Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika Kombe la Kiarabu la mwaka huu huko Doha, sura isiyotarajiwa imevuta hisia za mashabiki wa Palestina na vyombo vya habari vya eneo hilo: Emilio Saba, mchezaji wa Peru mwenye mizizi iliyo imara Palestina, ambaye si tu ameonesha kiwango bora uwanjani, bali pia kwa unyenyekevu wake, utambulisho wake wa pande mbili na hamasa yake ya Kihispania (Latini), amekuwa chanzo cha msukumo kwa mashabiki wa Palestina.
Kombe la Kiarabu daima limekuwa jukwaa la kuonesha vipaji na simulizi mpya, lakini mwaka huu moja ya hadithi tofauti zaidi za mashindano haya imetokana na beki wa Peru mwenye umri wa miaka 23; mchezaji aliyekulia akiwa amevaa jezi nyeupe na nyekundu ya Peru, lakini moyo wake kwa miaka mingi ulikuwa kimya unadunda upendo wa Palestina, maelfu ya kilomita mbali.
Emilio Saba, aliyezaliwa Lima na kulelewa katika akademi za “Esther Grande”, “Sport Boys”, “Alianza Lima” na “Melgar”, ni miongoni mwa wanasoka ambao safari ya maisha yao haiwezi kufafanuliwa kwa soka pekee. Mwaka 2020 alipata uzoefu wake wa kwanza wa kitaalamu, lakini hatima ilikuwa imemwandalia jambo la kina zaidi: kupatanisha utambulisho wa pande mbili ambao kwa miaka mingi ulikuwa kimya ndani yake.
Kuitwa timu ya taifa ya Palestina ilikuwa ndio hatua ya mabadiliko katika safari hii; nchi ambayo baba yake, nyanyake na mababu zake walihama, na leo kizazi kipya kinaitetea kwa kuvaa jezi ya ardhi hiyo hiyo. Baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya “Euskadi”, kwa haraka akawa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Palestina, na katika Kombe la Kiarabu la mwaka huu, kwa maonesho yake ya kuvutia alileta shauku kwa mashabiki. Ushindi wa Palestina wa 1–0 dhidi ya Qatar na nafasi yake katika mechi hiyo, ilikuwa hatua iliyolifanya jina lake liwe maarufu miongoni mwa waandishi wa habari wa eneo hili.
Yeye mwenyewe anasema kuwa; kujiunga na Palestina haikuwa mshangao kwake: “Nimekulia katika utamaduni, chakula, mila na hata muziki wa Kipalestina. Daima ilikuwa nchi yangu ya pili; nchi inayounda mizizi yangu.”
Muunganiko huu wa kifamilia umemfanya asijisikie mgeni katika timu ya taifa ya Palestina, licha ya ukweli kwamba hajui Kiarabu: “Ninazungumza Kiingereza na wachezaji wenzangu wananisaidia sana. Kuanzia siku ya kwanza nilijisikia kama sehemu ya familia yangu.”
Hisia hii ya ukaribu inaonekana wazi hata katika chumba cha kubadilishia nguo cha Palestina. Uwepo wa Saba mwenye nishati yake ya Kilatini umeipa timu rangi na roho mpya.
Pamoja na yote hayo, Saba haisahau Peru na kumbukumbu zake. Akiwa na tabasamu pana mbele ya kamera anasema: “Salamu za kipekee kwa watu wa Peru. Nimeichezea timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 ya nchi yangu, na daima ninaipa heshima na upendo mkubwa.”
Hadithi hii haijawavutia mashabiki wa Palestina pekee; waandishi wa habari wa Peru pia waliitikia baada ya kuisikia simulizi yake. Juan Palacio Casas, mwandishi wa habari anayeishi Paris, alisema: “Hadithi hii inapaswa kusimuliwa; inastahili.”
Wakati huo huo, Sheila Vargas, mtaalamu wa michezo huko Lima, aliongeza: “Ni bora zaidi kwamba anacheza hapa. Nchini Peru vipaji haviungwi mkono ipasavyo, na hapa anaweza kung’ara.”
Leo Emilio Saba amebeba bendera mbili; bendera ya nchi aliyozaliwa na bendera ya ardhi iliyoijenga mizizi yake. Anatumaini kwamba safari hii italeta furaha zaidi kwa mashabiki wa Palestina na pengine, siku moja, hadithi yake itakuwa chanzo cha msukumo kwa kizazi kipya cha wanamichezo waliotokana na jamii za wahamiaji.
Maoni yako