Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawadi Amuli katika moja ya hotuba zake alizungumzia mada ya “Falsafa ya Wilayatul-Faqiih na athari zake” mada ambayo tunawasilisha kwenu kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
Mwishoni mwa Suratul Maida, kuna masuala kadhaa yaliyotajwa, na kati yake yapo maswali mawili muhimu kuhusiana na Wilayatul-Faqiih, ambayo nitayabainisha kwa muhtasari.
Swali la kwanza:
Je, Wilayatul-Faqiih inalingana na demokrasia na uhuru au la?
Hakika, uhuru ni kanuni takatifu, yenye kuheshimiwa na yenye kukubalika kiakili, hata hivyo, maamuzi na chaguo la mtu kwa mujibu wa akili na pia kwa mujibu wa mantiki ya uhuru, huwa na mipaka; kwa sababu hakuna taifa lolote ambalo wananchi wake ni huru kabisa bila ya kujali sheria.
Kila jamii ina sheria inayotawala, iwe ni sheria ya mtu mmoja mmoja, au sheria iliyowekwa kwa ushirikiano na wataalamu (yaani mfumo wa watu kwa ajili ya watu), au iwe ni sheria ya Mwenyezi Mungu, kwa vyovyote vile, kila taifa lina sheria, na uhuru wa watu huwa na maana ndani ya mipaka ya sheria hiyo.
Uhuru katika Uislamu:
Ikiwa uhuru utatafsiriwa kwamba mtu ana hiari isiyo na kikomo hata mbele ya sheria, jambo hilo halikubaliki kiakili na pia halipo kivitendo, lakini ikiwa uhuru ni kuishi ndani ya mipaka ya sheria, basi watu wako huru kabisa, na hakuna mfumo wowote unaounga mkono aina hii ya uhuru kama Uislamu.
Kwa hivyo, Muislamu anapokubali Uislamu na kuifahamu Qur’ani na Ahlulbayt kama msingi wa sheria, hawezi kudai uhuru wa kuikataa Qur’ani, badala yake, anajiona kuwa ni mja na yuko chini ya uongozi wa Qur’ani na Ahlulbayt, na si huru kutoka humo.
Wilayatul-Faqiih si uongozi juu ya watoto au waliopungukiwa akili:
Wapo wanaopinga Wilayatul-Faqiih kwa kudhani kuwa “wilaya” ni uongozi juu ya watu waliopungukiwa akili au watoto wadogo, hivyo wakisema, ikiwa faqihi ana wilaya juu ya watu, basi watu hao ni wendawazimu au wasio na uwezo. Hii ni dhana potofu, Wilayatul-Faqiih si ya aina hiyo, uongozi wa faqihi ni uongozi juu ya watu wenye akili, hekima na maarifa.
Qur’ani inasema: “Hakika kiongozi wenu ni Mwenyezi Mungu, Mtume wake na wale walioamini, ambao huswali na hutoa sadaka hali ya kuwa katika rukuu.” (ikimrejelea Imam Ali a.s).
Kwa hivyo, wilaya hii ni juu ya wenye akili na imani, Faqihi, kama mwakilishi wa Imam Maasumu wakati yupo ghaiba, anaongoza kwa misingi ya Qur’ani na Sunna.
Uhuru na heshima katika mfumo wa Wilayatul-Faqiih:
Katika Uislamu, walii na wananchi wote wako sawa mbele ya sheria ya Mwenyezi Mungu, Faqihi mwenyewe yuko chini ya sheria hizo, lakini tofauti na sheria za kibinadamu zinazoweza kubadilika kwa mujibu wa masharti, Qur’ani na Sunna havibadiliki, sheria hizi ndizo msingi mkuu, na zote – kiongozi na wananchi – lazima wazifuate, kwa mfano, katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, cheo cha waziri mkuu kiliondolewa baada ya kugundua kuwa kinasababisha matatizo katika usimamizi wa nchi, hii ilikuwa mabadiliko ya sheria ya kimaumbile (katiba), si kinyume na sheria ya dini.
Umuhimu wa ushiriki wa wananchi:
Hata kama kiongozi ni mtu kama Imam Ali (a.s), ikiwa watu hawatamkubali na kushirikiana naye, serikali itashindwa, historia imeshuhudia hilo, Hivyobasi, uhalali wa faqihi unatokana na dini, lakini utekelezaji wake unategemea ridhaa na ushirikiano wa watu.
Kwa mfano, kama alivyo marjaa wa dini – anapokuwa na sifa zinazohitajika, anakuwa na uwezo wa kutoa fatwa, watu wakimfuata, wanafanya uwezo wake wa kisheria uonekane kivitendo, lakini hawampi cheo, cheo hicho kimetolewa na Sheria Takatifu.
Vivyo hivyo, Wilayatul-Faqiih siyo uwakilishi kutoka kwa watu, bali ni nafasi iliyowekwa na Mwenyezi Mungu, na watu wanapokubali, nafasi hiyo inatekelezwa kijamii.
Uislamu na uhuru:
Uislamu umefuta mfumo wa utumwa wa kijahiliya na umeweka mfumo mpya wa uhuru na heshima ya mwanadamu, Mtume (s.a.w.w) katika hotuba ya ufunguzi wa Makka alitangaza kwamba Mwenyezi Mungu ameondoa majivuno ya kijahiliya na ubaguzi wa kikabila, hakuna Mwarabu aliye bora kuliko asiye Mwarabu, wala asiye Mwarabu aliye bora kuliko Mwarabu.
Uislamu uliweka haki kwa mateka wa vita na njia nyingi za kuwaachia huru, miongoni mwazo ni kuweka kuwakomboa mateka kama kafara ya baadhi ya madhambi, katika mfumo huu, mtumwa ana haki zake za kibinadamu na za kidini; anaweza hata kuwa imam wa sala ikiwa ni mwadilifu, lakini tajiri au bwana fasiki hana haki ya kuongoza sala, kwa hivyo, Uislamu umeondoa utumwa wa kijahiliya na badala yake umeweka mfumo wa haki, heshima na uhuru wa kweli.
Maoni yako