Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mufti na Imamu wa Msikiti wa As-Safaa, Hujjatul-Islam Sheikh Hasan Sharifah, amesema: “Wakati adui Mzayuni anapovunja nyumba za watu kusini mwa Lebanon na kwa mtindo wake wa kigaidi kuharibu maisha ya watu, jambo la kwanza linalokuja akilini mwa raia wa kusini ni hili: Serikali iko wapi?”
Amesema raia huyo anatarajia serikali kutimiza wajibu wake, kuonekana kwa vitendo, kuleta matumaini, na kumwambia raia wa kusini: “Wewe haupo peke yako.”
Sheikh Sharifah ameongeza kuwa, hali halisi ni ya maumivu makubwa, kwani kuonesha huruma pekee hakuwezi kumrudisha marehemu, kujenga nyumba iliyobomoka, kumponya majeruhi, wala kufidia hasara ya duka lililoungua au kubomoka. Amesema watu wanahitaji serikali inayowaunga mkono, si serikali inayotosheka na kutoa pole; wanahitaji viongozi wanaopanga mipango ya ujenzi upya, si wale wanaobobea tu katika kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari. Aliashiria kuwa, “misingi ya ustahimilivu haijengwi kwa maneno bali kwa matendo.”
Amesisitiza kuwa watu wa kusini hawahitaji huruma, bali wanataka ushirikiano katika kubeba maumivu na kushiriki katika ujenzi.
Sheikh Sharifah amepongeza wito wa Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, wa kuitisha mkutano wa kitaifa wa ujenzi upya, akisema kuwa; huo si mkutano wa kiufundi au wa kisiasa tu, bali ni kuigeuza dira ya taifa kuelekea upande wa kusini uliojeruhiwa.
Ameongeza kuwa, katika wakati huu nyeti wa kitaifa, ingepaswa badala ya kususia, watu waalikwe kushiriki, na badala ya kukwepa majukumu, watu waitwe kuyakubali. Amebainisha kuwa; katika kipindi ambacho misimamo imegawanyika kati ya ukimya na kusitasita, wito huu unadhihirisha umuhimu wa umoja wa hatima na kuamsha dhamiri ya serikali kwa wale wanaolipa gharama kwa damu na kwa nyumba zao.
Amesema kusini hakuhitaji hotuba, bali msimamo unaolingana na ukubwa wa kujitolea kwa wananchi wake.
Sheikh Sharifah ameashiria kuwa mazungumzo ya moja kwa moja ambayo Marekani na Israel wanayatangaza hayabadilishi ukweli wa mgogoro, bali yanajaribu kufunika hakika ya uvamizi.
Amebainisha kuwa “Marekani bado ni ileile — taifa lililofungwa na maslahi yake ya kidunia — na Israel bado ni ileile — kitu kimoja kilichojengwa juu ya ugaidi na upanuzi wa mipaka. Haitambui lugha nyingine isipokuwa nguvu, na wala mazungumzo hayawazuii, wala makubaliano hayaiwazibiti.”
Mwisho wa hotuba yake, Sheikh Sharifah amewaonya wale wanaokimbilia ndoto ya kuleta uhusiano na utawala wa Israel, akisema: “Warehemu mashahidi waliotoa nafsi zao katika ardhi hii, roho zao bado zinalinda heshima na utu wa kusini. Hakuna usawazishaji wa uhusiano na muuaji. Adui huyu anaelewa lugha moja tu — lugha ya kuzuiwa. Na mpaka atakapo kumbana na msimamo wa kudumu na ujasiri wa chuma, hatakoma kuvamia.”
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa; muqawama si chaguo la kifahari, wala la dharura, bali ni ngao ya kujilinda kwa ajili ya ardhi, heshima, na utu, na ndio dhamana ya mamlaka na dira ya uadilifu katika nyakati za udhaifu na kupuuzia wajibu.
Maoni yako