Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kuitambua hakika ya mahitaji ya mwanadamu na lengo la mwisho la maisha ni miongoni mwa masuala ya msingi kabisa ya fikra na itikadi; kwa sababu ikiwa mwanadamu hatautambua mwisho wake wa kweli, huenda akaweka mipaka ya maisha yake katika kiwango cha mahitaji ya kimada na matamanio ya muda mfupi ya kidunia. Kujua suala hili humuelekeza mwanadamu kutoka katika sura ya nje ya mahitaji kuelekea katika ukweli wa “kumjua Mungu” na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa msingi huu, sehemu ya hotuba za Ayatullah Misbah Yazdi inawasilishwa kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu
Sote tunakiri kwamba hitaji la ndani kabisa la uwepo wa mwanadamu ni utegemezi wake kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; jambo ambalo hakuna akili timamu inayoweza kulikanusha, lakini swali ni hili: ni kwa kiwango gani sisi tunajitahidi katika kukidhi hitaji hili tukufu? Wengi wetu huweka kiwango cha mwisho cha juhudi zao katika kujiepusha na dhambi na kutekeleza wajibu wa kidini.
Kwa upande mwingine, tunawaona watu ambao usiku na mchana wao huupitisha katika ibada na kuomba dua; watu ambao huswali maelfu ya rakaa na kuwasaidia wahitaji katika nyumba za mafakiri. Watu hawa, kama Imam Ali (as), katika kilele cha ikhlasi na ukaribu na nyakati za alfajiri, huomba na kulia kwa sababu ya umbali na urefu wa njia, uelewa wao kuhusu hitaji lao kwa Mwenyezi Mungu una tofauti kubwa sana na uelewa wetu.
Mawalii hawa wa Mwenyezi Mungu wanayatambua mahitaji ambayo sisi hata hatujawahi kuyafikiria, hawafanyi mzaha na Mwenyezi Mungu; machozi yao ni ya ukweli, na baada ya ibada ndefu hukiri: “Ah! Njia iliyo mbele ni ndefu sana na nimechukua akiba ndogo mno!” Hili linaonesha kwamba wao wameutambua ukweli wa hitaji lao kwa namna ya kina zaidi.
Ni kana kwamba sisi, kutokana na kushikamana na mambo ya kidunia, “tumeharibika” na hatuna uelewa sahihi wa mahitaji yetu halisi, sisi zaidi tunayatambua mahitaji yetu ya kihayawani na kimwili, lakini hitaji halisi la kibinadamu kwa Mwenyezi Mungu hatulielewi ipasavyo, ikiwa tu tutafanikiwa kulitambua hitaji hili, hilo lenyewe ni mafanikio makubwa kabisa.
Baada ya kuutambua ukweli huu, kiwango cha juhudi zetu za kuliondoa hitaji hili na kujikurubisha kwa “Chanzo cha kutohitaji” ndicho kitakuwa kipimo cha kutathminiwa kwetu, kutembea katika njia hii ndiyo maana ya “kuwa Shia wa Ali”, “kufuata njia ya Imam Hussein (as)” na “kuwa Hussein”.
Lakini ikiwa sisi tutabaki tu katika kiwango cha mahitaji yetu ya kimada, mwisho wa matamanio yetu utakuwa ni kwamba dhulma iondoke ili watu waishi kwa starehe zaidi; na katika hali bora zaidi, kila kitu kitarejea kwenye “raha za dunia”.
Je, mnakumbuka kwamba Imam alisema Uislamu na Mitume wote wamevumilia mateso kwa ajili ya kusimamisha uadilifu; lakini kusimamisha uadilifu hakukuwa mwisho wa lengo, alifafanua wazi lengo la mwisho ni nini: “Kumjua Mwenyezi Mungu”. Na huu ni ukweli ambao huenda mimi na watu kama mimi bado hatuwezi kuuelewa kwa kina ipasavyo naam, kuielewa maana hii ni jambo lililo juu ya upeo wa ufahamu wa wengi wetu.
Jambo tunalopaswa kuelewa si kutambua mahitaji tu; bali ni kwamba mwanadamu, zaidi ya mahitaji ya nje na ya kimwili, anahitaji ukweli ulio wa juu zaidi, Ulimwengu huu ni uwanja wa vipaji na uwezo uliojificha; na mwanadamu anapaswa kujitahidi kuvifanya vipaji vile alivyowekewa na Mwenyezi Mungu ndani yake viwe halisi.
Mitume walikuja ili kutuonesha njia ya kufikia uhalisia huu; walikuja ili kusema nini kifanyike ili mwanadamu achanue na afikie ukamilifu.
Maoni yako