Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza A‘arafi katika hafla ya kufunga Kongamano la Kitaifa la “Sayansi za Kibinadamu za Kiislamu katika upeo wa Tamko la Hatua ya Pili ya Mapinduzi”, lililofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Hikma, Chuo Kikuu cha Qum, alisisitiza umuhimu wa elimu na utafiti pamoja na nafasi ya msingi ya falsafa na maadili katika maendeleo ya sayansi za kibinadamu na teknolojia. Alisema: Tunaiadhimisha Wiki ya Utafiti na Uchunguzi, na pia tunaheshimu Wiki ya Umoja wa Hawza na Chuo Kikuu, na tunapeleka salamu kuzielekea roho za mashahidi watukufu wa hawza na vyuo vikuu, mashahidi wa muqawama wa Kiislamu, mashahidi wa ulinzi mtukufu wa miaka minane na siku kumi na mbili, mashahidi wa chuo hiki na mashahidi wa Imam.
Ushauri wa kwanza wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika Tamko la Hatua ya Pili
Mkurugenzi wa Hawza aliendelea kusema: Ushauri wa kwanza wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika Tamko la Hatua ya Pili ni elimu na utafiti; na hili ni jambo muhimu sana. Nitapitia vifungu viwili au vitatu vya tamko hilo na kueleza hoja kadhaa.
Alisisitiza kuwa: Elimu na utafiti ndio chombo cha wazi zaidi cha heshima na nguvu ya nchi. Uso mwingine wa maarifa ni uwezo. Ustaarabu wa Magharibi, kutokana na elimu yake, uliweza kujipatia utajiri, ushawishi na nguvu ya takribani miaka mia mbili; na licha ya udhaifu katika misingi ya maadili na imani, kwa kulazimisha mtindo wa maisha ya Magharibi kwa jamii nyingine, uliudhibiti kwa kiwango kikubwa msafara wa elimu, siasa na uchumi. Katika kifungu hiki, nguvu na udhaifu wa msingi wa ustaarabu wa Magharibi vimeangaziwa: nguvu yake ni kasi katika kugundua ukweli na kufikia siri za ulimwengu na kuzitumia katika maisha; na udhaifu wake ni kwamba mti huu wa elimu ulikua katika ardhi isiyo na rutuba, bila kuzingatia furaha na mafanikio ya mwanadamu, na ulikuwa na matatizo katika misingi ya kifalsafa na mitazamo ya msingi.
Ayatollah A‘arafi aliongeza kuwa: Haipaswi kudhaniwa kwamba Magharibi ilipata utajiri na elimu hii bila falsafa; falsafa ilikuwepo. Falsafa iliyoanzia kwa Kant, ikaendelea kwa Descartes, hadi vipindi vya baadaye katika misingi ya falsafa ya jumla, falsafa mseto na mitazamo ya kifalsafa. Falsafa ya Kant, falsafa ya Descartes, Hume, Popper na wengineo, pamoja na falsafa mseto, zote zimeunda mfumo mkubwa wa falsafa ya Magharibi; lakini msingi huu baada ya Renaissance umevurugika, umekuwa na uwezekano wa kupingwa na umekumbana na udhaifu mpya.
Sayansi za Kibinadamu za Kiislamu ni msingi na roho ya Tamko la Hatua ya Pili ya Mapinduzi
Katika hitimisho la sehemu hii ya hotuba yake alisema: Hoja ya msingi inayopaswa kuzingatiwa ni kwamba sayansi za kibinadamu za Kiislamu ndizo msingi na roho ya Tamko la Hatua ya Pili ya Mapinduzi. Ingawa jina hili halikutajwa moja kwa moja katika tamko, lakini roho ya tamko inasisitiza kwamba sayansi za kibinadamu zinapaswa kuundwa katika muktadha wa fikra za Kiislamu. Hili ni jukumu la hawza na chuo kikuu, na halihusiani na sayansi za kibinadamu pekee; bali linamaanisha kuunda mtazamo wa Kiislamu na kifalsafa katika nyanja zote za kielimu.
Muungano wa sayansi za kibinadamu na za Kiislamu katika maendeleo ya ustaarabu
Mkurugenzi wa Hawza alisisitiza umuhimu wa muungano wa sayansi ya kibinadamu na ya Kiislamu katika maendeleo ya ustaarabu, na ulazima wa mwingiliano kati ya hawza na chuo kikuu, akisema: Kubuni mifumo mipya ya kiustaarabu bila muungano huu hakuwezekani.
Muunganiko wa fiqhi ya kisasa na falsafa na sayansi za kibinadamu za Kiislamu
Ayatollah A‘arafi alisisitiza ulazima wa mabadiliko ya kifiqhi na kifalsafa katika hawza na kuviunganisha na sayansi za kibinadamu za Kiislamu pamoja na chuo kikuu, akasema: Bila muunganiko huu, maendeleo ya kielimu ya nchi yatakuwa pungufu. Mimi nilikuwa nikifuatilia mada hii mara mbili hadi tatu kwa wiki, na niliona kwamba kila kinachofanyika katika uwanja huu ni kazi ya kina na yenye thamani.
Aliongeza kuwa: Muunganiko huu ni hitaji la lazima kwa fani ya fiqhi. Hata wale wasiofanya kazi ya fiqhi moja kwa moja wanapaswa kuunganishwa na mazingira haya na kunufaika nayo; kwa sababu kazi ya kielimu bila kuunganishwa na fiqhi na fikra ya ijtihadi huwa na athari ndogo na pungufu. Kwa sasa, Ofisi ya Fiqhi ya Kisasa katika hawza imepiga hatua nzuri na imewasilisha tafiti zenye thamani.
Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini pia alitaja uwanja wa falsafa na kusema: Uwanja wa falsafa na mwendelezo wake unahitaji kuimarishwa kazi ya kina ya ijtihadi. Mwaka huu, inatarajiwa, sawa na Ofisi ya Fiqhi ya Kisasa, kuanzishwa ofisi maalumu katika uwanja wa falsafa ili masomo ya kina ya ijtihadi katika falsafa, falsafa mseto na mwendelezo wa falsafa yaweze kuwa hai zaidi. Hii itajumuisha pia falsafa ya malezi, falsafa ya siasa na falsafa ya uchumi, ili mtazamo wa Uislamu, kwa njia ya ijtihadi na hikma, uwasilishwe katika tafiti hii. Hatua hii inalenga kupanua mipaka ya sayansi za Kiislamu na kuendana na mabadiliko ya sayansi za kibinadamu na sayansi nyingine, ili tafiti na vyanzo vya utafiti wa Kiislamu viende katika mwelekeo sahihi wa kielimu.
Maendeleo ya elimu za kibinadamu za Kiislamu na akili bandia
Aliongeza kuwa: Kwa mfano, katika uwanja wa akili bandia, kwa sasa kuna miradi mikubwa inayohusiana na ijtihadi na sayansi za utambuzi inayoendelea, ambayo inahitaji misingi imara ya kifalsafa, kikalamu, kifiqhi na kiitikadi. Miradi hii, licha ya kuwa na changamoto nyingi, inaonesha kwamba ushirikiano kati ya hawza na chuo kikuu ni muhimu katika kuendeleza elimu za kibinadamu za Kiislamu na teknolojia.
Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini alisisitiza: Uzalishaji wa nadharia za kielimu zenye ithibati katika sayansi za kibinadamu za Kiislamu na teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia, hauwezekani bila kujenga upya na kuimarisha misingi ya kifalsafa, kifiqhi, kikalamu na kimaadili; na ushirikiano endelevu kati ya hawza na chuo kikuu ni jambo la lazima.
Ayatollah A‘arafi aliendelea kusema: Akili bandia, ambayo imeunganishwa na elimu za utambuzi, ina misingi muhimu sana ya kifalsafa, kikalamu, kifiqhi na kiitikadi, na ina athari kubwa nchini. Kwa sasa, hawza na chuo kikuu vinapaswa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kufikiria mwingiliano kati ya akili bandia, teknolojia zinazohusiana na elimu za utambuzi na fikra za Kiislamu. Mwingiliano huu una ngazi nne hadi tano, ikijumuisha falsafa ya akili bandia kwa mtazamo wa Kiislamu, fiqhi na sheria ya akili bandia, maadili ya akili bandia, matumizi yake na athari zake katika uwanja wa elimu ya dini (theolojia) na kalamu. Hivi sasa, masomo nane ya kielimu katika uwanja huu yamebuniwa na yanafundishwa na watafiti.
Aliongeza: Bila mtazamo wa kina kuhusu fikra za sayansi za Kiislamu na bila kuzijenga upya na kuzikuza, haiwezekani kuzalisha nadharia za kielimu zenye ithibati katika uwanja wa sayansi za kibinadamu za Kiislamu na teknolojia mpya. Hili ni miongoni mwa masharti ya msingi ya maendeleo ya kielimu na utafiti wa nchi.
Maoni yako