Ijumaa 5 Desemba 2025 - 15:30
Jinsi ya Kujiepusha na Majivuno Wakati wa Mafanikio Makubwa

Hawza/ Wakati wa kufikia daraja za kidunia au kiakhera, hatari ya majivuno hutukabili; Imam Zaynul Abidin (a.s.) anatupa mwongozo wa kujilinda na hatari hii.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Imam Sajjad (a.s.) katika Sahifa Sajjadiyya humwomba Mwenyezi Mungu kwa maneno haya:

«اَللَّهُمَّ ... وَ لاَ تَرْفَعْنِی فِی النَّاسِ دَرَجَةً إِلاَّ حَطَطْتَنِی عِنْدَ نَفْسِی مِثْلَهَا؛ وَ لاَ تُحْدِثْ لِی عِزّاً ظَاهِراً إِلاَّ أَحْدَثْتَ لِی ذِلَّةً بَاطِنَةً عِنْدَ نَفْسِی بِقَدَرِهَا.»

Usinipandishe hadhi mbele ya watu isipokuwa unishushe kwa kiwango hicho hicho mbele ya nafsi yangu; wala usinijalie utukufu wa dhahiri isipokuwa unijalie unyenyekevu wa ndani kwa kadiri hiyo. (1)

Sherehe:
Mwanadamu katika maisha yake anaweza kufikia vyeo vya kidunia na kiroho. Kinachoweza kuwa balaa baada ya kufikia daraja hizi ni kiburi na kujiona.

Njia madhubuti ya kujikinga na balaa hii ni kujijengea roho ya mizani na uwiano ndani ya nafsi.

Kwa kuzingatia mafundisho ya Imam Sajjad (a.s.), tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu kwamba kwa kadiri tunavyopata izza (heshima) na kuinuliwa daraja— iwe ya duniani au ya akhera— pia atupe unyenyekevu, ili izza hiyo na udhilili huu viwe kama mizani mbili zinazolingana, na hivyo moyo wetu ubaki salama kutokana na kiburi na majivuno.

Mtu ambaye ataweza kufikia mizani hii ndani ya nafsi yake, anaweza kuwa miongoni mwa watu bora. Ndiyo maana Mtume Mtukufu (s.a.w.w) anasema:

«افْضَلُ النّاسِ مَنْ تَواضَعَ عَنْ رِفْعَةٍ.»

“Mbora wa watu ni yule anayenyenyekea kutokana na cheo alicho nacho.” (2)

Huyo ndiye anayeweza kuwa mfano wa kauli ya Imam Ali (a.s.) aliposema:


«ذُو اَلشَّرَفِ لاَ تُبْطِرُهُ مَنْزِلَةٌ نَالَهَا وَ إِنْ عَظُمَتْ کَالْجَبَلِ اَلَّذِی لاَ تُزَعْزِعُهُ اَلرِّیَاحُ»

“Mtu mwenye heshima hatetereki kwa cheo chochote akikipata, hata kiwe kikubwa sawasawa na mlima ambao upepo hauutikisi.” (3)

Na yule ambaye hawezi kujipamba kwa mizani hii hubadilika na kuwa mtu wa hali ya chini, kama alivyoeleza Amirul Mu’minin (a.s.):

«اَلدَّنِیُّ تُبْطِرُهُ أَدْنَی مَنْزِلَةٍ کَالْکَلاَءِ اَلَّذِی یُحَرِّکُهُ مُرُّ اَلنَّسِیمِ.»

“Mtu wa hali ya chini hupepesuka kwa cheo kidogo sana, kama jani la majani mwitu linalotikiswa na upepo mdogo.” (4)

Rejea:
1. Sahifa Sajjadiyya, dua ya 20.
2. I’lām al-Dīn, juzuu 1, uk. 337.
3. Ghurar al-Hikam wa Durar al-Kalim, juzuu 1, uk. 371.
4. Neno hili pia limenukuliwa katika kitabu hicho hicho.

Imeandaliwa na Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha