Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, ujumbe wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya kufunguliwa kwa kipindi cha kwanza cha Bunge la Ushauri la Kiislamu na kuanza mwaka wa tatu wa shughuli za Bunge la kumi na mbili umechapishwa.
Matini ya ujumbe wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.
Nawapongeza wananchi wote wapendwa wa Iran na wawakilishi waheshimiwa wa Bunge la Ushauri la Kiislaam kwa mnasaba wa Idi Tukufu ya Adh-ha na kumbukumbu ya kufunguliwa kwa kipindi cha kwanza cha Bunge la Ushauri la Kiislamu, na kwa mnasaba huu ninatoa shukrani kutokana na juhudi za wawakilishi, hususan Spika mtukufu wa Bunge la Ushauri la Kiislamu, Mheshimiwa Dkt. Qalibaf, katika njia ya kuinua hadhi ya nchi.
Bunge la Ushauri la Kiislamu ni kiini cha taifa, ni dhihirisho la demokrasia ya kidini, na ni nguzo ya sheria na utungaji wa sheria katika Jamhuri ya Kiislamu ambayo ina nafasi muhimu katika kutekeleza matakwa ya wananchi. Sasa baada ya kupita miezi mitatu tangu Vita Takatifu vya tatu, ubora wa ndani na kiini halisi cha wananchi wa Iran katika imani, matumaini na vitendo vimethibitika kwa rafiki na adui; na kuinuka kwa kiwango cha wananchi wa Iran kumeweka wazi kwa namna ya kuvutia sana kiini cha fadhila za taifa hili.
Kwa kuwa mwakilishi wa kweli wa taifa anapaswa kuwa wa aina ya taifa lenyewe, kipindi cha sasa ni hatua ya mageuzi ya kudhihiri kwa mwamko wa wananchi ndani ya wawakilishi na Bunge la Ushauri la Kiislamu ili waanze utekelezaji wa wajibu wao kwa kiwango cha taifa lililoamshwa, na kwa kazi na ubunifu wa ziada, waharakishe na kuimarisha utungaji wa sheria na usimamizi katika njia ya kuweka misingi ya mustakabali wa Iran.
Katika uwanja huu wa jihadi, kiti cha uwakilishi kinachukuliwa kama handaki la mstari wa mbele wa mageuzi katika njia ya maendeleo ya nchi; hivyo inafaa wawakilishi wa taifa, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa kutawassali kwa Imaam wa Zama (as), na kwa kuhifadhi damu safi za mashahidi madhulumu wa vita viwili vya kulazimishwa vya Marekani na Kizayuni, na katika kilele chao akiwa kiongozi wetu shahidi mtukufu (ra), watumie kwa juhudi zote uwezo na nguvu zao kwa ajili ya utawala unaoshirikiana kwa ukamilifu na serikali pamoja na taasisi nyingine huku wakihifadhi uhuru wa mhimili wa kutunga sheria, katika njia ya kuifanyia nchi mageuzi yanayostahili, kutatua matatizo ya wananchi hususan masuala ya kiuchumi na maisha, kuimarisha uzalishaji na ajira, kukuza kiwango cha elimu na viwanda, kuinua utamaduni na maadili, kupambana na ufisadi wa kifedha, kudhibiti mfumuko wa bei na gharama za maisha, pamoja na kuondoa umaskini kwa upana.
Kwa msingi huu, ni lazima maamuzi ya Bunge yawe na uhusiano wa moja kwa moja na unaoonekana wazi na masuala makuu ya nchi pamoja na mahitaji ya wananchi, na yaelekezwe katika kuleta matumaini na kujenga mustakabali wa nchi.
Jamii kabla ya kila kitu inahitaji kuona dalili halisi za matumaini, njia thabiti na upeo ulio wazi wa mustakabali ili iweze kupanga na kusonga mbele kwa msingi huo; na wawakilishi wa Bunge kupitia misimamo yao, maamuzi yao na hotuba zao wanaweza kulifanya Bunge la Ushauri la Kiislamu kuwa taasisi inayoongoza katika kuleta matumaini, miongoni mwa hayo ni kwamba katika mazingira ya sasa, kwa kushirikiana kwa mihimili ya utendaji na mahakama, kwa kuzingatia kaulimbiu ya “Uchumi wa kujitegemea, chini ya kivuli cha umoja wa taifa na usalama wa taifa” katika mwaka 1405, waweke uthabiti wa kiuchumi, kupunguza mfumuko wa bei, kusimamia ukwasi, kukuza uzalishaji, kurekebisha mpango wa saba wa maendeleo, na kuongeza vipengele vinavyohusiana na ukarabati na ujenzi mpya wa hasara za vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa kuwa ajenda kuu, na wachore ramani ya mwendo wa serikali na sekta nyingine katika hali ya sasa na kipindi cha baada ya vita.
Kwa ajili ya kutekeleza wajibu kwa kiwango cha taifa lililoamshwa, pia kunahitajika maandalizi na masharti mbalimbali ambayo katika fursa hii fupi ninawashauri tu ndugu na dada waheshimiwa kuyasoma kwa makini na kwa uzito maelezo ya kauli za Kiongozi wetu mkuu shahidi (as), katika mikutano ya kila mwaka na wawakilishi wa Bunge la Ushauri la Kiislamu, hususan katika miaka ya hivi karibuni ambayo yana thamani kubwa ya kimajaribio na kiutendaji. Ni jambo la kawaida kwamba kuzingatia uchamungu binafsi kuna nafasi ya msingi katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo hayo na kutekeleza kwa usahihi wajibu mzito katika kipindi hiki nyeti, kutambua kwa usahihi vipaumbele, maoni yanayotokana na tafiti, mashauriano ya kina ya kitaalamu, maisha ya karibu na wananchi na mawasiliano mapana na wananchi, kupambana kwa upana dhidi ya ufisadi, kutanguliza maslahi ya taifa na madai ya umma juu ya mahitaji na maslahi ya kisiasa ya makundi na maeneo, kuzingatia diplomasia ya kibunge, ujasiri na kutangaza misimamo ya wazi na madhubuti mbele ya tamaa za wakandamizaji wakubwa, pamoja na kuzingatia kwa akili na kimapinduzi nafasi mpya ya Iran katika eneo na duniani, ni miongoni mwa masharti hayo. Miongoni mwa mifano ya uchamungu ni kuhifadhi neema kubwa ya umoja wa taifa na mshikamano wa kipekee ambao umetolewa kwa taifa lililoamshwa chini ya bendera ya Iran, na ambazo ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za ushindi mbele ya Shetani Mkubwa.
Shukrani za neema hii ni juhudi za watu wote wa taifa, hususan wasomi wa fikra na siasa, wakiwemo wawakilishi wa Bunge, katika kulinda umoja huu na kujiepusha na tofauti za kisiasa zisizo na maana pamoja na kuonesha tofauti za kijamii. Mpango na njama za kipofu za adui — baada ya vita vya kulazimishwa, shinikizo la kiuchumi, na mzingiro wa kisiasa na kipropaganda — ni kuleta mifarakano na mgawanyiko wa kijamii ili kufidia kushindwa kwake katika medani ya kijeshi na kulipigisha taifa magoti, ni lazima kila mmoja wa wale wanaojitoa mhanga ambao nyoyo zao zinadunda kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi au kwa ajili ya uhuru na utukufu wa Iran, hivi sasa zaidi kuliko hapo awali, wajitahidi kulinda umoja wa safu zilizoungana na kushikamana za taifa, na wasigeuze tofauti zisizo na msingi na hata zenye msingi kuwa mizozo na mifarakano, na kwa kauli na vitendo wawe dhihirisho la mshikamano na umoja wa taifa, InshaAllah.
Ninakuombeeni mafanikio katika wajibu mzito sana wa kuliwakilisha taifa adhimu ambalo limesimama kifua mbele dhidi ya dhulma na uvamizi wa wanyama wakali na waovu wa zama hizi, na ambalo linaielekeza historia katika mwelekeo wake sahihi. Kwa matumaini kwamba dua ya Imam wetu (as) iwe yenye kuwasaidia, kuwaongoza na kuvutia mafanikio ya Mwenyezi Mungu kwa ajili yenu wapendwa.
Wassalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei
7/Khordad/1405 - 28 Mei 2026
Maoni yako