Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Raji kufuatia kuanza kwa harakati ya kimataifa ya Sumud, aliandika barua akiwahutubia washiriki wa harakati hii na ikachapishwa kwa lugha kadhaa.
Barua muhimu ya Hujjatul-Islam Raji kwa msafara wa Uhuru wa Ghaza, maelezo yake ni haya:
Enyi wapigania uhuru! Enyi wapiganaji wasio na mipaka! Enyi mliojenga jeshi kubwa kutoka mashariki hadi magharibi, kutoka kaskazini hadi kusini! Angalieni uwanja huu, historia kama Karbala imerudia kufufuka, na ninyi kwa jeshi ambalo si kwa mapanga yaliyooza ya ubeberu na uliberali, bali kwa imani thabiti na moyo uliojaa mapenzi kwa wanyonge, mmeingia uwanjani, ninyi, watu wa mataifa mbalimbali, madhehebu tofauti, rangi na lugha tofauti, lakini mna lengo moja: “Kuvunja minyororo ya Kizayuni inayoinyonga Ghaza!”
Enyi wasafiri! Mistari yenu mirefu ya kujiandaa kuelekea Ghaza inakumbusha safu za kuelekea kwenye medani za damu za haki dhidi ya batili. Mmesimama imara, macho yenu yakiwaka moto na nyoyo zenu zikiwa na matumaini. Meli zenu ambazo si za biashara ya kidunia, bali kwa ajili ya kubeba mzigo wa kujitolea na msaada kwa kaka na dada zenu Wapalestina zinajiandaa. Ninyi ni wafuasi wa Nuhu, Ibrahim na Musa; mkiwa mmepanda majahzi, katikati ya moto, bahari mtaipasua ili kufika pwani ya Ghaza na kuuvunja mzingiro.
Enyi mashujaa! Mnaojua roho zenu zipo hatarini! Naam, mnajua kwamba Wazayuni wakatili, kwa manowari na makombora yao, wameweka mitego. Mnajua kwamba huenda damu yenu itamwagika juu ya mawimbi ya bahari, kama damu ya mashahidi wa msafara wa Uhuru kuelekea Ukanda wa Ghaza mwaka 2010. Lakini mnahofia nini? Ninyi ni jeshi la Hizbullah ya kimataifa! Hizbullah ambayo haipo tu Iran, Iraq, Yemen, Lebanon na Syria, bali pia katika moyo wa kila mwanadamu huru. Mmesimama kidete upande wa wanyonge wa Palestina, kama wafuasi wa Hussein (as) waliokuwa Karbala na wakasema: “Haitatupasa fedheha!” Harakati yenu hii si tu kuvuka bahari; hii ni mwanzo wa mwisho wa utawala wa Kizayuni muuaji wa watoto, hii ni kuuvunja mzingiro wa Ghaza; mzingiro ambao kwa miaka mingi umewaacha watoto wakiwa na njaa, akina mama wakiwa wamefiwa, na wanaume wakiwa mateka.
Enyi msafara wa uhuru! Ninyi ambao kutoka Marekani hadi Iran, kutoka Ulaya hadi Afrika, kutoka Asia hadi Amerika ya Kusini; Waislamu, Shia na Sunni, Wakristo na watu huru, nyote mmefika kusema: Ghaza haiko peke yake! Na kazi yenu ni tamu mno; pale mnapopakia misaada, chakula kwa wenye njaa, maji kwa wenye kiu, dawa kwa waliojeruhiwa, mavazi kwa watoto mayatima. Lakini zaidi ya hayo, meli zenu ni wabebaji wa ujumbe: ujumbe wa muqawama wa kimataifa dhidi ya dhulma. Baada ya muda mchache, boti na meli zenu zitasafiri; matanga yamepandishwa, mitambo ikivuma, na nyoyo zenu zikijaa dhikri “Ya Hussein” na “Ya Quds”.
Na wewe ewe Ghaza! Ewe Quds tukufu! Ewe Palestina shujaa! Jeshi hili, kama mawimbi yanayochemka, linakuendea. Wazayuni watikisike, Marekani na washirika wake waingiwe na hofu; kwa sababu hii ni mwanzo wa Tofanu-l-Aqsa ya kimataifa. Kuvunja mzingiro, si kwa silaha za kisasa, bali kwa azma za chuma, hawa ni wanaotafuta shahada; wako tayari damu zao ziwe maji yanayonywesha mti wa uhuru.
Na ninyi enyi mataifa huru! Ikiwa mioyo yenu inapiga kwa ajili ya wanyonge, simameni na kutangaza harakati yao, toeni sadaka kwa ajili yao na kuwaombea dua.
Na wewe, ewe Mkombozi wa ulimwengu, ewe tumaini la wanyonge wote wa dunia, wewe ambaye Masihi atakuja pamoja nawe, hongera kwenu kwa kuwa na jeshi hili la zama za mwisho; jeshi hili ni jeshi lako, marafiki kutoka pande zote za dunia; matumaini yao yapo kwako, wawe wanaokujua au wasiokujua, lakini matumaini ya mioyo yao yanakuita, wale ambao historia daima itawakumbuka kwa wema na ukuu, na Mwenyezi Mungu ndiye msaidizi wa wanyonge wote duniani.
Mdogo wenu,
Sayyid Muhammad Husayn Raji
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kistratejia ya Saada
Maoni yako