Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ihab Hamadeh, mbunge na mwanachama wa Kundi la “Uaminifu kwa Muqawama”, katika hafla ya kuwaenzi mashahidi mujahidi Muslih Najib Saqr na Hassan Radhi Saqr, iliyofanyika katika Husseiniyya ya mji wa Hadath Baalbek huku ikuhudhuriwa na wanazuoni, familia za mashahidi na jamii za watu wa eneo hilo, alisisitiza kwamba: Hata kama dunia yote itaungana dhidi yetu, hawataweza kamwe kutunyang’anya kwa nguvu hata chembe ya heshima yetu, ardhi yetu na ari yetu; ingawa sasa wameungana dhidi yetu; kuanzia ndani ya Lebanon, hadi utawala wa Kizayuni, Waarabu wa umma huu, na hata waliotengwa na kufukuzwa na ulimwengu, aliongeza: Wako katika vita dhidi yetu na sisi tumesimama imara, na kama ilivyokuwa katika vita vyote vilizopita, tutashinda, leo tunaona kwamba wanajeshi wa Kizayuni katika maeneo yote ya kusini na katika vituo vyao vyote vya kijeshi, wanalengwa na wapiganaji wa Muqawama na wananaswa kama mawindo.
Hamadeh katika hotuba yake aliongeza kwamba; wachambuzi wengi ndani ya utawala wa Kizayuni wanazungumzia kuhusu “mtego wa kimkakati” ambao wamekwama ndani yake baada ya kuingia katika ardhi ya kusini mwa Lebanon.
Mwanachama huyo wa Kundi la Muqawama katika sehemu nyingine ya hotuba yake, huku akirejelea vikwazo vipya vilivyowekwa dhidi ya baadhi ya wstu, alisema: Jana waliweka kundi fulani katika orodha ya vikwazo; orodha hii kwetu ni orodha ya fahari na heshima, kuwekwa kwa majina ya ndugu zetu katika orodha ya vikwazo vya “Shetani Mkubwa” kunamaanisha kwamba tumesimama mahali sahihi na katika nafasi ambayo Mwenyezi Mungu ametutaka tusimame, hatua hizi ni vitisho na jaribio la kutisha watu, ambalo hufanyika pale karata zao za ushindi zinapowatoka mikononi, ndipo hukimbilia orodha kama hizi ambazo hazitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuongeza uimara wetu na kusisitiza kwetu kuendelea kupambana na madhalimu.
Hamadeh aliendelea kusema: Jambo la kuzingatiwa katika orodha hii ni kuwepo kwa majina ya maafisa kutoka Jeshi la Lebanon na vikosi vya Usalama wa Umma, jambo linaloonyesha mambo mawili: Kwanza, pale maafisa wa jeshi wanapowekewa vikwazo kwa visingizio vya kipuuzi na visivyo na thamani, maana yake ni kwamba taasisi ya kijeshi na Jeshi la Lebanon limegeuzwa kuwa shabaha ya wazi ya mradi wa Kizayuni na Amerika nchini Lebanon, tunapaswa kutoa tahadhari kuhusu jambo hili na kulikabili; kwa sababu jeshi hili la kitaifa halikutii maagizo ya mradi wa Kizayuni na Amerika, na sasa wanaliwekea shinikizo ili kulisukuma katika mwelekeo utakaohudumia maslahi ya mradi huo, yaani “fitna na migogoro ya ndani” nchini Lebanon.
Mwishoni, alisisitiza kuwa: Utawala huu ni utawala tegemezi na uliosalimu amri; kama hatutasema kwamba ni mshirika katika kumwaga damu za watoto, wanawake na vijana wetu, vipi utawala huu unaweza kuunyoosha mkono wake kuelekea mkono ule mchafu wa “Israel”? Na vipi mkono unaojiita wa Kilebanoni unaweza kusalimiana na mkono uliolowana na kuzama katika damu za Walebanoni?
Mwishoni mwa hafla hiyo, baada ya hotuba ya Imamu wa jamaa wa mji huo, Sheikh Majid Saqr, kwa niaba ya familia za mashahidi, ilionyeshwa video maalumu ya shahidi Muslih Saqr, na hafla ikahitimishwa kwa kumbukumbu ya msiba wa Ahlul-Bayt (as) iliyosomwa na Sheikh Talal Al-Mismar.
Maoni yako