Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, “Muungano wa Al-Wafaa wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiriwa nchini Lebanon” ulieleza kwamba; kile ambacho Lebanon imeshuhudia ni hatua ya maamuzi, ambapo mizania ya nguvu ilijithibitisha kupitia ulinzi wa kishujaa wa wapiganaji wa muqawama kwa ardhi na watu, na kushikamana kwao na haki ya Lebanon katika kukabiliana na uvamizi na kulinda mamlaka yake; ambapo kwa kujitolea kwao waliweka mfano wa hali ya juu wa ustahimilivu na mapambano.
Muungano huu, katika taarifa iliyotolewa kwa wananchi wote wa Lebanon na hasa wafanyakazi na waajiriwa katika sekta mbalimbali, ulieleza kwamba; uthabiti huu haukuwa wa kujitenga na mambo mengine, bali uliibuka ndani ya muktadha wa ukamilishaji wa juhudi katika mhimili wa muqawama.
Muungano huo huku ukitoa shukrani na pongezi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jukumu lake la msingi na la kipekee katika kuiunga mkono Lebanon na muqawama wake, ulisisitiza kwamba; msaada huu—ikiwemo uungaji mkono wa kisiasa na kimkakati—umechangia kuimarisha ustahimilivu na kuthibitisha mizania ya kuzuia, na hata kufikia ushiriki madhubuti katika kusimamisha mapigano.
Muungano wa Al-Wafaa pia ulisifu ustahimilivu wa wananchi wa vijiji na miji ambao walikuwa waungaji mkono wa kweli wa muqawama, na ukatoa shukrani kwa uthabiti wao na kurejea kwao katika ardhi yao licha ya changamoto zote. Muungano huo ulisisitiza kwamba irada ya mataifa bado ndiyo kigezo cha msingi katika kukabiliana na uvamizi.
Muungano huu pia ulitoa salamu maalum kwa wafanyakazi na waajiriwa wa sekta mbalimbali, hususan wale wa sekta ya afya, huduma za uokozi na huduma za umma; ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na athari za uvamizi na walisimama katikati ya uwanja wa ustahimilivu pamoja na wananchi wao.
Muungano wa Al-Wafaa ulimalizia taarifa yake kwa kuonesha fahari kwa mashahidi waliopoteza maisha wakilitetea taifa, na kuwatakia majeruhi uponaji wa haraka.
Maoni yako