Jumapili 4 Januari 2026 - 13:38
Sifa tatu muhimu za serikali ya Amirul-Mu’minin (a.s.) kwa mtazamo wa mtafiti wa Ahlus-Sunna

Hawza/ Maulavi Ruhul-Amin katika hotuba zake alisisitiza kuwa; mwenendo na sera za Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali bin Abi Talib (a.s.), ni zaidi ya historia; ni mfano hai wa vitendo wa haki, uwajibikaji na kusimama dhidi ya dhulma katika uongozi wa leo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Maulavi Ruhul-Amin, mtafiti wa Kiislamu na Rais wa Taasisi ya AIMAI ya India, katika mazungumzo yake na Shirika la Habari la Hawza, alisisitiza kuwa maisha na sira ya Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali (a.s.), ni zaidi ya urithi wa kihistoria, na vinaweza kuwa mwongozo wa vitendo kwa uongozi na usimamizi wa jamii ya leo. Aliongeza kuwa kuzingatia haki, uwajibikaji na kusimama dhidi ya dhulma ni miongoni mwa mafundisho makuu ya Nahjul-Balagha na ni mifano ya kipekee ya jambo hili.

Unamuelezeaje Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali (a.s.), kama “kiongozi bora wa Kiislamu”?

Ruhul-Amin: Kwanza kabisa, nashukuru Shirika la Habari la Hawza kwa kunipatia fursa hii. Mtukufu Ali (a.s.) hakuwa tu mtawala wa kisiasa; alikuwa mfano hai wa uongozi unaojengwa juu ya haki na uchamungu. Kuna sifa tatu mashuhuri katika serikali yake zinazostahili kuzingatiwa:

1. Uongozi unaotegemea uchaji wa Mwenyezi Mungu: Mtukufu Ali (a.s.) alisisitiza mara kwa mara kwamba “uongozi lazima uambatane na uchaji wa kina kwa Mwenyezi Mungu,” na kwamba kila uamuzi uchukuliwe ndani ya mipaka ya taqwa na haki ya Mwenyezi Mungu.

2. Uhusiano wa karibu na wananchi: Mtukufu huyo alikuwa akienda sokoni binafsi, akichunguza bei, na kujua matatizo na mahitaji ya watu. Mwingiliano huu wa moja kwa moja ulikuwa msingi wa maamuzi ya haki na wa kujibu mahitaji ya jamii.

3. Kujitolea na uwajibikaji: Mtukufu Ali (a.s.) amesema: “Kabla ya kusikia kilio cha mtu dhaifu, mtawala anapaswa kujiuzulu kutoka kwenye wadhifa wake.” Mtazamo huu unaonyesha kiwango cha juu cha uwajibikaji na hisia za kijamii alizokuwa nazo. Katika serikali ya Mtukufu Ali (a.s.), haki ilikuwa mhimili mkuu wa sera kwa kiwango gani?

Ruhul-Amin: Haki ilikuwa uti wa mgongo wa serikali yake. Moja ya nyaraka mashuhuri za kihistoria ni barua ya Mtukufu Ali (a.s.) kwa Malik al-Ashtar, ambapo amesema wazi: “Jiepushe kuingilia mambo usiyokuwa na elimu nayo.” Barua hii inaonyesha kuwa haki haikuzingatiwa tu miongoni mwa marafiki na wafuasi, bali hata kwa maadui pia. Kwa mfano, kuna wakati fulani vazi la Mtukufu Ali (a.s.) lilipatikana katika duka la Myahudi. Kesi ilipopelekwa mahakamani na ushahidi wa kuthibitisha madai haukupatikana, hata ingawa hakimu alikuwa miongoni mwa walioteuliwa na Mtukufu Ali (a.s.), hukumu ilitolewa kwa faida ya Myahudi. Mtukufu huyo aliikubali hukumu hiyo bila kupinga. Huu ni mfano ulio wazi wa utekelezaji kamili wa haki na heshima kwa sheria.

Serikali ya Mtukufu Ali (a.s.) ni mfano adimu wa uongozi unaohamasisha, unaozingatia uchamungu, mawasiliano ya moja kwa moja na watu, na mshikamano thabiti na haki; mfano ambao si tu katika historia ya Uislamu bali pia katika dunia ya leo, ni kielelezo bora cha kiongozi na mtawala wa kibinadamu. Mtindo huu wa utawala unaonyesha kuwa haki na maadili katika siasa vinaweza kuwa nguzo imara ya jamii iliyo hai na yenye usawa.

Mtukufu Ali (a.s.) aliwezaje kudumisha uwiano wa kiuchumi na haki ya kijamii katika serikali yake?

Ruhul-Amin: Mtukufu Ali (a.s.) alisisitiza mara nyingi: “Mali ya nchi ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu.” Kwa mtazamo huo, aliweka mfumo wa mgawanyo wa haki wa hazina ya umma (Baytul-Mal). Hata katika kugawa mgao kwa wanafamilia, alizingatia kanuni zilezile za haki. Kwa mfano, wakati ndugu yake Mtukufu Ali (a.s.) alipodai mgao mkubwa zaidi, Mtukufu huyo alisema: “Je, unataka haki za watu zipotezwe?” Aliweka mgao maalumu kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi kama masikini, mayatima na wajane, na alitekeleza haki na uadilifu katika ngazi zote za utawala.

Kwa maoni yako, mafundisho ya kiuchumi na kijamii ya Mtukufu Ali (a.s.) yanaweza kutumika kwa kiasi gani leo hii hasa katika nchi za Kiislamu?

Ruhul-Amin: Mafundisho haya yanafaa sana na yanafungua njia. Ikiwa marais na viongozi wa leo watasoma barua na sera za Mtukufu Ali (a.s.) na kuzitekeleza, wanaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza rushwa, udikteta na ukosefu wa usawa. Mtukufu huyo alisema:

“Ikiwa mtawala atakuwa dhalimu, nchi itaangamia; usisaliti uaminifu wa watu, la sivyo kuanguka kwako ni hakika.”

Kanuni hizi ni ujumbe wa kimataifa kwa viongozi wa leo na zinaonyesha kuwa utawala usiozingatia haki na maadili hauwezi kudumu.

Kwa mtazamo wako, ni sifa gani kuu za kitabia za Mtukufu Ali (a.s.) ambazo viongozi wa leo wanaweza kujifunza?

Ruhul-Amin: Kuna sifa tatu kuu za Mtukufu Ali (a.s.) ambazo daima zinafaa kuigwa:

1. Elimu na hekima: Mtukufu Ali (a.s.) alitambulika kama “Bab al-Ilm” yaani “Mlango wa Elimu,” na maamuzi yake yote ya kiserikali aliyafanya kwa kuzingatia elimu, ufahamu na tafakuri ya kina. Mtazamo huu unaonyesha umuhimu wa elimu katika uongozi na uendeshaji wa jamii.

2. Ushujaa na kusimama dhidi ya dhulma: Ushujaa wake katika kukabiliana na dhulma na uonevu haukuwa na mfano. Kwa mfano, katika Vita vya Siffin, wakati jeshi pinzani lilipoziba njia ya maji na askari wakapata kiu, Mtukufu Ali (a.s.) alisema: “Maji ni haki ya wote.” Uamuzi huu ni mfano wa ujasiri wa kimaadili na mshikamano na haki hata katika mazingira magumu.

3. Haki na ukarimu wa nafsi: Mtazamo wa Mtukufu Ali (a.s.) kuhusu haki na tabia yake ya ukarimu ni mfano adimu kwa uongozi wa leo. Kuweka usawa na kuheshimu haki za wengine, hata mbele ya maadui, ni funzo muhimu kwa wasimamizi na viongozi duniani, na linaonyesha kuwa nguvu bila haki na maadili haiwezi kudumu.

Vijana wanawezaje kupata ilhamu kutoka katika maisha na sira ya Amirul-Mu’minin, Mtukufu Ali (a.s.)?

Ruhul-Amin: Vijana kwanza wanapaswa kusoma Nahjul-Balagha, moja ya kazi bora zaidi za fasihi na falsafa duniani. Mtukufu Ali (a.s.) daima alikuwa “rafiki wa vijana” na alikuwa na imani na uwezo, vipaji na nguvu ya kizazi kipya. Kutokana na maisha na sira yake, kuna masomo matatu ya msingi yanayoweza kuchukuliwa:

1. Uongozi ni uwajibikaji, si kutafuta starehe: Utawala na madaraka kamwe si chombo cha anasa binafsi, bali vinaambatana na kujitolea na uwajibikaji kwa watu.

2. Elimu na maarifa ni sharti la nguvu: Bila ufahamu na hekima, nguvu inaweza kusababisha maangamizi makubwa zaidi.

3. Jihadi kubwa zaidi ni kusimama dhidi ya udikteta na kutetea ukweli: Kukabiliana na dhulma na mamlaka ya kiimla kunahitaji ujasiri na mshikamano na misingi ya kimaadili.

Hitimisho

Mfano wa uongozi na utawala wa Mtukufu Ali (a.s.) si urithi wa kihistoria tu; bali ni mwongozo wa vitendo na muhimu kwa dunia ya leo katika siasa na uendeshaji wa jamii. Sira na maisha yake vinaonyesha kuwa serikali ya Kiislamu itakuwa thabiti na yenye mafanikio pale tu itakapoendeshwa kwa muungano wa haki, ubinadamu na hekima. Mafundisho ya Alawi yanathibitisha kuwa uongozi wa kimungu na wa kimaadili unaweza kutoa mfano wa kipekee wa kujenga jamii yenye haki, utu na uhai.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha