuelekea kujisalimisha mbele ya maadui na kujitenga na misingi ya imani na mafundisho ya Uislamu.

Kama isingekuwa kusimama imara kwa wanazuoni wachamungu, wenye kutenda na wenye kuwajibika, pamoja na uthabiti wa viongozi wa dini, sehemu kubwa ya utambulisho wa Kiislamu ingekuwa imetoweka na ukafiri pamoja na ubeberu wa kimataifa vingekuwa vimetawala kikamilifu ardhi na rasilimali za Kiislamu; kama ambavyo kwa masikitiko mifano yake inaonekana katika baadhi ya nchi za Kiislamu. Ukweli huu unaonesha wazi umuhimu wa watu kufuata uongozi wa dini, kama tulivyoshuhudia mfano ulio wazi katika maisha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uhusiano wa pande mbili kati ya Imam na Umma.

Katika kipindi cha sasa pia, kama ulimwengu unavyoshuhudia, hawa ndio wafuasi wa madhehebu ya Ghadir ambao katika maeneo mbalimbali duniani kuanzia Iran, Iraq, Lebanon, Yemen na maeneo mengine, kwa kufuata viongozi wa dini na viongozi wa Mwenyezi Mungu, wamesimama kwa uthabiti na heshima katika medani ya itikadi na vitendo dhidi ya njama na mipango ya madhalimu na watawala wa kidhalimu, na wameyatoa maisha yao na mali zao katika njia hii.

Bila shaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwasaidia Waumini imetimia na itaendelea kutimia, na hivi karibuni ushindi wa wazi wa Uislamu na kushindwa kwa fedheha kambi ya ukafiri vitaonekana zaidi, kilele cha nusra hii ya Mwenyezi Mungu kitafikiwa kwa kudhihiri Mtukufu Imam wa zama (roho zetu ziwe fidia kwake) na kusimamishwa serikali ya kimataifa ya uadilifu na Tawhidi, Inshaallah Ta'ala.

Linalothibitisha na kufafanua jambo hili ni mwelekeo unaoongezeka wa wapenda uhuru na watafuta haki katika sehemu mbalimbali duniani — kutoka madhehebu mbalimbali ya Kiislamu na hata wafuasi wa dini nyingine — kuelekea kwenye bendera hii na madhehebu haya ya Mwenyezi Mungu; mwelekeo ambao unatoa bishara ya maandalizi ya nyoyo kwa ajili ya kukusanyika chini ya bendera ya mapinduzi ya Mahdi Aliyeahidiwa (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Kwa mara nyingine tena, sambamba na kutoa pongezi kwa Idi hii kubwa, ninatoa shukrani kutokana na juhudi za waandaaji wote wa Kongamano la Ghadir na Muqawama pamoja na washiriki wote waheshimiwa, na ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie sote kuwa miongoni mwa Mashia wa kweli wa Amirul Muuminin Ali (as) na miongoni mwa watakaonufaika na uombezi wake.

Na amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake

Qum

Nasser Makarim Shirazi
Khordad 1405 – Dhul-Hijjah 1447

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha