Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Makarim Shirazi, katika kikao chake na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Iran, huku akirejelea ugumu na unyeti wa uga wa diplomasia, alisema: Kama ambavyo matatizo ya uwanja wa vita si madogo kuliko uga wa diplomasia, masuala na changamoto za Wizara ya Mambo ya Nje pia ni mazito sana na nyeti, na kadiri umakini, busara na mipango zaidi vitakavyowekwa katika suala hili, ndivyo matokeo bora zaidi yatakavyopatikana.
Katika muendelezo wa hotuba yake alieleza kuwa; mhimili muhimu zaidi wa mafanikio ya taasisi za utekelezaji na za utawala ni uwepo na ushirikiano wa wananchi wenye uelewa, na akasisitiza: Maadamu wananchi wataendelea kuwepo uwanjani, nchi itakuwa mbali na madhara.
Mtukufu huyo akisisitiza kwamba; kulinda uwepo huo kunahitaji kushughulikia kwa kweli matatizo yao, aliongeza: Maafisa wanapaswa kujua kwamba; wananchi wana wasiwasi na matatizo gani, na wachukue hatua za kivitendo kwa ajili ya kuyatatua. Matatizo mengi yaliyopo yanaweza kutatuliwa, lakini wakati mwingine baadhi yake hayapatiwi umakini unaostahili.
Ayatullah Makarim Shirazi, huku akiunga mkono shughuli na juhudi za serikali, alisisitiza: Sisi daima tunawaombea viongozi na tunaunga mkono hatua nzuri za serikali, lakini sambamba na hilo, matarajio na madai ya haki ya wananchi pia yanapaswa kupewa umuhimu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa mahusiano na nchi jirani na kusema: Katika mazingira ya sasa ambapo nchi inakabiliana na baadhi ya tawala za kibeberu na tabia zao zisizo za kimantiki, tunapaswa zaidi kuliko hapo awali kuhifadhi na kuimarisha mahusiano yetu na majirani, bila shaka kwa sharti kwamba wao pia waheshimu ujirani mwema.
Mtukufu huyo, huku akirejelea vita vya tatu vya kulazimishwa pamoja na uwepo wenye nguvu wa majeshi ya ulinzi katika Mlango wa Hormuz, aliongeza kusema: Inshaallah katika suala hili pia, kwa kuchukua hatua na mipango inayofaa huku tukihifadhi mafanikio ya medani, njama zote za maadui zitabatilika.
Mtukufu huyo, akirejelea umuhimu wa faradhi ya Hija, alisisitiza: Mwaka huu serikali ya Saudi Arabia imeweka vizuizi na masharti zaidi kwa mahujaji. Ni lazima mazungumzo ya kutosha yafanywe na serikali ya Saudi Arabia ili isiunganishe masuala ya vita na faradhi ya Hija. Hija ni suala linalojitegemea.
Ayatullah Makarim Shirazi pia huku akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi utambulisho wa Kiislamu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ina upande wa wananchi na pia upande wa Kiislamu, na haifai upande wowote kati ya hizi mbili kupuuzwa.
Pia alieleza kuwa; nafasi ya kujenga utamaduni katika kutatua matatizo mengi ya jamii ni muhimu sana, na akasisitiza: Masuala mengi ya nchi yanaweza kutatuliwa kupitia marekebisho ya utamaduni wa jamii, na taasisi kama redio na televisheni, shule na vyuo vikuu zinapaswa kutekeleza nafasi ya kiutendaji zaidi katika suala hili.
Mtukufu huyo pia alisisitiza umuhimu wa nafasi ya wafadhili katika kutatua matatizo ya jamii na alisema: Moja ya uwezo wenye thamani mkubwa wa nchi ni uwepo wa wafadhili ambao huingia katika medani ya kutoa huduma kwa motisha za kidini, na wanaweza kupunguza sehemu kubwa ya matatizo ya wananchi.
Ayatullah Makarim Shirazi mwishoni mwa hotuba yake, huku akieleza matumaini yake kwa mafanikio ya rais na serikali tukufu katika kutatua matatizo ya nchi, kuboresha mambo na kutekeleza majukumu yao ya kisheria, alisisitiza: Mimi katika swala zangu zote ninaomba dua kwa ajili ya ushindi dhidi ya maadui wa Uislamu, na ninatumaini kwamba vita hivi vya kidhalimu vitamalizika haraka iwezekanavyo kwa nusura ya Mwenyezi Mungu.
Maoni yako