Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hutuba ya kiongozi wa Mapinduzi wa Irani ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرّحمن الرّحیم
والحمد لله ربّ العالمین والصّلاة و السّلام علی سیّدنا محمّد وآله الطّاهرین سیّما بقیّة الله فی الارضین
Ninatoa salamu kwa taifa lote tukufu la Iran, nimeona ni vyema kushirikiana na watu wetu wapendwa baadhi ya maelezo; kuna mada mbili au tatu ambazo sasa nitazifafanua.
Kabla ya kuanza katika jambo hili, naona ni muhimu kutoa pongezi kwa kuingia mwezi wa Mehr, Mwezi wa Mehr ni mwezi wa masomo, shule, elimu na vyuo vikuu, ni mwezi wa kuanza harakati za mamilioni ya vijana, barobaro na watoto kuelekea kwenye ujuzi na uwezo, hii ndiyo sifa mahsusi ya mwezi wa Mehr.
Mimi ninatoa ushauri kwa viongozi wetu wapendwa, hasa viongozi wa elimu na malezi, Wizara ya Sayansi, na ya Afya na Tiba, kwamba daima wazingatie thamani na umuhimu wa vipaji vya vijana wa Kiairani, vijana wa Iran wameonesha vipaji vyao katika elimu na katika masuala mengi mengine ya maisha.
Hapa nitawasomea takwimu hizi: katika mashindano mbalimbali ya wanafunzi duniani, hivi karibuni, licha ya matukio ya vita vya siku kumi na mbili na changamoto zilizokuwepo, wanafunzi wetu walipata medali arobaini tofauti, ambazo kati yake kulikuwa na medali kumi na moja za dhahabu. Hizi zina umuhimu mkubwa, zina thamani. Katika Olimpiadi walipata nafasi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi washiriki kimataifa, katika fani nyingine pia walipata nafasi nzuri, katika uwanja wa michezo pia, kama mnavyoona siku hizi; awali mpira wa wavu, sasa mieleka, vijana wetu wako hivi; kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu vipaji vyao ni vya kipekee mno; inapaswa kufaidika navyo.
Naona ni muhimu, katika siku hizi za kumbukumbu ya shahada ya mpiganaji mkubwa, Shahidi Sayyid Hasan Nasrallah, nimtaje. Sayyid Hasan Nasrallah alikuwa ni hazina kubwa katika ulimwengu wa Uislamu; si kwa Shia tu, si kwa Lebanon tu; bali alikuwa ni utajiri kwa ulimwengu wa Uislamu, bila shaka, utajiri huu haukupotea; bado upo; yeye ameondoka, lakini utajiri aliouasisi umebaki, hadithi ya Hizbullah ya Lebanon ni hadithi inayoendelea, haitakiwi Hizbullah kudharauliwa wala kusahaulika utajiri huu muhimu, huu ni utajiri kwa Lebanon na kwa wasiokuwa Lebanon pia.
Na ni muhimu pia kuwakumbuka mashahidi wa hivi karibuni waliouawa katika tukio la vita vya siku kumi na mbili — iwe ni makamanda wa kijeshi, au wanasayansi, au watu wengine waliofikia daraja ya shahidi katika tukio hili — na ninawapa pole za dhati kabisa kwwnye familia zao tukufu.
Lakini yale mambo ambayo nimeona yafaa kuyazungumza, ni mambo matatu:
Jambo la kwanza ni juu ya mshikamano wa taifa la Iran; ingawa yameshazungumzwa mengi kuhusu hili; mimi nataka kutoa nukta moja katika jambo hili.
Jambo la pili ni kuhusu suala la urutubishaji (ghināsāzī), kwamba nitoe ufafanuzi kuhusu utajirishaji huu unaozungumziwa na kurudiwa sana.
Na jambo la tatu ni kuhusu mazungumzo na Marekani, ambapo wenye kalamu na wenye kusema wamesema maneno mbalimbali; wengine wakiwa wanakubaliana, wengine wakipinga; wengine kwa hoja, wengine bila hoja, kuhusu hili pia, kwa kadiri ya uwezo, nataka kusema sentensi chache.
Ama kuhusu jambo la kwanza, yaani mshikamano wa taifa la Iran, neno langu la kwanza ni kwamba katika vita vya siku kumi na mbili, mshikamano wa taifa la Iran, umoja wa taifa la Iran, ulimkatisha tamaa adui; yaani adui, kuanzia siku za mwanzoni na katikati mwa vita, alitambua kwamba hatofikia malengo na makusudio aliyokuwa nayo, kusudio la adui halikuwa kuwaua makamanda; hilo lilikuwa ni nyenzo tu, adui alikuwa amefikiria kwamba kwa kuwaua makamanda wa kijeshi, na kuuwa baadhi ya shakhsia muhimu za mfumo, kutazuka machafuko nchini na hasa hapa Tehran, mawakala wao wangefanya fujo na ghasia na kuwaingiza mitaani, na kwa njia ya watu, kuunda tukio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, hilo ndilo lilikuwa lengo.
Kwa hiyo lengo lilikuwa ni Jamhuri ya Kiislamu; lengo lilikuwa ni kuutenganisha mfumo, ambao mimi katika hotuba nyingine nilisema kwamba hawa walikuwa hata wamekaa na kuchora ramani ya baada ya Jamhuri ya Kiislamu, na walikuwa wamepanga na kufikiri, walitaka kuunda fitna, kuunda fitna za mitaani, kuanzisha magenge na kung’oa mizizi ya Uislamu nchini; hilo ndilo lilikuwa lengo la adui.
Basi, lengo hili lilianguka hatua za mwanzo kabisa, makamanda walibadilishwa haraka, wengine waliteuliwa badala yao, na hali, nidhamu, mpangilio na kanuni za majeshi ya ulinzi vikabakia pale pale kwa uimara ule ule na kwa ari iliyo juu zaidi, lakini watu, ambao ndio kipengele chenye taathira zaidi, hawakuathirika kabisa na yale aliyotaka adui; maandamano yalitokea, barabara zikajaa watu lakini dhidi ya adui, si dhidi ya mfumo wa Kiislamu.
Watu walipeleka mambo hadi kufikia hatua ambapo adui, wale walioko nje ya mipaka, waliwaambia mawakala wao: «Wadhalili nyinyi! Sasa sisi ni nini kingine tungeliweza kuwafanyia ambacho hatukuwafanyia? Tumewaandalia mazingira, tumebomoa, tumewauwa watu kwa mauaji ya kigaidi, tumewaua; mbona hamfanyi chochote?». Hawa mawakala wao walioko Iran, mjini Tehran — ambao bila shaka wapo — walijibu wakasema: Tulitaka tufanye mambo fulani [lakini] watu hawakutujali, walitugeuzia mgongo; na viongozi pamoja na wale waliokuwa na jukumu la kulinda nidhamu ya nchi hawakuruhusu, walituzuia, na hatukuweza kufanya chochote. Hivyo basi, mpango wa adui ukashindwa vibaya.
Naam, haya niliyoyasema, baadhi yake au yote tumewahi kuyaeleza, au wengine wamekwisha kuyaeleza, nukta ninayotaka kusisitiza ni kwamba sababu hii bado ipo; sababu ya mshikamano wa taifa la Iran bado ipo, kuna watu — ambao chimbuko lao ni nje ya nchi, kwa mujibu wa habari zilizotufikia — wanataka kuonesha kana kwamba ule mshikamano uliojitokeza mwanzoni mwa vita vya siku kumi na mbili na kipindi kilichofuata, ulikuwa wa muda huo tu; baada ya siku chache utadhoofika, migawanyiko itaibuka, tofauti za maoni zitatawala, na mshikamano huo utatoweka; watu wa Iran watatawanyika, na hivyo wataweza kutumia ufa wa kikabila, kutumia tofauti za kisiasa, na kuwasukuma Wairani kugombana wao kwa wao, wakazue machafuko na fujo! Hivyo ndivyo wanavyotangaza.
Ninataka niseme wazi kwamba maneno haya ni upotoshaji mtupu. Ndiyo, katika masuala ya kisiasa tofauti za mitazamo zipo; na sisi tuna makabila mengi nchini ambayo yote ni Wairani, na yanajivunia Uiran wao; haya yapo, lakini mbele ya adui, jumla hii yote ni kama ngumi moja ya chuma thabiti inayoshuka moja kwa moja juu ya kichwa cha adui, leo hali iko hivi, jana ilikuwa hivi, na kesho pia, kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, itabaki hivi, Iran ya leo na, inshallah, ya kesho, ni ile ile Iran ya tarehe 23 na 24 Khordad, ile ambayo watu walijaa mitaani na kutoa kauli dhidi ya Mzayuni aliyelaaniwa na Marekani muhalifu, hili ndilo suala la kwanza nililotaka kulizungumzia. Nukta yake ni hii: mshikamano wa kitaifa, umoja wa watu, bado upo na utaendelea kuwepo; na bila shaka sote tuna wajibu mbele ya jambo hili.
Nukta ya pili ni suala la «urutubishaji» (غنیسازی). Katika mazungumzo na majibizano ya Wizara ya Mambo ya Nje na pande za kisiasa, neno urutubishaji limekuwa likitajwa mara kwa mara. Wao hulizungumza kwa namna fulani, nasi tunalizungumza kwa namna nyingine, ndani ya nchi pia, katika mijadala mbalimbali, neno hili hutajwa mara nyingi, nataka nitoe ufafanuzi mfupi kuhusu urutubishaji, kabisa, urutubishaji ni nini? Ni nini kinachofanya kuwa jambo la umuhimu kiasi hiki? Mazungumzo yote yanaelekezwa kwake: urutubishaji wa uranium.
Ninataka niseme: urutubishaji ni neno moja tu, lakini ndani yake kuna kitabu kizima cha maana, nitatoa dondoo chache tu, ikiwa wataalamu katika nyanja hizi watazungumza na wananchi kuhusu jambo hili, itakuwa vizuri na inafaa.
Urutubishaji wa uranium unamaanisha kwamba wanasayansi na wataalamu wa fani hii huuchukua uranium ghafi — ambao migodi yake ipo hapa Iran — na kwa juhudi kubwa za kiteknolojia ngumu na za hali ya juu, huubadilisha kuwa mada yenye thamani kubwa sana, inayokuwa na athari katika nyanja nyingi za maisha ya watu, hii ndiyo maana ya urutubishaji, yaani kitu kinachochimbwa ardhini, kwa teknolojia tata, kwa juhudi kubwa, kwa utaalamu wa hali ya juu na kwa stadi mahsusi, hugeuzwa na kuwa mada ambayo ndiyo uranium iliotajirishwa; huufikisha katika viwango tofauti vya urutubishaji, na mada hii huwa na athari pana katika maisha ya watu. Watu hunufaika kwayo na hutumia uranium iliyorutubishwa katika nyanja nyingi za maisha, zikiwemo: kilimo, ambacho kinaathirika kwa kiasi kikubwa; viwanda na uzalishaji wa malighafi; lishe, inayohusiana moja kwa moja na kilimo; mazingira na rasilimali asilia; pia katika utafiti, elimu, na tafiti za kielimu; na zaidi ya yote, katika uzalishaji wa nishati ya umeme, ambapo manufaa yake yako wazi kabisa.
Leo katika nchi nyingi zilizoendelea, mitambo ya kuzalisha umeme huendeshwa kwa uranium; ilihali sisi mitambo yetu mingi tunaendesha kwa petroli na gesi, ambavyo vina gharama kubwa, na zaidi vinachafua mazingira na hewa, lakini umeme unaozalishwa kwa uranium iliyorutubishwa na mitambo ya nyuklia hauna uchafuzi wowote wa mazingira, gharama zake ni ndogo mno, maisha ya mitambo yake ni marefu mno, na una faida nyingine nyingi ambazo wataalamu wanapaswa kuzielezea.
Waelezee watu kwa undani. Kwa mtazamo wangu, tukifika tukiandika orodha ya matumizi mbalimbali ya uranium iliyorutubishwa, itaibuka orodha ndefu sana.
Hadi sasa tusingelikuwa na teknolojia hii muhimu; hatukuwa na uwezo wa urutubishaji, maadui walikataa kutupatia, na hakuna mwingine aliyeturuhusu, mameneja wachache wenye dhamira thabiti na wanasayansi waliowajibika — kwa maana ya kweli — waliianza kazi ya urutubishaji wa uranium hapa nchini zaidi ya miongo mitatu iliyopita, na waliileta hadi mahali ilipo leo, leo tunaelekea kiwango cha juu katika utajirishaji wa uranium, Bila shaka, nchi zile zinazotaka kutengeneza silaha za nyuklia zinaweza kufikisha usafi hadi asilimia tisini; sisi, kwa kuwa hatuna hitaji la silaha na sisi tumeamua kuwa bila silaha za nyuklia, hatukufikia kiwango hicho; tulifikia hadi asilimia sitini — kiwango cha juu sana, kinachostahili pongezi na kinachotumika kwa baadhi ya mahitaji yetu ya kitaifa; mpaka hapa tumeweza kufanikiwa. Sisi ni moja ya nchi kumi duniani zenye uwezo huu; yaani, kati ya nchi za dunia zaidi ya mia mbili, nchi kumi zina uwezo wa urutubishaji, na moja ya hizo ni Iran ya Kiislamu.
Kwa kuwa nchi nyingine tisa zinamiliki pia bomu la nyuklia, sisi ni tofauti kwa kuwa hatuna bomu la nyuklia na hatukutaka kuwa nalo wala hatutekelezi matumizi ya silaha ya nyuklia — lakini tunao urutubishaji. Sisi tumejihakikishia nafasi miongoni mwa nchi kumi zinazobobea katika sekta hii; na wale wanasayansi niliyowataja ndio walioweka misingi ya kazi hii; walitumia pesa nyingi, lakini muhimu zaidi walileta kizazi kikubwa cha watu waliopata mafunzo katika nyanja hii. Huo ni ujumbe imara tulioupokea kutoka kwa wahusika — ripoti thabiti na ya kuaminika: leo ndani ya nchi kuna makumi kadhaa ya wanasayansi na waliofundishwa wa kiwango cha juu, mamia ya watafiti, na maelfu ya wahitimu wa vikosi vya nyuklia katika taaluma mbalimbali zinazohusiana, wote wakiendelea na kazi zao, watu hawa walikuja na kujenga taasisi fulani ambazo baadaye zililipuliwa kwa mabomu; tatizo ni kwamba hiyo ni sayansi — sayansi haianguki kwa mabomu wala kwa vitisho; sayansi haianguki; ipo. Nilisema na ninarudia: Makumi ya wanasayansi mahiri na walimu wenye ujuzi, mamia ya watafiti, na maelfu ya wahitimu wa kazi tofauti za nyuklia — kwa mfano, nimesitisha kutaja matumizi ya nyuklia katika tiba; tiba ni moja ya matumizi muhimu ya urutubishaji nyuklia, katika fani mbalimbali za tiba kuna wengi wanaofanya kazi; vivyo hivyo katika sekta ya kilimo, viwanda na shughuli nyingine mbalimbali — wote wanaendelea kufanya kazi na kutoa jitihada.
Katika miongo iliyopita, tunapofanya kazi hizi hapa nchini, kumekuwa na shinikizo kubwa juu yetu — juu ya Iran, juu ya viongozi wetu, juu ya serikali zetu — wakitaka kwa shinikizo hilo Iran iache kazi hizi; lakini sisi hatukukata tamaa wala hatutakata tamaa katika jambo hili, na katika masuala mengine yote, hatukukubali kushinikizwa na hatutakubali. Sasa upande wa Marekani umeweka msimamo mkali: kwao Iran haistahili kuwa na urutubishaji; hapo awali walisema tusiwe na urutubishaji wa kiwango cha juu, au tusihifadhi bidhaa za urutubishaji ndani ya nchi — vitu ambavyo hatukukubali, sasa wanasema kabisa msiwe kabisa na urutubishaji. Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba mafanikio haya makubwa ambayo taifa letu limejitahidi kuyapata, kuwekeza, na kuvumilia taabu nyingi ili kuyafikia si sawa na hakuna kitu! Hiyo ndio maana ya kusema «kutokuwa na urutubishaji». Hakika, taifa lenye ghera kama taifa la Iran halitaikubali kauli kama hiyo; halitakiwi kuikubali, hilo ni pia jambo lililotajwa kuhusu urutubishaji.
Na sasa suala la tatu: suala la mazungumzo na Marekani, katika usemi wa watu wa siasa, mada ya mazungumzo na Marekani inatajwa mara kwa mara; mitazamo ni mchanganyiko, nilisema baadhi wanaona hilo linafaa na ni muhimu; wengine wanadhani ni hatari; wengine wako katikati, ninachokielewa, nimekiona, nimehisia na nimepata uzoefu mwaka baada ya mwaka, nitatamka kwa taifa letu tukufu.
Nawaomba viongozi wa siasa na wanasiasa wayatie akilini; wafikirie kwa makini maneno haya, wazame, na wahukumu kwa msingi wa maarifa na ujuzi kisha ndio watoe taarifa, neno langu ni hili: kwa hali ilivyo sasa — mtu anaweza kusema miaka ishirini au thelathini ijayo hali itabadilika; hilo ni suala tofauti — kwa hali iliyopo sasa, mazungumzo na serikali ya Marekani, kwanza kabisa, hayatakuwa na msaada kwa maslahi yetu ya kitaifa; hayatatuletea faida yoyote, wala hayatamkatisha adui yoyote dhidi yetu; yaani ni jambo lisilo na faida, bila faida kwa taifa,
pasi na kuzuia madhara; kabisa haina athari hiyo. Hilo ndilo la kwanza.
Pili, kwa upande mwingine kuna hasara ambazo zitajitokeza. Yaani, faida hakuna kabisa, na kama kile nilichosema pili ni kwamba mazungumzo na Marekani katika hali ya sasa yanaweza kuleta madhara makubwa kwa taifa, ambayo baadhi yao huenda yakawa yasiyoweza kurekebishwa; kuna aina hiyo ya hasara, sasa nitayafafanua haya.
Lakini tulipo sema hayatuletei faida ni kwa sababu upande wa Marekani tayari ametangulia kuamua matokeo ya mazungumzo; yaani ameeleza kuwa anataka mazungumzo ambayo lengo la mwisho litakuwa kusitishwa kwa shughuli za nyuklia na urutubishaji hapa nchini Iran. Hii inamaanisha tuketi mezani mwa mazungumzo na Marekani lakini matokeo yatakuwa yale waliyoyasema wao «lazima yafanyike»! Hiyo si mazungumzo tena; ni agizo, ni kulazimisha; umetakiwa kukubali kujadiliana na upande ambao matokeo ya mazungumzo lazima iwe yale anayotaka, yale anayoagiza! Je, hayo ni mazungumzo? Mwendesha mazungumzo anavyosema leo hivi, anasema tujadiliane na matokeo ya mazungumzo yawe kwamba Iran isiwe na urutubishaji! Hivi sasa, mtu huyo alisema urutubishaji; siku chache kabla yake, makamu wake alitangaza kwamba Iran inapaswa isiwe na makombora pia! Sio makombora ya muda mrefu tu; hata makombora ya kati hayastahili kuwepo, hata makombora ya muda mfupi hayastahili kuwepo! Hii inamaanisha Iran iwe mikono yake imefungwa kabisa, ili ikiwa itafanyiwa mashambulizi hata haiwezi kujibu hata kambi ya Marekani huko Iraq au sehemu fulani; hiyo ni maana ya kauli hizi; «tujadiliane ili lile nalo liwe matokeo»! Hilo si tija; ni mazungumzo ambayo hayana faida kabisa kwetu—yote ni hasara; hayo ndio matokeo ya mazungumzo ya aina hiyo, Hayo si mazungumzo; ni ubabe, ni kutenzwa nguvu na Marekani, Mtu anayeitazama Iran kwa namna hii, kutoa matarajio na kauli za aina hii, ni mtu ambae hajui taifa la Iran; haijui Jamhuri ya Kiislamu; hajui falsafa na mwelekeo wa Iran; kwa kutokujua wao huongea hivi; kama tunavyosema sisi, «maneno haya ni makubwa kuliko mdomo wa msemaji», na kauli ya kusema «tujadili hili» kwa ajili ya jambo la namna hiyo haiwezi kupewa uzito, hivyo basi, kwao si faida kwetu.
Na kuhusu hasara—nilisema kuna hasara. Hilo ni la muhimu zaidi, upande wa pili umetishia kwamba ikiwa hamtajadiliana, kutakuwa na matokeo fulani—kulipuliwa mabomu, kutafanywa mambo fulani; maneno haya yanasemwa kwa njia isiyo wazi kidogo na kwa uwazi kidogo; ni tishio: «au mjadiliane au tutafanya hivyo na hivyo!» Sawa, kukubali mazungumzo ya namna hiyo kunamaanisha kukubali tishio kwa Iran ya Kiislamu. Ikiwa mtaingia katika mazungumzo kwa sababu ya tishio, maana yake tunataka kusema kwamba tunahofia mara moja mbele ya tisho lolote, tunatetemeka na tunauogopa upande mwingine na tunaunyenyekea; hii ndiyo maana yake, ikiwa hali ya kukubali tishio ikaja, haitakuwa na mwisho. Leo wanasema ikiwa mtakuwa na urutubishaji tutafanya hivi; kesho wanasema ikiwa mtakuwa na makombora tutafanya hivyo; kisha watasema ikiwa mtashirikiana na nchi fulani mtapigwa; ikiwa mtashirikiana na nchi nyingine mtapigwa! Tishio litakuwa la kudumu na tutalazimika kurudi nyuma kila mara mbele ya tishio la adui, yaani maana ni kwamba kukubali mazungumzo yenye tishio hakuna taifa lenye heshima litakalofanya hivyo, wala mwanasiasa mwenye busara hatayakubali, hivyo hali iko hivi.
Pande pinzani pia, labda, wanasema wanataka watoe fadhila fulani kwa upande wetu! Huo ni uongo. Kile wanachoahidi kama fursa ni uongo, miaka kumi nyuma tulitia saini mkataba na Marekani ambao ndani ya nchi yetu huitwa «برجام». Katika mkataba huo ilikubaliwa kwamba sisi tufanye mambo fulani kuhusu nyuklia—tufunge kitu fulani cha uzalishaji; ile bidhaa ya asilimia tatu na nusu tuliyokuwa tukitengeneza wakati huo iondolewe au ichanganywe ili isibaki, iondolewe urutubishaji wake; na mambo mengine—wakati huo wao pia walisema wataondoa vikwazo vyao, na baada ya miaka kumi faili la Iran katika Shirika la Nishati ya Nyuklia la Kimataifa (IAEA) litarudi kuwa la kawaida.
Sasa, wakati ule walikuja mbele yetu wakisema «miaka kumi», mimi nikasema «miaka kumi ni muda mrefu sana, kwa nini mkubali miaka kumi?» wakasema hivi na hivi, lakini hatimaye walikubali «miaka kumi». «Miaka kumi» imekamilika hivi karibuni; ile miaka kumi ambayo walipewa kama muhula wa kurekebisha hali ya faili la Iran la nyuklia ndani ya IAEA imekamilika hivi karibuni.
Ebu leo angalieni: si kwamba faili limekuwa la kawaida tu — la hasha — bali matatizo ya masuala ya nyuklia yameongezeka hadi kufika Baraza la Usalama, Umoja wa Mataifa, na katika masuala ya nyuklia yamezidi kuongezeka; yamezidi mara kadhaa! Hivyo ndivyo upande wake ulivyo; hilo ndilo alilosema! Sisi tumefanya kazi zote tulizotakiwa tufanye, lakini wao hawakuondoa vikwazo; wala hawakutekeleza ahadi yoyote waliyotoa, na baadaye kabisa wao walivunja, kwa kusema ya kawaida, mkataba huo au makubaliano yaliyoamuliwa — waliingia kabisa nje ya Barjam na kukataa kabisa.
Ikiwa mtafanya mazungumzo na adui na kukubali yale anayotaka, basi hilo ni kukubali na kuonyesha udhaifu wa nchi na kuharibu heshima ya taifa; ikiwa mtakubali tisho lake ambalo anawatishia, basi ndivyo itakuwa; kama msikubali mtabaki kama ilivyo sasa, ile migogoro itabaki. Hivyo basi, mazungumzo haya hayatoshi kuwa mazungumzo sahihi, tusisahau uzoefu; tusisahau uzoefu wa miaka kumi iliyopita, msemo wetu wa msingi ni Marekani; kwa sasa sitotaka kuingia katika mjadala kuhusu Ulaya.
Upande ule kwetu una tabia ya kukiuka ahadi zote, kuongopeana kila wakati, kutegemea udanganyifu; mara kwa mara hutishia kwa kutumia nguvu za kijeshi; wanapotaka hufanya uhalifu wa kuuawa kwa watu, kama walivyomfanyia shahid, Jenerali Suleimani; au huzipiga kwa mabomu taasisi zenye shughuli za nyuklia; wanapoweza hufanya hivyo. Hali ya upande huo ni ile; siwezi kuzungumza nao kwa uaminifu na kwa matumaini ya kutimiza ahadi na makubaliano.
Kwa mtazamo wangu, mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya nyuklia, na pengine kuhusu masuala mengine pia, ni zamu wazi ya kukosa njia — ni njia ya msongamano wa kutofaulu kabisa; hakuna njia sahihi iliyo wazi kwa masuala hayo, ni ngumu kabisa, waangalie, wafikirie, bila shaka mazungumzo hayo yanamfaa rais huyo wa sasa wa Marekani; atajisifu duniani kwamba alishaitisha Iran na kuileta mezani; atajivunia heshima hiyo, lakini kwetu sisi ni hasara kabisa; hakuna faida kwetu.
Na kile ninachotaka kusema hatimaye ni hiki: tiba ya maendeleo ya taifa ni kuwa imara; lazima tuwe wenye nguvu. Ukomavu wa kijeshi unahitajika, ukuaji wa kisayansi unahitajika, uimarishaji wa serikali, muundo na muundo wa taasisi unahitajika, watu wetu wenye akili, raia wenye maarifa na moyo wa dhati wanapaswa kukaa pamoja, wapate njia za kuimarisha taifa, na wazifuate njia hizo, tukifanya hivyo, adui hatatishia tena; akiona kwamba upande mwingine ni wenye nguvu hata hatatishia, kwa mtazamo wangu hakuna njia nyingine.
Tunahitaji kumuomba Mwenyezi Mungu Msamaha, kumtumainia Mwenyezi Mungu, kutawasali kwa Maimamu watoharifu (as) ili wawe wakubali kutuombea na kutusaidia, kisha tuweke juhudi za kitaifa na, inshallah, tusonge mbele kikazi, Na hili, kwa ridhaa ya Mwenyezi Mungu, litafanikiwa.
والسلام علیکم ورحمة الله وبرکاته
Maoni yako