Ijumaa 24 Oktoba 2025 - 12:36
Ijitihaidishaji wlya ubunifu na juhudi za kielimu za Mirza Nāīnī ni kielelezo kwa wanafunzi na watafiti wa Hawza

Hawza/ Ayatullah Subhānī alisema: Marehemu Mirza Nāīnī, kwa kutumia mbinu bunifu za kielimu katika fiqhi, kama vile kugawa kadhia katika vigawanyo vya kihakika (ḥaqīqiyyah) na vya kihalisia (khārijiyyah), na kwa kuunganisha elimu na maanawi, aliandaa njia iliyo wazi na yenye kuleta msukumo kwa taasisi za kielimu za Kiislamu na watafiti wa leo na wa kesho.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Subhānī, katika hotuba yake kwenye kongamano la kumbukumbu ya Mirza Nāīnī lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kiislamu cha Imamu Kādhim (a.s.), alisisitiza hadhi ya kielimu na kiakhlaqi ya mwanachuoni huyo mashuhuri na akaipitia historia ya miaka elfu moja ya Hawza ya Najaf. Alibainisha kuwa nafasi ya marehemu Nāīnī katika kuendeleza juhudi za kielimu na kiutamaduni za hawza ni muhimu mno, akasema:
“Kongamano hili kubwa limeandaliwa kwa lengo la kumheshimu mwanachuoni mkubwa aliyetoa huduma adhimu kwa jamii ya Uislamu na Ushia, na ambaye ametokana na mti wenye matunda mengi wa Najaf al-Ashraf.

Tukio hili limeambatana na kumbukumbu ya miaka elfu moja tangia kuanzishwa Hawza ya kielimu ya Najaf, ambayo ilianzishwa mwaka 147 Hijria, na sasa zimepita miaka elfu moja tangia kuanzishwa kwake.”

Akaongeza kwa kuashiria umuhimu wa kuchunguza maisha na kazi za marehemu ‘Allāmah Nāīnī:

“Kabla ya kujadili shakhsia ya Nāīnī, ni lazima pia tuitazame historia ya Hawza ya Najaf. Mwanzoni, Najaf ilikuwa mji mdogo wa jangwani, lakini kwa kupita muda, iligeuka kuwa jamii ya kielimu na kituo cha kulea wanachuoni. Hata kabla ya kuhama kwa Shaykh Tūsī, Najaf tayari ilikuwa na jamii ya kielimu, wakazi na wanavyuoni. Ibn al-Hajjāj al-Baghdādī, aliyefariki mwaka 391 Hijria — wakati Shaykh Tūsī alizaliwa mwaka 385 Hijria — anaashiria kuwa katika kipindi hicho Najaf ilikuwa na mashairi katika haramu na taasisi za kielimu. Vivyo hivyo, Sayyid ‘Abdulkarīm ibn Ṭāwūs katika kitabu chake Farḥat al-Gharī anasema kuwa; alitoka Baghdad kwenda Najaf na akatenga dirham elfu tano kwa ajili ya majirani wa haramu, jambo linaloonesha kwamba kulikuwa na wasomaji wa Qur’an na wanazuoni wa fiqhi mjini Najaf.”

Ayatullah Subhānī, akisisitiza juhudi za kielimu za Shaykh Tūsī, alisema: “Shaykh Tūsī, wakati maktaba yake ilipoteketea kwa moto, alihamishia sehemu kubwa ya vitabu vyake Najaf na akaweka katika mji huo kazi zake adhimu, zikiwemo tafsiri mashuhuri at-Tibyān. Kitendo hiki ni mfano bora wa jihadi ya kielimu na juhudi za kuhifadhi urithi wa fikra na utamaduni.”

Akiendelea kumtukuza Mirza Nāīnī, alisema: “Marehemu Mirza Nāīnī ni alama ya akili yenye jihadi na mfano wa faqihi mwana siasa katika zama za migogoro. Kurejea kwenye fikra zake ni kurejea katika akili, uhuru na ucha Mungu ndani ya mipaka ya dini. Kwa hivyo, kumheshimu mtu mkubwa kama huyu si tu ni kutekeleza wajibu wa kimaadili, bali ni kutoa utambulisho na uhai kwa jamii ya Kiislamu na hawza.”

Marja‘ huyu pia akigusia athari na maandiko ya kielimu ya marehemu Nāīnī alisema: “Marehemu Naīnī alikuwa na upeo wa kipekee katika fani za fiqhi, usul, kalam na elimu ya hadithi. Alikuwa na athari kubwa katika majlisi zote za kielimu za Najaf. Kazi zake, zikiwa na muundo wa ndani uliofungamana na hoja sahihi na roho ya ijtihadi, bado ni mwongozo kwa hawza na watafiti. Kuwakumbuka wanazuoni kama hawa ni kuwatia moyo wanafunzi, walimu na watafiti vijana, na kuweka njia ya mustakbali wa hawza katika mwendelezo wa njia ya wanafunzi wa kielimu wenye juhudi na basira, mfano wa Nāīnī.”

Mirza Naīnī: Mfasiri, Faqihi na Mbunifu wa Hawza

Ayatullah Subhānī, akisisitiza hadhi ya kielimu na kimaadili ya mwanachuoni huyo mashuhuri, alitambulisha maisha, kazi na ubunifu wake kama kielelezo kwa hawza za leo na za baadae, akasema: 

“Katika historia, Najaf imefanya mambo mawili makubwa ya kielimu:


Kwanza, uandishi wa Tafsīr at-Tibyān ya Shaykh Tūsī — tafsiri kamili ambayo kati yake na Tafsīr al-Mīzān hakuna umbali mkubwa. Kwa upande wa ukamilifu, ni kitabu kisicho na mfano. Shaykh Tūsī alitumia vyanzo vya maktaba za Najaf na akafaidika na elimu za fiqhi, hadithi na tafsiri vilivyokuwepo katika uandishi wa kazi hii ya thamani. Bila ya vyanzo hivyo, kitabu kama hicho kisingeweza kuandikwa. Wakati huo, Najaf ingawa ilikuwa ndogo, ilikuwa na shule na kiwanda cha elimu, na Shaykh Tūsī alianzisha hawza kubwa kwa ajili ya Waislamu wa Kishia.

Jambo kubwa jingine lililofanywa Najaf, ni kuandaa mazingira ya jihadi ya kielimu na kueneza ijtihadi. Mambo haya yalisababisha hawza ya Najaf kuwa kituo cha kielimu na kiroho cha kulea wanazuoni.”

Akaendelea kusema: “Maisha ya marehemu Mirza Nāīnī yanaweza kuchunguzwa kwa hatua kadhaa: kuzaliwa na utotoni mwake mjini Nāīn, maisha ya kielimu na uhamiaji wake kwenda Samarra na Najaf, kazi na maandiko yake, ibada na kusimama usiku, kujishughulisha kwake na siasa na mambo ya kijamii, ubunifu wake wa kifiqhi na kiusuli, na jumla ya mafanikio yake — ambayo kuyajadili kikamilifu kunahitaji kitabu maalumu na kamili.”

Ayatullah al-‘Udhma Subhānī alisema pia: Kuhusu mwaka wa kuzaliwa kwa marehemu Mirza Nāīnī, alisema kuwa kuna tofauti baina ya vyanzo mbalimbali, kwani baadhi vimetaja mwaka 1272 H, vingine 1277 H. Alizaliwa mjini Nāīn na maisha yake ya kielimu na kimatendo aliyaendeleza juhudi na utafiti ndani ya hawza za kielimu.

Akaongeza kwa kusisitiza umuhimu wa kuchunguza upya athari za kielimu na kimaadili za wakubwa wa hawza, kwa kusema:
“Maisha na maandiko ya marehemu Nāīnī ni kielelezo kisicho na mfano kwa wanafunzi, walimu na watafiti vijana. Kwa upeo wake wa kielimu, roho ya jihadi ya kielimu na uadilifu wa kimaadili, ameandaa njia iliyo wazi kwa hawza za kisasa.”

Maisha ya Kielimu ya Mirza Nāīnī — Kielelezo Kisicho na Mfano kwa Hawza

Mwalimu wa Hawza ya Qom, akifafanua hatua za maisha ya kielimu ya Nāīnī, masomo yake, uhamaji wake na kunufaika kwake na wanazuoni wakubwa wa Najaf na Samarra, aliutaja urithi wake wa kielimu na kimaadili kuwa ni mfano wa kuigwa kwa hawza na watafiti, akasema: 
“Alizaliwa Nāīn, na huko ndipo aliposomea masomo ya awali ya kielimu. Kisha mwaka 1293 Hijria alielekea Isfahan, ambako alisoma chini ya walimu wawili wakubwa — marehemu ‘Āshiq Muhammad Bāqir Dakkī na marehemu Kallbāsī. Nāīnī alikaa Isfahan takriban miaka kumi, na katika kipindi hicho aliimarisha misingi ya elimu yake.”

Akaendelea: “Baada ya Isfahan, alihamia Samarra — mji uliokuwa na hadhi kubwa ya kielimu wakati huo, ukiwa chini ya uongozi wa marehemu Mujaddid Shīrāzī. Alikaa Samarra hadi mwaka 1303 Hijria, akinufaika na mafunzo ya wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Baada ya kufariki kwa marehemu Mirza Shīrāzī, alibaki Samarra kwa takribani miaka miwili zaidi, kisha akarudi Najaf. Huenda pia alisafiri Karbala njiani, lakini sehemu kubwa ya masomo yake aliimalizia Najaf.”

Marja‘ huyo akaongeza kusema: “Tangu mwaka 1315 hadi 1355 Hijria, marehemu Nāīnī aliendelea na masomo na kufundisha Najaf. Katika kipindi hiki alinufaika sana na marehemu Shaykh Muhammad Kādhim Khurāsānī. Alishiriki katika majlisi za istiftā’ (maswali ya kifiqhi) na darsa zake, na yeye mwenyewe pia alifundisha na kulea wanafunzi wengi hadi akafikia hadhi ya juu ya kielimu na kijamii. Wanazuoni wamemuelezea marehemu Nāīnī kuwa alikuwa na upeo wa kielimu, ustadi katika fiqhi na usul, ubunifu katika ijtihadi, na alijulikana kwa maadili na hali ya kiroho. Walisisitiza kwamba hakuwa tu hodari katika kuelewa elimu za dini, bali pia alikuwa mstari wa mbele katika kuzifafanua na kuzifundisha, akilea wanafunzi wengi.”

Mitazamo ya Wanazuoni Kuhusiana na Marehemu Mirza Nāīnī

Ayatullah Subhānī akaendelea kusema: “Marehemu Shaykh Muhammad Kādhim Khurāsānī katika kitabu Tanbīh al-Ummah (mwaka 1322 H), pamoja na marehemu Shaykh ‘Abdullāh Mārzandarānī, wamethibitisha hadhi ya kielimu na kimaadili ya Nāīnī na wamemtambua kuwa ni mujtahid mkubwa na faqihi mwenye upeo mpana. Vilevile marehemu Muhsin Jabal-‘Āmilī, mwandishi wa A‘yān ash-Shī‘ah, amemtaja Nāīnī kuwa ni mwanachuoni mbunifu, faqihi wa usul, ‘ārif na fasihi, na amesisitiza ustadi wake wa kifasihi na kimaadili.”

Ayatullah Subhānī akaongeza: “Shakhsia ya kielimu na kimaadili ya Mirza Nāīnī ilikuwa adhimu kiasi kwamba haikuhitaji sifa wala pongezi. Wakubwa wa hawza na watafiti wa Najaf daima wamekiri fadhila zake za kielimu na kimaadili, wakisisitiza upeo wake wa elimu, ikhlāṣ yake, na juhudi zake katika masuala ya kijamii.”

Akaendelea kukumbusha kuwa: “Walimu wakubwa wa hawza, kama vile marehemu Shaykh Āghā Buzurg Tehrānī, katika maelezo yao kuhusu maisha ya Nāīnī, wamethibitisha hadhi yake ya kielimu na kimaadili. Nāīnī katika mikutano ya kielimu na darasa zake, kwa ikhlāṣ na juhudi zisizochoka, aliwalea wanafunzi wake na akawa mfano wa kuunganisha elimu na ucha Mungu.”

Mwanachuoni Ayekuwa katika kilele cha hofu kwa Mwenyezi Mungu

Ayatullah Subhānī, akizungumzia upande wa kimaadili na kiroho wa Mirza Nāīnī, alisema: “Katika ibada na tahajjud za usiku, daima alikuwa katika hali ya khofu na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu. Marehemu Nāīnī alionesha kwa vitendo kwamba kadiri elimu ya mtu inavyoongezeka, ndivyo khofu na unyenyekevu wake mbele ya Mola wake vinavyoongezeka. Kupitia ushiriki wake katika ibada na swala, alikuwa akiunganisha moyo na roho yake na Mwenyezi Mungu, na wanafunzi wake walinufaika na ukuu wa kiroho huo.”

Akaongeza: “Marehemu Nāīnī hakuwahi kupuuza masuala ya kisiasa. Katika kipindi cha Mapinduzi ya Katiba (Mashrūṭiyyah), kwa uchambuzi wa kina na kwa kurejea Aya za Qur’an na hadithi, aliepuka ushiriki wa kisiasa usio wa kisheria na ulio na upotovu. Alisisitiza umuhimu wa kulinda asili ya Kiislamu na dini ya katiba hiyo. Kwa misimamo ya kimantiki na ya kisheria, alikusudia kuhifadhi haki za wananchi na kuimarisha uadilifu katika jamii.”

Kisha akabainisha: “Mwaka 1340 Hijria, Nāīnī alitoa fatwa nchini Iraq akiharamisha kuingia kiharamu katika Bunge la Kiislamu, akasisitiza kwamba yeyote atakayehusika katika jambo hilo anakwenda kinyume na hukumu ya Mwenyezi Mungu, Sunna ya Mtume na njia ya Ummah. Hii inaonesha umakini na upeo wake wa kisiasa, na kwamba daima alizingatia mipaka ya kidini na kijamii.”

Ubunifu wa Mirza Nāīnī — Msukumo kwa Wanafunzi wa Leo

Ayatullah Subhānī alihitimisha kwa kusema: “Ubunifu wa kielimu na fikra wa Mirza Nāīnī ni chanzo cha msukumo kwa wanafunzi wa leo wa hawza. Kwa akili yake ya ijtihaadi, maadili yake, na juhudi zake zisizo na kikomo, ameacha urithi unaoendelea kuangaza njia ya elimu na ucha Mungu katika jamii ya kielimu.

Ayatullah al-‘Udhma Subhānī alisema: Kujifunza na kuchunguza kazi za Mirza Nāīnī kunadhihirisha kwamba yeye, kwa kutumia mbinu na funguo za kielimu alizozibuni, aliweza kutoa suluhisho thabiti na za kimatendo kwa masuala magumu ya kifiqhi na kimaadili. Ubunifu huu wake bado unaendelea kuwa chanzo cha msukumo kwa wanafunzi na watafiti wa leo ndani ya hawza.

Akaongeza kwa kukumbusha: “Marehemu Nāīnī alikuwa na kumbukumbu yenye nguvu ya ajabu na uwezo wa kipekee katika kukumbuka masuala na kutoa ushahidi mwingi kutoka katika vyanzo mbalimbali vya kifiqhi na kielimu. Kila suala lilipojadiliwa, Nāīnī kwa utulivu na fikra mpya, alikuwa akitoa hoja thabiti kutoka katika misingi na mitazamo tofauti. Uwezo huu unaonesha ukakamavu wa akili na umakini wa kielimu aliokuwa nao.”

Ayatullah Subhānī akaendelea kusisitiza: “Mizizi ya fikra za Nāīnī inarudi kwa walimu wake wakubwa, wakiwemo Mirza Shīrāzī na marehemu Sayyid Muhammad Fashārakī. Ingawa baadhi wana mashaka kuhusu ushiriki wa Nāīnī katika darsa za marehemu Fashārakī, ushahidi unaonesha kwamba alikuwa akihudhuria katika masomo yake na alinufaika na fikra na mbinu za kielimu za wanazuoni hao wakubwa. Ni muhimu kuelewa kwamba msingi wa maoni ya Nāīnī ulitokana na fikra za walimu wake, lakini yeye mwenyewe aliziendeleza na kuzitumia katika njia ya kipekee na bunifu. Mchanganyiko huu wa kunufaika na walimu na ubunifu binafsi ndio uliomfanya Nāīnī kuwa mwanachuoni kamili na mwenye nguvu katika nyanja za fiqhi, usul na siasa za kidini.”

Mwisho, Ayatullah Subhānī alisema: “Maisha ya marehemu Mirza Nāīnī ni mfano wa kuigwa wa muunganiko wa elimu, taqwa na uwajibikaji wa kijamii. Kuchunguza upya kazi na mwenendo wake ni chanzo cha msukumo kwa wanafunzi, walimu na watafiti vijana, na bila shaka mustakbali wa hawza utakuwa mwendelezo wa njia ya wanazuoni mashujaa wa kielimu na kimaadili kama Nāīnī.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha