Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, kwa kuzingatia kukaribia kwa siku za Arbaeen ya Hussein, kila mara mjadala wa kufunikwa kwa habari za tukio hili la kimataifa hujitokeza. Swali ni, je, kwa ukuaji wa teknolojia za kisasa kama akili mnemba, inawezekana kuvunja kizuizi hiki cha habari?
Kuhusu jambo hili, Dk. Muhammad Reza Qasemi, mtaalamu wa akili mnemba, katika makala yenye kichwa kisemacho “Akili mnemba Katika kutoa Huduma ya Arbaeen ya Husein”, amechambua suala hili.
Matini ya makala hii ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mungu
Tukio la ajabu la matembezi ya Arbaeen ya Husein, kama mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu duniani, kila mwaka huvutia mamilioni ya waumini kutoka pembe zote za dunia kuelekea Karbala al-Mualla; tukio lililo zaidi ya ibada ya kidini, ni alama ya umoja, mshikamano, kujitolea na mapenzi ya haki.
Katika hali hii, mtiririko mkuu wa vyombo vya habari vya dunia kila mara husitisha na kuweka pembeni hadithi hii isiyo na mfano. Vyombo vya habari ambavyo vingi vyao ni watumwa wa mfumo wa ukoloni na hupata maslahi ya wawekezaji wao katika kuondoa imani na maadili ya kiroho ya binadamu, kwa kuwa wanajua kwamba binadamu huru si mtii kwa wanyonyaji wa dunia.
Hata hivyo, tunapozitazama fursa ambazo teknolojia mpya zinazotegemea uchambuzi wa data na akili mnemba zinatoa, pamoja na uwezo wake wa ajabu katika kuchambua data, uwezo wa kuchakata lugha asilia, uzalishaji wa maudhui, na utambuzi wa mifumo ya maneno na hata mienendo, tunaona wazi tumekabiliwa na milango mikubwa na nafasi pana ya kuingia katika utamaduni wa dunia na kufikia kina cha fikra na imani za binadamu katika sehemu za mbali ulimwenguni. Hiki ni chombo kinachoweza kutekeleza jukumu kubwa katika simulizi yenye ufanisi ya tukio hili la kipekee la Arbaeen.
AI (akiki mnemba) ina uwezo wa kutafsiri maudhui ya Arbaeen katika lugha mbalimbali, kwa namna ya kiotomatiki na ya lugha nyingi, ili kuyafikisha kwa hadhira duniani. Inaweza kukusanya na kuchambua hisia za mitandao ya kijamii, kuonesha wimbi kubwa la mapenzi na uaminifu wa watu kutoka ulimwenguni kote kwa Imam Husein (as). Uzalishaji wa kiotomatiki wa video, picha, mabango, podikasti, usomaji wa maandiko kwa sauti, uandishi wa makala na kuunda machapisho ya mitandao ya kijamii kwa kutumia data za tukio hili na picha za mahujaji, ni miongoni mwa matumizi ya kawaida ya leo ya AI.
Chombo hiki kina uwezo wa kufuatilia kwa wakati halisi habari rasmi na zisizo rasmi, ili kutoa mapendekezo ya mwitikio sahihi kwa kufunikwa kwa habari kupitia mifano ya hali ya juu ya utambuzi wa upendeleo wa vyombo vya habari na ubaguzi wa taarifa.
Leo, badala ya kulalamikia kufunikwa kwa vyombo vya habari, inapaswa kutumika akili mnemba kwa ajili ya kuunda “chombo cha habari huru na chenye akili”; chombo cha habari kitakachoweza kuwasiliana na hadhira ya dunia, kuelewa lugha yao, na kuwasilisha ukweli wa Arbaeen moja kwa moja kwao. Majukwaa yanayotegemea akili mnemba yanaweza kuondoa simulizi ya Arbaeen kutoka katika ukiritimba wa vyombo vya habari vya Magharibi na kufikisha sauti ya mahujaji duniani. Hii ni nguvu laini isiyo na mfano ambayo ikitumiwa ipasavyo, itaigeuza Arbaeen kuwa “tukio kubwa la kiutamaduni na kimaandishi” katika ngazi ya kimataifa.
Siku moja, Bwana wa mashahidi wa kalamu; Shahidi Sayyid Murtadha Avini, alitabiri kuibuka kwa tukio hili la kimataifa kwa mtazamo wake wa kipekee, katika kitabu chake "Rastakhiz-e Jan":
“Kijiji cha dunia kitapatikana, iwe tunataka au hatutaki. Ukweli huu hautatuweka sisi pekee yetu ambao si raia watiifu kwenye kijiji hiki kikubwa katika wasiwasi, bali hata Magharibi, tena wao zaidi kuliko sisi, watakuwa na wasiwasi. Tunaishi katika dunia ambayo mipaka yake iko mbioni kubomoka, magharibi ina asili ya kupingana yenyewe na migongano hii ya mwisho ni hatima isiyokwepeka ambayo ustaarabu wa sasa unaiendea, mlipuko wa taarifa unatoka kwenye vituo hivi vinavyoonesha migongano iliyojificha ndani ya ustaarabu wa sasa. Wakati kizuizi cha taarifa kitakapoanguka, watu duniani wataona kwamba ngome hii inayoonekana imara ina misingi iliyooza sana kiasi kwamba itaporomoka kwa msukumo mdogo, nguvu ya Magharibi ni nguvu iliyoanzishwa juu ya ujinga, na ufahamu wa pamoja unaozalisha mapinduzi utajitokeza ghafla, kama mlipuko wa nuru.”
Arbaeen si tukio tu, ni kipande cha kudhihiri kwa haki, kila hatua inayochukuliwa kuelekea Karbala ni hatua kuelekea kudhihiri kwa haki na maandalizi ya jamii duniani kwa ajili ya serikali ya Mahdi (aj). Ikiwa akili mnemba itatumiwa ipasavyo katika kubainisha na kueneza kimataifa harakati hii kubwa, jihad ya ufafanuzi itaingia katika hatua mpya ambayo itainua bendera ya haki katika anga ya mtandao, kwa msaada na nguvu ya Mwenyezi Mungu.
Maoni yako