Jumatano 24 Desemba 2025 - 22:00
Doria zilizofanywa na wanajeshi wavamizi wa Israel zaingia Quneitra na kufunga barabara

Hawza/ Vyombo vya habari vya Syria vimeripoti kuwa doria mbili zilizofanywa na jeshi la Israel zimeingia katika vijiji vya pembezoni mwa mkoa wa Quneitra, kusini mwa Syria.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, vyombo vya habari vya Syria vimetangaza kuwa doria mbili za kijeshi zilizofanywa na Israel zimeingia katika vijiji vya “Ain Ziwan” na “Al-Ajraf” vilivyoko katika maeneo ya kandokando ya mkoa wa Quneitra kusini mwa Syria.

Vyanzo vilieleza kuwa kundi moja la Israel liliyojumuisha magari 7 ya kijeshi lilianzia eneo la Tal Ahmar Magharibi, likapitia njia ya kijiji cha “Kudna” na kufika kijiji cha “Ain Ziwan”, ambapo waliweka kizuizi cha muda na kufunga barabara inayounganisha Ain Ziwan na kijiji cha “Suwaysa”, kisha wakaondoka katika eneo hilo.

Hata hivyo, kikosi cha pili kilichojumuisha magari 3 ya kijeshi aina ya “Hammer (Hummer)” na gari moja aina ya “Hilux”, kiliingia katika kijiji cha “Al-Ajraf” kilichoko katika eneo la kati la mkoa wa Quneitra, na kikaweka kizuizi cha muda kwa ajili ya kuwakagua wapita njia. Lakini kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Syria (Sana), waliondoka bila kumkamata mtu yeyote.

Baada ya kuanguka serikali ya rais wa zamani wa Syria, Bashar al-Assad, tarehe 8 Desemba 2024, jeshi la uvamizi la Israel limeongeza mashambulizi yake katika mikoa ya Daraa na Quneitra kusini mwa Syria.

Aidha, vyombo vya habari vya Syria viliripoti kuwa; mwishoni mwa Oktoba iliyopita maeneo ya kandokando ya kijiji cha “Kuya” pembezoni mwa mkoa wa Daraa kusini magharibi mwa Syria yalilengwa na vikosi vya Israel kwa makombora matatu tofauti ya mizinga.

Mtandao wa Al-Ikhbariyya wa Syria uliripoti kuwa; vikosi vya uvamizi vilishambulia kaskazini magharibi mwa kijiji cha Kuya kwa kutumia makombora matatu tofauti, huku shambulio hilo likiambatana na ufyatuaji wa risasi nyingi katika eneo hilo.

Mtandao huo ulisisitiza kuwa; huuu ni uchokozi mwingine mpya wa Israel unaoingia katika mlolongo wa mashambulizi ya mara kwa mara ambayo jeshi vamizi la Israel limekuwa likiyatekeleza katika wiki za hivi karibuni katika maeneo ya kusini, hususan pembezoni mwa Quneitra na Daraa; jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Kutenganisha Vikosi wa mwaka 1974, maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na misingi ya kuheshimu uhuru wa nchi na umoja wa ardhi zao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha