Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kufuatia uchochezi wa wazi uliofanywa na imamu wa msikiti katika mji wa Hujayra dhidi ya Waislamu wa Kishia, mvutano wa kimadhehebu umeongezeka katika maeneo yanayozunguka jiji la Damascus. Hatua hiyo ilisababisha maandamano yaliyodai kufukuzwa kwa Waislamu wa Kishia katika eneo la Sayyida Zaynab (as), huku kukiwa na hofu kwamba hali hiyo inaweza kusababisha mapigano ya ndani.
Katika vitongoji vya Damascus, wimbi jipya la mvutano wa kidini linaendelea kuongezeka, likiwa na hatari ya mlipuko mkubwa wa machafuko. Imamu wa msikiti wa Hujayra amefanya propaganda za waziwazi dhidi ya wafuasi wa madhehebu ya Kishia katika eneo la Sayyida Zaynab (a.s) na amewahamasisha watu kufanya maandamano ya usiku. Hatua hii hatari — kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binadamu cha Syria, ambacho kina ushahidi wa sauti na picha — imeongeza hofu ya kuvunjika zaidi kwa muundo dhaifu wa kijamii wa mji mkuu na maeneo yake ya jirani.
Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binadamu cha Syria kimeripoti kuwa kina picha zinazoonesha mvutano wa kimadhehebu katika maeneo hayo pamoja na ushiriki wa moja kwa moja wa huyo imamu katika maandamano hayo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya taasisi hiyo, imamu huyo amekuwa na jukumu kuu katika kuamsha hisia za kimadhehebu na amewahamasisha watu kupinga kile alichokiita “kuenea kwa ushawishi wa Kishia” — jambo lililozua hofu kuhusu kurejea kwa migawanyiko ya kidini katika maeneo ya kusini mwa Damascus.
Jana, katika eneo la Sayyida Zaynab (a.s), kundi la watu lilifanya maandamano wakiwa na kauli zinazomlenga Sheikh Adham Al-Khatib — jambo lililotokea wiki moja tu baada ya yeye kukamilisha ukarabati na kufungua upya Husayniyya Al-Zahra.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binadamu cha Syria, maandamano hayo yalifanywa zaidi na baadhi ya wakaazi wa jiji hilo — hasa wahamiaji kutoka Joulan na mikoa mingine — ambao wanaamini kwamba kuwepo kwa Husayniyya kunachochea hisia za kidini, na wamemshutumu Al-Khatib kwa kuchochea fitna.
Sheikh Adham Al-Khatib ni mwakilishi wa Marja wa Kishia Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah, anayejulikana kwa msimamo wake wa wastani, wito wake wa umoja kwa Waislamu, na kuonya dhidi ya matusi kwa maulama au viongozi wa madhehebu mengine.
Wengi miongoni mwa wakaazi wa Kishia wanaamini kwamba mashambulizi dhidi ya Al-Khatib hayalengi mtu binafsi pekee, bali ni ishara ya kulenga uwepo wa Waislamu wa Kishia katika eneo hilo.
Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binadamu cha Syria kimeonya kwamba kuongezeka kwa hotuba za kibaguzi na za kuwatenga wengine kunaweza kuwa na matokeo hatari, na kimezitaka taasisi za kimataifa ziiombe serikali ya Syria ichukue hatua za kuzuia mienendo kama hiyo, na kuhakikisha uhuru wa itikadi na kuimarisha hali ya kuishi kwa amani baina ya madhehebu mbalimbali.
Mnamo tarehe 12 Agosti, Sheikh Adham Al-Khatib — imamu na khatibu wa msikiti wa Sayyida Zaynab (a.s) — alitoa khutba kali, akionya kuhusu “mashambulizi na ukiukaji” ambao Waislamu wa Kishia wa eneo hilo wamekuwa wakifanyiwa na watu wanaohusishwa na serikali.
Alisema kuwa matendo hayo yanajumuisha kuchukua nyumba za watu kwa nguvu, kuwafukuza wakazi, wizi wa mali, vitisho kwa kutumia silaha, matusi, kurusha mabomu madogo kwenye nyumba na magari, pamoja na unyang’anyi wa fedha nyingi — yote hayo yakifanyika kwa maneno ya kibaguzi ya kimadhehebu na ya matusi.
Maoni yako