Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Muungano wa Watetezi wa Katiba ya Indonesia, unaojumuisha makundi 36 ya wananchi, ulikusanyika mbele ya jengo la serikali la Grahadi mjini Surabaya nchini Indonesia katika hatua ya kibinadamu, washiriki katika mkusanyiko huo waliitaka serikali kuimarisha msimamo wake wa kupinga ukoloni na kuhifadhi uhuru wa diplomasia ya Indonesia.
Katika mkusanyiko huo, waandamanaji pia walitaka serikali ijiondoe mara moja kutoka katika kile walichokiita “Bodi ya Amani” (BOP), ambayo kwa mtazamo wao inaweza kuathiri mwelekeo wa diplomasia ya taifa.
“Bodi ya Amani” ni taasisi ya kimataifa ambayo, kwa mujibu wa waandamanaji hao, imejionesha kwa sura ya kuendeleza ajenda ya amani ya dunia na ujenzi wa Ghaza baada ya usitishaji vita, walisema kuwa; taasisi hiyo ilianzishwa kutokana na kile walichokitaja kuwa hila za Donald Trump, Rais wa Marekani, kwa lengo la kuhalalisha uhalifu wa Israel, aidha walieleza kuwa, Prabowo Subianto, Rais wa Indonesia, alitia saini tarehe 22 Januari 2026 pembezoni mwa mkutano wa Davos. Ushiriki wa Indonesia katika taasisi hiyo hivi karibuni umekabiliwa na ukosoaji mkali wa ndani ya nchi.
Saleh Ismail Makdar, mratibu wa mkusanyiko huo, alisisitiza kwamba; harakati hiyo imejengwa juu ya wasiwasi kuhusu masuala ya kibinadamu ya kimataifa na haijaathiriwa na maslahi ya kundi lolote maalumu.
Aliwaambia waandamanaji: "Hii ni hatua ya kibinadamu, tunapinga aina yoyote ya ukoloni na ubeberu dhidi ya mataifa huru."
Muungano wa Watetezi wa Katiba unaamini kwamba; Indonesia haipaswi kuingia katika mzunguko wa maslahi ya kambi za madola makubwa duniani, waliitaka serikali kufufua misingi ya sera ya mambo ya nje ya “uhuru wa kujitegemea na kutofungamana na upande wowote”, kwa mujibu wa Katiba na roho ya Mkutano wa Afrika na Asia.
Aliongeza: "Indonesia haipaswi kujisalimisha mbele ya maslahi ya dola yoyote kubwa, sera ya mambo ya nje lazima irejee katika maelekezo ya Katiba; yaani kuwa huru, hai na inayopinga aina zote za ukoloni."
Waandamanaji pia walirejelea mgogoro wa kibinadamu nchini Palestina, hasa Ghaza, ambao kwa mtazamo wao unahitaji msimamo wa kidiplomasia ulio wazi zaidi na wenye hatua madhubuti kutoka Indonesia katika majukwaa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa muungano huo, Indonesia ina jukumu la kihistoria na kimaadili la kubaki mstari wa mbele katika kuunga mkono mapambano ya mataifa yaliyodhulumiwa.
Walisema kwamba; kuongezeka kwa shinikizo la umma kuhusu msimamo wa serikali katika masuala ya kimataifa kunaonesha matarajio makubwa ya jamii kwa Indonesia ili ibaki thabiti katika kuunga mkono uhuru na uadilifu wa kimataifa.
Saleh alisisitiza: "Ikiwa Indonesia itanyamaza, itakuwa imeisaliti historia ya mapambano ya watu wake."
Katika kipindi chote cha mkusanyiko huo, waandamanaji walibeba mabango na vipeperushi vyenye ujumbe wa kupinga ukoloni, kuonesha mshikamano wa kibinadamu na kuunga mkono uhuru wa Palestina, vikosi vya usalama vilikuwa vimeimarisha ulinzi mkali, huku wazungumzaji mbalimbali wakisisitiza kwa zamu umuhimu wa kuhifadhi uhuru wa sera ya mambo ya nje ya Indonesia katika mazingira ya kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa wa kimataifa.
Mwishoni mwa mkusanyiko huo, waandamanaji walisoma kwa pamoja tamko la kupinga aina zote za ukoloni na uingiliaji wa kigeni, sauti zao zilienea mbele ya jengo la Grahadi huku wakisisitiza matakwa yao kwamba; Indonesia ibaki katika mstari wa sera ya mambo ya nje iliyo huru, hai na isiyofungamana na upande wowote kwa mujibu wa Katiba na historia ya diplomasia ya taifa lao.
Waandamanaji walipaza sauti huku wakisema: “Ukoloni ukomeshwe duniani kote, Indonesia irejeshwe katika sera ya kujitegemea na kutofungamana na upande wowote, simameni pamoja na watu wanaodhulumiwa.”
Chanzo: Ahlulbait Indonesia.
Maoni yako