Ijumaa 29 Mei 2026 - 19:00
Erdogan: Netanyahu Atapata Funzo Lake Mbele ya Ulimwengu wa Kiislamu

Hawza/ Rais wa Uturuki, Rajab Tayyib Erdogan, katika hotuba yake baada ya Swala ya Idi ya Adh-ha ndani ya Msikiti Mkuu wa Çamlıca mjini Istanbul, huku akisisitiza umuhimu wa umoja wa ulimwengu wa Kiislamu na akirejelea maendeleo ya Ghaza, alibainisha kwamba “Benjamin Netanyahu” atapata jawabu la matendo yake mbele ya Waislamu duniani.

Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Rajab Tayyib Erdogan, rais wa Uturuki, asubuhi ya Idi ya Adh-ha alitoka katika makazi yake mjini Istanbul na kuelekea Msikiti Mkuu wa Çamlıca kwa ajili ya kuswali Swala ya Idi, alipowasili msikitini alikutana na kuzungumza na wananchi, na akaswali Swala ya Idi nyuma ya Hafidh Karim Ozturk, Imam-Khatibu wa msikiti huo, pamoja na wananchi.

Baada ya swala hiyo, Erdogan alisikiliza khutba ya Idi na kisha katika hotuba yake kwa waumini alimwomba Mwenyezi Mungu aufikishe Umma wa Kiislamu katika Idi zijazo kwa afya na amani, na akasema: “Natumai umoja na mshikamano wetu utaendelea kudumu na undugu huu utaendelea hadi Siku ya Kiyama.”

Rais wa Uturuki huku akiashiria kwamba Idi ya Adh-ha kuwa ni “Idi ya kudhihirisha kujisalimisha mbele ya Mwenyezi Mungu” alisema: “Tunamuomba Mola atupe sisi sote roho hii ya kujisalimisha; tusijitenge kamwe na njia hii na tuendelee na njia yetu kwa imani hii hii, leo tunaitafuta roho hii ya kujisalimisha huko Ghaza na Palestina, maadamu roho hii ipo, ulimwengu wa Kiislamu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu utabaki wenye umoja, nguvu na uhai, na undugu wa Kiislamu utaendelea kuwepo.”

Erdogan aliendelea kwa kuyapa pongezi za Idi ya Adh-ha mataifa ya Kiislamu, na baada ya kumalizika kwa hafla hiyo alikutana na waumini walioshiriki Swala ya Idi.

Pia katika mazungumzo yake na waandishi wa habari nje ya msikiti, alisema Idi za Kiislamu ni alama ya mapenzi, heshima, umoja na mshikamano, na akaongeza: “Idi ya Adh-ha ina sifa ya pekee; Idi hii ni Idi ya kujisalimisha na kujitoa mhanga, katika Idi hii tunashuhudia kujisalimisha kwa baba na mwana mbele ya amri ya Mwenyezi Mungu, na kuchinja ni alama ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.”

Rais wa Uturuki akirejelea ibada ya Hijja alisema: “Huko Arafat tulishuhudia mkusanyiko wa Waislamu na mandhari ya umoja pamoja na kujisalimisha, sasa Mahujaji wameanza kurejea, Tunamuomba Mwenyezi Mungu aikubali Hijja ya mahujaji wote na awajalie Waislamu wote roho hii ya umoja na mshikamano.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake huku akirejelea maendeleo ya Palestina na Ghaza alisisitiza: “Tumepitia siku ngumu za Palestina na Ghaza, kinachotokea Palestina na Ghaza kina maana maalumu na msimamo tofauti kwetu katika Idi hii, ninaamini kwamba; mtu kama Netanyahu ambaye amekuwa alama ya dhulma na jinai, atapata funzo linalostahili mbele ya Waislamu wa dunia. Tunatumaini kwamba hivi karibuni tutashuhudia matunda ya kusimama huku imara na mamilioni ya Waislamu watahisi hilo moja kwa moja, Mwenyezi Mungu awe msaidizi na mlinzi wetu, tunatumaini Idi ya Adh-ha itakuwa sababu ya umoja wa ulimwengu wa Kiislamu.”

Katika hafla ya Swala ya Idi ya Adh-ha, idadi ya viongozi na shakhsia za kisiasa za Uturuki walihudhuria, miongoni mwao alikuwa ni Ismail Kahraman, aliyekuwa spika wa zamani wa Bunge la Taifa la Uturuki, Osman Askin Bak Waziri wa Michezo na Vijana, Mehmet Fatih Kacır Waziri wa Viwanda na Teknolojia, Burhanettin Duran mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya Rais, Süleyman Soylu mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Ndani ya Bunge na mwakilishi wa Istanbul, Davut Gül gavana wa Istanbul na wengineo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha