Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi ya Iran, katika taarifa yake kuhusu mpango wa kusitisha mapigano huko Ghaza, imesisitiza kwamba Iran daima imekuwa ikiunga mkono kila juhudi inayolenga kusitisha mauaji ya kikabila na uhalifu wa kivita huko Ghaza.
Taarifa hiyo imesema: Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikikumbushia wajibu wa kisheria na wa kimaadili wa jumuiya ya kimataifa kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Ghaza kwa mujibu wa “Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948 wa Kuzuia na Kuwachukulia Hatua Wanaofanya Mauaji ya Kimbari,” pamoja na wajibu wa kisheria na wa kimaadili wa kila serikali kusaidia mapambano halali na ya kisheria ya taifa la Palestina kwa ajili ya kutimiza haki yao ya kujitawala na kujikomboa kutoka katika minyororo ya uvamizi, ubaguzi wa rangi na ukoloni unaofanywa na utawala wa Kizayuni daima imekuwa ikiunga mkono kila mpango unaolenga kusitisha mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu huko Ghaza, na kutoa mazingira ya kufanikisha haki ya kujitawala kwa taifa la Palestina.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikizingatia vipengele na athari hatari za mpango huu, na ikitoa onyo tena kuhusu kurudiwa kwa ukiukwaji wa ahadi na hujuma za utawala wa Kizayuni katika kutekeleza yale wanayoyasema — hasa kwa kuzingatia mipango yake ya upanuzi na sera za kibaguzi za kikabila — inasisitiza kwamba maamuzi yote kuhusu suala hili yako mikononi mwa watu na harakati ya muqawama ya Palestina. Iran itakaribisha kila uamuzi wao utakaolenga kusitisha mauaji ya kimbari ya Wapalestina, kuondoka kwa jeshi la uvamizi la Kizayuni kutoka Ghaza, kuheshimu haki ya kujitawala ya watu wa Palestina, kuruhusu kuingia kwa misaada ya kibinadamu, na kuanza upya ujenzi wa Ghaza.
Kusitishwa kwa uhalifu na mauaji ya kimbari huko Gaza hakutaondoa wajibu wa serikali na taasisi za kimataifa zenye mamlaka za kufuatilia kisheria na kimahakama uhalifu wa utawala wa Kizayuni, na kuwatambua na kuwashtaki waagizaji na watendaji wa uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Ghaza, kwa lengo la kumaliza hali ya kutoadhibiwa utawala wa Kizayuni kwa miongo kadhaa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kuelezea matumaini kwamba mazingira ya kutuma haraka misaada ya kibinadamu kwa watu wanyonge wa Ghaza yatapatikana, imetangaza utayari wake kushiriki katika jukumu hili.
Maoni yako