Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika mji wa Houmine al-Tahta, mlingano wa dhahabu wa “Jeshi, Taifa, Muqāwama” haujasalia kwenye kaulimbiu tu, bali ulijidhihirisha kwa vitendo, katika hafla tukufu ya kuaga iliyoandaliwa kando ya majeneza ya mashahidi: Shahidi Sajini Ali Hassan Abdullah (kutoka Jeshi la Lebanon) na mashahidi wawili wa jihadi, Hassan Khidr Issa na Mustafa Muhammad Ballout (kutoka Hizbullah), waliounganisha damu moja na hatima ya pamoja.
Hizbullah, kwa kuandaa hafla tukufu, iliwaaga mashahidi wake wawili wa jihadi. Katika hafla hiyo, kundi la wapiganaji wa jihadi, kwa kutoa kiapo cha uaminifu, walisisitiza kusimama imara katika njia ya kujitoa muhanga na kulinda wasia ulioandikwa kwa damu.
Katika taswira moja ya kitaifa, Jeshi la Lebanon pia, kwa ushiriki wa maafisa na wanajeshi wake, liliandaa hafla ya kumuenzi shahidi Sajini Ali Hassan Abdullah, ili kumheshimu yule aliyeuawa kishahidi katika njia ya kuilinda ardhi na heshima ya taifa.
Katika wakati wa mkusanyiko, miili mitakatifu ilikutanishwa katika eneo la msikiti. Sheikh Hani Ballout, Imamu wa mji wa Houmine al-Tahta, aliswalia miili ya mashahidi; tukio ambalo huzuni ilichanganyika na fahari, na machozi yakachanganyika na heshima, ili bendera ya utu na heshima ipae juu.
Katika hafla hiyo, Ali Fayyadh, mjumbe wa kundi la wabunge la “Uaminifu kwa Muqāwama” katika Bunge la Lebanon, alisema katika hotuba yake: Leo, damu takatifu za Jeshi shujaa la Lebanon, ambalo tunalithamini kwa misimamo ya busara ya uongozi wake, zimechanganyika na damu za Muqāwama jasiri; Muqāwama ambao wapiganaji wake wameutoa uhai wao katika kuilinda nchi na katika njia ya uhuru, kujitegemea na mamlaka yake.
Aliongeza kusema: Mashahidi watatu waliuawa kishahidi kutokana na usaliti na uhalifu uluofanywa na adui wa Kizayuni; adui anaeikalia kwa mabavu ardhi yetu, anaekiuka mamlaka yetu, anaewaua vijana wetu, na anayeharibu mali zetu, vijiji vyetu na nyumba zetu. Adui huyu haheshimu ahadi yoyote, makubaliano yoyote, azimio lolote wala sheria yoyote ya kimataifa; huvuka mipaka na kanuni zote, hueneza ufisadi na uharibifu ardhini, kisha kwa kutegemea uhalifu huu wote, anataka kutulazimishia masharti ya kusalimu amri na udhalili; masharti yanayowanyang’anya wakazi maeneo yetu ya mipakani, yanayopunguza mamlaka yetu na kunyakua rasilimali zetu.
Fayyadh alisisitiza: Mbele ya miili ya mashahidi wetu mashujaa, kwa heshima ya damu zao na kwa ahadi thabiti tuliyofunga kupitia shahada na kujitoa muhanga kwao, tunasema kwa uwazi kamili: Utawala huu utaendelea kubaki kuwa adui mnyakuzi na mhalifu, hata kama dunia nzima itautambua. Adui huyu anaweza kuendelea na mauaji na uharibifu, lakini kamwe hawezi kunyang’anya haki yetu ya kujilinda, kuilinda nchi na ardhi yetu, wala haki ya taifa la Lebanon ya kuishi kwa usalama, uhuru na utulivu; haki ambayo taifa la Lebanon linaitekeleza kupitia serikali yake katika kusimamia mamlaka juu ya ardhi, haki na rasilimali zake.
Alibainisha kuwa; lengo la Muqāwama kupitia kujitoa muhanga huku ni kuondoka Israel kutoka katika ardhi yetu, kusitishwa vitendo vya uadui dhidi ya watu na vijiji vyetu, kuachiliwa wafungwa wetu, na kutekelezwa haki yetu ya kujenga upya nyumba na maslahi yetu.
Akauliza kwa kusema: Kasoro au ajabu ya madai haya iko wapi, ilhali mara nyingi na kwa uaminifu tumesisitiza kushikamana na Azimio 1701 na tangazo la kusitisha mapigano?
Baadaye, Fayyadh aliitahadharisha Serikali ya Lebanon akisema: Adui anapoendelea kuwaua Walebanon, mazungumzo naye yana thamani gani? Na ikiwa anaendelea na vitendo na misimamo yake ya kuchochea mvutano, thamani ya kumpa misamaha ya bure ni ipi? Ni nini asili ya mazungumzo haya ambayo yanamruhusu adui kuzungumzia ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi, miradi ya kiuchumi, na muingiliano wa majukumu ya kisiasa na kiusalama?
Mjumbe huyo wa kundi la Muqāwama aliongeza kuwa; serikali ya Lebanon inapaswa kujibu maswali haya kwa uwazi kamili, na kusisitiza kwamba wawakilishi wake katika kamati ya utekelezaji watabaki kujikita katika misingi iliyotangazwa ya Lebanon pekee, nayo ni: kuondoka kwa Israel, kusitishwa kwa vitendo vya uadui, na kuachiliwa kwa wafungwa.
Alikosoa akisema: Badala ya serikali kuelekeza juhudi zake katika kutimiza madai haya ya msingi, baadhi wamechukua sera ya kutoa misamaha ya bure, na kwa pupa wanajadili suala la silaha kaskazini mwa Mto Litani; ilhali adui wa Kizayuni hajazingatia hata kifungu kimoja cha makubaliano ya kusitisha mapigano, na bado anazuia kukamilika kwa uenezaji wa Jeshi la Lebanon kusini mwa Mto Litani.
Aliutaja msimamo huo kuwa wa kushangaza na unaostahili kulaaniwa, kama kilele cha msururu wa makosa ya serikali; makosa ambayo hayajaleta matokeo yoyote katika kuwalinda Walebanon au kuikomboa ardhi. Akasema huu ni mwenendo usio wa busara na ni kuruka ombwe, wenye athari mbaya, na utasababisha zaidi kudhoofika msimamo wa Lebanon kwenye mazungumzo.
Maoni yako