Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, vyama na nguvu za kitaifa za Lebanon, chini ya anuani “Lebanon inayopinga, huru na yenye kujitegemea”, vilikusanyika katika makao makuu ya “Sindiketi ya Waandishi wa Habari wa Lebanon” mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Rabii Banat, rais wa “Chama cha Kisoshalisti cha Kitaifa cha Syria”, katika hotuba yake kwenye mkutano huo alisema: Imekuwa wazi kabisa kwamba diplomasia, katika mfumo uliotumika katika kipindi kilichopita, imeshindwa kuilinda Lebanon na kuhifadhi mamlaka yake; pia nguvu, katika nyakati nyingi, ilishindwa katika mtihani wa kubeba majukumu yake ya kitaifa, hasa pale ilipochagua mazungumzo ya moja kwa moja na kuacha karata yake pekee ya ushindi, ambayo ni muqawama.
Banat aliongeza: Hatutaki kubadilishwa utambulisho wa Lebanon, hatutaki kuanguka kwa nchi na kuvunjika kwa uthabiti wa ndani, na hatutaki kufanya Lebanon iwe Israeli.
Aliendelea kusema: Leo Lebanon inakabiliwa na chaguo la msingi: ima ibaki katika mfumo wa dola inayohifadhi mamlaka yake na watoto wake kuungana chini ya mwamvuli wa taasisi zake, ikiwa na karata zote za ushindi zilizopo, hasa muqawama; au iingie katika fitna ambayo itakuwa nguzo ya adui katika juhudi zake za kuipiga Lebanon.
Alisisitiza kusema: Njia yoyote ya kitaifa yenye kuwajibika lazima ianze kwa kuilinda ardhi na mwanadamu; ardhi ambayo mamlaka yake hayakiukiwi, na mwanadamu ambaye haachiwi peke yake chini ya shinikizo la migogoro. Hili linailazimisha dola kuwa na uwepo kamili kupitia taasisi zake zote, kuwa na nguvu kutokana na irada ya watu wake, na kuwa na uwezo wa kutekeleza jukumu lake kikamilifu, si kwa upungufu wala kwa masharti; si kuhifadhi chuki ya watu wake wala kuuza hatima ya Walebanon wote kwa mfanyabiashara wa kimataifa anayependa vita, damu na mgawanyiko.
Kukataa mazungumzo na adui na kushikamana na muqawama
Emile Lahoud, mbunge wa zamani, alisoma tamko la mwisho la mkutano huo, ambapo ilitolewa salamu na heshima kwa mashujaa wa muqawama wanaoandika visa vya ushujaa.
Pia alituma salamu kwa roho za mashahidi miongoni mwa wapiganaji, watoto wa taifa, waandishi wa habari, wahudumu wa afya, vikosi vya usalama, wafungwa na majeruhi waliotoa maisha yao katika njia ya kuitetea Lebanon, pamoja na kupongeza uthabiti wa wananchi waliolazimika kuacha nyumba na vijiji vyao kutokana na mashambulizi lakini wakaendelea kushikamana na haki ya kurejea na kuishi kwa heshima.
Tamko hilo lilisisitiza kwamba; kupinga ukaliaji na kukabiliana na uchokozi ni haki halali na ya kudumu kwa Lebanon, iwe ni serikali au wananchi, mbele ya uhalifu unaofanywa na adui “Israel”. Haki hii imejengwa juu ya misingi ya sheria za kimataifa, mkataba wa Umoja wa Mataifa, katiba ya Lebanon na Hati ya Taif. Ilielezwa kuwa muqawama ulitokana na ukaliaji na uchokozi huo, na hautasimama maadamu adui anaendelea na ukiukaji, vitisho na ukaliaji wa ardhi ya Lebanon.
Mkutano huo ulitangaza upinzani wake mkali dhidi ya kanuni ya mazungumzo ya moja kwa moja na adui “Israel”, kwa sababu chaguo hili halipatani na mahitaji ya kulinda mamlaka ya kitaifa wala maslahi ya juu ya Lebanon. Tamko hilo lilisisitiza kwamba; uamuzi huo haupaswi kujengwa juu ya kujitenga au uamuzi wa upande mmoja, kwani ni suala nyeti na la kimkakati linalohitaji mwafaka mpana wa kitaifa.
Mkutano huo pia uliwataka viongozi wa kisiasa wajiondoe mara moja katika mazungumzo ya moja kwa moja, hasa katika hali ya kuendelea kwa uchokozi na ukiukaji wa “Israel”.

Maoni yako