Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Majma’ ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) kwa kutoa taarifa rasmi imeonesha msimamo wake kuhusu kufutwa uraia wa baadhi ya wananchi wa Bahrain na utawala wa Aal Khalifa pamoja na kuongezeka kwa vikwazo dhidi ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s) katika eneo hilo, na imezilaani vikali hatua hizo.
Majma’ hiyo katika taarifa yake ilisisitiza kwamba; ukimya au hatua hafifu za Jumuiya ya kimataifa mbele ya mwenendo huu hatari zitasababisha tawala za kidikteta kuwa na ujasiri zaidi katika ukiukaji wa wazi wa haki za kiraia na kueneza adhabu za pamoja katika eneo hili.
Matini ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:
Majma’ ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), huku ikionesha wasiwasi mkubwa na kwa maneno makali kabisa, inalilaani tendo haramu, la kiholela na linalokiuka haki za binadamu lililofanywa na serikali ya Bahrain la kuwanyang’anya uraia watu 69 wananchi wa nchi hiyo, pamoja na kuwakamata baadhi ya wanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo na kufuta uanachama wa wabunge watatu wa bunge hilo.
Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, miongoni mwa watu hao wapo wanazuoni wa dini, wasomaji wa nauha, wanaharakati wa kijamii, wanawake, wanaume na hata watoto pamoja na watoto wachanga, ambao bila ya taratibu zozote za kimahakama, bila ya uchunguzi wa kisheria na nje ya mamlaka ya vyombo vya mahakama, na kwa kutegemea tu amri ya Mfalme wa Bahrain, wameondolewa haki yao ya kiasili ya uraia. Hatua hii ni mfano wa wazi wa hukumu za pamoja na adhabu zisizo za kisheria ambazo hazikubaliki katika mfumo wowote wa sheria wenye ustaarabu.
Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, haki ya uraia ni miongoni mwa haki za msingi kabisa za kila mtu. Kifungu cha 15 cha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, ambacho kinaakisi sheria za kimataifa za kimila, kinaeleza wazi kwamba: “Hakuna mtu anayepaswa kunyimwa uraia wake kwa njia ya kiholela.” Hatua ya serikali ya Bahrain ya kuwanyang’anya watu uraia bila kupitia mchakato wa haki wa kimahakama na bila kutenganisha kati ya watuhumiwa na wanafamilia wao, hususan watoto na vichanga ambao hawana nafasi yoyote katika tuhuma zinazowekwa, ni ukiukaji wa wazi wa wajibu wa kimataifa wa nchi hiyo chini ya kifungu cha 24 aya ya 3 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, pamoja na vifungu vya 7 na 8 vya Mkataba wa Haki za Mtoto. Kujumuishwa kwa watoto wachanga katika uamuzi huu si tu kunapingana na misingi ya haki za binadamu, bali ni mfano wa kunyimwa uraia kwa lazima na adhabu za pamoja ambazo zimekatazwa vikali na taasisi za usimamizi za Umoja wa Mataifa.
Majma’ ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) inasisitiza kwamba; tuhuma za uongo na za kurudiwa-rudiwa za kuisaidia Iran au kufanya ujasusi kwa ajili ya taasisi za kigeni ni visingizio tu vya kukandamiza wapinzani na kufanya ukiukaji wa kimfumo wa haki za kiraia nchini Bahrain. Mfumo huu wa ukandamizaji unakumbusha mwenendo usio wa kibinadamu wa tawala za kiimla na unaharibu kabisa uhalali wa madai yoyote ya kuwepo kwa utawala wa sheria nchini Bahrain. Hatua hii pia ni ukiukaji wa kanuni ya kutokuwepo kwa ubaguzi na kanuni ya uwiano katika utoaji wa adhabu, kwa sababu kuwanyima watoto na vichanga uraia hakuna uhusiano wowote na tuhuma za kisiasa zinazowekwa kwa wazazi wao.
Majma’ ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) inazitaka taasisi zote za uangalizi wa haki za binadamu za Umoja wa Mataifa, hususan Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Baraza la Haki za Binadamu, Kamati ya Haki za Mtoto, pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, na pia Mara'ji' wakubwa na wanazuoni mashuhuri, kwamba kwa haraka na rasmi zilaani hatua hii isiyo ya kibinadamu na isiyo ya kisheria, na kuitaka serikali ya Bahrain kurejesha bila ya kuchelewa uraia wa watu wote husika, hasa
watoto na viachanga, na kutangaza kwamba hakuna mtu anayepaswa kunyimwa haki yake ya kiasili ya uraia nchini Bahrain kwa sababu ya uhusiano wa kifamilia au mitazamo ya kisiasa.
Ukimya au hatua hafifu za Jumuiya ya kimataifa mbele ya mwenendo huu hatari zitasababisha tawala za kidikteta kuwa na ujasiri zaidi katika ukiukaji wa wazi wa haki za kiraia na kueneza adhabu za pamoja katika eneo hili.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku ikitangaza mshikamano wake na familia zilizodhuriwa na kulaani vikali hatua hii ya kupinga ubinadamu, imeonya kuhusu matokeo hatari ya kuenea kwa mwenendo kama huu, na imesisitiza umuhimu wa nchi zote kushikamana na misingi ya haki za binadamu na kukataza kunyimwa uraia kwa njia ya kiholela.
Pia inafaa kutajwa kwamba kufuatia mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuanza kwa Vita vya Tatu vya Kulazimishwa, ambavyo vilifanyika kwa ushirikiano wa watawala waliojiuza na makoloni ya Marekani katika eneo hili, watawala hao katika kilele cha fedheha na kuvunjika moyo, na kwa hofu ya kuporomoka kwa taji zao za kifalme na utawala wao dhaifu, wameweka vikwazo na mashinikizo yasiyokuwa na mfano dhidi ya Mashia kwa kosa la kuwaonesha mshikamano wananchi pendwa wa Iran katika huzuni ya kumpoteza Kiongozi wao mkubwa.
Na kwa ajili ya kueneza hofu na vitisho miongoni mwa Mashia, hata watu ambao katika profaili za simu zao au katika ujumbe wao waliandika aya ya:
إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ
“Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika Kwake Yeye tutarejea,”
wamekuwa wakifuatiliwa, kukamatwa, kunyang’anywa uraia na kufukuzwa nchini.
Maoni yako