Jumamosi 20 Septemba 2025 - 20:34
Vitabu vya masomo ya Hawza viwe vinaendana na mahitaji ya zama hizi

Hawza/ Mtukufu Ayatullah Subhani amesema: “Kwa muda wa miaka hamsini hadi sitini sasa tumefikia hitimisho kwamba ndani ya Hawza za kielimu, vitabu vya masomo vinapaswa kuwa vinaendana na mahitaji ya zama hizi.”

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatullah H'aj Sheikh Ja‘far Subhani, katika kikao alichokutana na Rais wa Jami‘at al-Mustafa al-‘Alamiyyah kilichofanyika katika Taasisi ya Kielimu na Utafiti ya Imam Sadiq (a.s), alisema:
“Jami‘at al-Mustafa inabeba jukumu kubwa sana, na insha-Allah matokeo yake yatakuwa yenye kung’aa sana.”

Akaendelea kubainisha kuwa:

“Kwa muda wa miaka hamsini hadi sitini sasa tumefikia hitimisho kwamba ndani ya Hawza vitabu vya masomo vinapaswa kuendana na mahitaji ya zama hizi, huenda si kila mwanafunzi wa dini kutoka sehemu mbalimbali duniani anayekuja hapa na kutaka kujisomea kwa miaka michache kisha kurudi kufanya kazi za kiutamaduni ataweza kufahamu undani wa fiqhi, na wala si lazima hivyo, inawezekana kutumia baadhi ya vitabu ambavyo vina ukamilifu, lakini vikiwa na lugha rahisi na ya kisasa zaidi.”

Ayatullah Subhani akaongeza kusema:

“Kwa lengo hili, tumeandika vitabu viwili: al-Mujaz na al-Wasit, ambavyo tumefanya jitihada visiwe vigumu ili wanafunzi waweze kufaidika kwa urahisi, ni vyema pia wanafunzi wa kimataifa wakapatiwa fursa ya kunufaika navyo wakati wa masomo yao.”

Mwanzoni mwa kikao hiki, Hujjatul Islam wal-Muslimin Ali Abbasi, Rais wa Jami‘at al-Mustafa al-‘Alamiyyah, akielezea furaha yake kwa kukutana na Ayatullah Subhani, alitoa maelezo kuhusu idadi ya wanafunzi, namna ya usajili na matawi ya Jami‘at al-Mustafa.

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi (Majlis Khobregan Rahbari) akaendelea kufafanua kwamba: “Mpaka sasa karibu vitabu 30 vya Mtukufu Ayatullah Subhani vimetafsiriwa na wanafunzi wa al-Mustafa kwa lugha mbalimbali, na kwa upande wa idadi ya vitabu vilivyotafsiriwa miongoni mwa vitabu vya wanazuoni, vitabu vyako vimeshika nafasi ya kwanza.”

Hujjatul Islam wal-Muslimin Abbasi akisisitiza juu ya umuhimu wa kutumia vitabu hivyo kama maandiko ya kimasomo katika Jami‘at al-Mustafa, alisema:
“Tunajitahidi kuhakikisha wanafunzi wa al-Mustafa wanapata urahisi zaidi wa kufikia kazi hizi adhimu za kielimu na kuweka mazingira bora ya kunufaika kwao na vitabu hivi.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha