Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Hajj Shaykh Ja‘far Subḥānī, katika hafla ya ufunguzi wa mwaka wa masomo 1405–1404 H.S, alisema:
Sherehe zinazofanyika katika nchi zote za Kiislamu — isipokuwa kwenye maeneo yenye wafuasi wa Uwahhabi — zinajulikana kwa jina la sherehe za kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w). Wapinzani wa sherehe hizi hudai kuwa ni bid‘a, wakisema kwamba katika zama za Mtume hakukuwa na jambo kama hili, na wamejitahidi mno kulipinga.
Kuhusu maana ya “Bid‘a” Ayatullah Subḥānī aliendelea kusema: Lazima kwanza tufafanue maana ya “bid‘a”. Bid‘a ni jambo ambalo halina dalili yoyote katika Qur’ani na Sunna — hili ndilo sharti la kwanza. Sharti la pili ni kwamba jambo hilo liingizwe kama “dini”, yaani lifanywe kama hukumu ya kidini. Kwa hivyo, baadhi ya mambo kama michezo ya sasa, ambayo ni halali na mubāḥ, kilinganisho cha kilugha yanaweza kuitwa “bid‘a”, lakini kwa kuwa hayafanywi kama dini, hayahesabiwi kuwa bid‘a ya kisheri‘a. Kwa hiyo lazima masharti haya mawili yaangaliwe: kwanza, jambo lisitokane na Qur’ani na Sunna, na pili, lifanywe kama dini. Sherehe za kuzaliwa Mtume (s.a.w), kwa bahati nzuri, zina mizizi yake katika Qur’ani na pia zina ushahidi katika riwaya.
Akieleza kuhusu sifa kumi za Mtume zilizotajwa katika Qur’ani Tukufu na hasa aya ya 157 ya Sura al-A‘rāf: “Basi wale waliomuamini, wakamheshimu na wakamsaidia…”, alisema:
Wafasiri wengi wamechukulia maneno “عَزَّروه” (wakamheshimu) na “نَصَروه” (wakamnusuru) kuwa na maana moja. Lakini si hivyo. “عَزَّروه” ni kumheshimu na kumtukuza, na “نَصَروه” ni kumnusuru na kumsaidia. Sasa swali langu ni: je, mikusanyiko ya Waislamu katika nchi mbalimbali kwa mnasaba wa kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w), ambako husomwa aya za Qur’ani na riwaya zinazomhusu Mtume, na hakuna kosa lolote la kisheri‘a, si mfano halisi wa aya hii? Bila shaka ni mfano wake. Ibn Fāris, msomi mkubwa wa lugha, amesisitiza kwamba kila mzizi wa neno una maana yake mahsusi, hivyo “نصر” (msaada) si sawa na “عزر” (heshima).
Upendo kwa Mtume ni msingi wa imani
Ayatullah Subḥānī alisisitiza: Upendo kwa Mtume (s.a.w) ni moja ya misingi mikuu ya Uislamu, ikiwa mtu ataishi kwa kufuata Qur’ani na Sheri‘a lakini akawa na chuki moyoni mwake kwa Mtume, huyo ni kafiri. Na hata kama hana chuki lakini hana umuhimu wala heshima kwa Mtume, basi si muumini wa kweli, Upendo kwa Mtume ni nguzo ya imani. Kwa hivyo, tunaposoma aya na hadithi kuhusu Mtume, tunadhihirisha upendo wetu wa ndani, upendo si jambo la moyoni pekee; hata kuonyesha upendo kwa vitendo ni ibada, hivyo, aya hizi pamoja na hadithi sahihi ndizo dalili madhubuti kwamba sherehe hizi si bid‘a, bali ni sehemu ya dini yenyewe na zina mizizi ya Qur’ani na Sunna.
Ayatullah Subhani aliendelea kusema: Vile vile imekuja katika aya:
“{Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha}
[Surah At-Tawbah: 122]
Wafasiri wametaja maana tatu. Lakini zote zina mushkeli wa kurudisha dhamiri zote katika rejeo moja. Hata hivyo, baadhi ya riwaya zinaonyesha maana ya nne: kwamba aya hii haihusu tu Madina, bali pia miji mingine kama Ṭā’if na Makka. Hivyo basi, katika zama hizi inaweza kufasiriwa kwa miji kama Kerman na Bam. Yaani, ni wajibu kwa baadhi ya watu wa miji hiyo kuondoka, wakajifunze dini kwa kina, kisha warudi kwa watu wao ili wawatahadharishe, hii ndiyo maana ya kweli ya aya, na kwa njia hiyo tatizo la wafasiri linatatuliwa.
Na akahitimisha kwa kusema: Kwa hivyo, aya hii haimhusu Mtume na Madina pekee, bali inahusu maeneo mengine pia, Mwenyezi Mungu ametupatia neema hii ya kuwa na Hawza imara na thabiti pamoja na walimu wakuu na mashuhuri, hii ni neema kubwa mno, na ni jukumu letu kuithamini, kuienzi, na kuifanyia kazi ipasavyo.
Maoni yako