Jumanne 13 Mei 2025 - 18:20
Masharti na Mazingira ya Kudhihiri kwa Imam Mahdi (as)

Hawzah/ Kila tukio katika ulimwengu huu linatokea pale masharti na mazingira yake yanapotimia, na bila kutimia kwa mazingira hayo, hakuna kitu chochote kinachoweza kuwepo.

Shirika la Habari la Hawza | Kudhihiri kwa Imam Mahdi (as) kuna masharti na alama ambazo huitwa mazingira ya kudhihiri au masharti yake. Tofauti baina ya hizi mbili ni kuwa mazingira yana athari halisi katika kudhihiri, kiasi kwamba pale mazingira hayo yanapopatikana, tukio la kudhihiri hufanyika; na pasipo na mazingira hayo, hakutakuwa na kudhihiri. Lakini alama hazina mchango wowote katika kutokea kwa kudhihiri, bali ni ishara tu zinazoweza kumfanya mtu kubaini uwepo wa kudhihiri au ukaribu wake.

Kwa kuzingatia tofauti hii, inadhihirika wazi kwamba mazingira na masharti vina umuhimu mkubwa zaidi kuliko alama na ishara. Hivyo basi, ni lazima tuzingatie mazingira zaidi ya ishara, na kadri ya uwezo wetu tushirikiane katika kuyatimiza. Kwa sababu hiyo, kwanza kabisa tutaelezea mazingira na masharti ya kudhihiri.

Mazingira ya Kudhihiri

Kila tukio katika ulimwengu huu linatokea pale masharti na mazingira yake yanapotimia, na pasipo na mazingira hayo, hakuna kitu chochote kinachoweza kuwepo. Siyo kila ardhi inafaa kupanda mbegu, wala kila hali ya hewa haifai kukuza kwa kila mmea au mti. Mkulima anaweza kutarajia mavuno mazuri kutoka kwenye ardhi pale tu ambapo ameshakamilisha mazingira yanayohitajika ili kupata mazao hayo.

Kwa msingi huu, kila mapinduzi au tukio la kijamii linahitajia mazingira na masharti. Harakati ya kimataifa ya Imam Mahdi "alayhi as-salām", ambayo ni harakati kubwa zaidi ya kimataifa, pia inafuata kanuni hiyo hiyo, na haitatokea ila pale mazingira na masharti yake yatakapotimia.

Madhumuni ya kauli hii ni kukanusha fikra ya kwamba harakati ya Imam Mahdi (as) na utawala wake ni jambo lililotengwa na mfumo wa maumbile wa ulimwengu, au kwamba harakati hiyo ya kuleta marekebisho itatimia kwa njia ya muujiza bila sababu na mazingira ya kawaida. Bali kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’ani na Maimamu watoharifu (as), ni Sunnah ya Mwenyezi Mungu kwamba mambo yote katika ulimwengu huu yanatokea kupitia njia za kawaida na sababu za kimaumbile.

Imam Swādiq (as) anasema kuhusu hili:


«أَبَی اَللَّهُ أَنْ یُجْرِیَ اَلْأَشْیَاءَ إِلاَّ بِأَسْبَابٍ.»


Mwenyezi Mungu anakataa kuendeshwa mambo ila kwa sababu maalumu. (Kāfī, j.1, uk.183)

Bila shaka, kauli hii haimaanishi kwamba katika harakati kubwa ya Mahdi hakutakuwa na msaada wa ghaibu na wa kimbingu, bali maana yake ni kuwa sambamba na msaada wa Mwenyezi Mungu, mazingira, sababu na masharti ya kawaida pia yanapaswa kutimia.

Mazingira muhimu zaidi ya kudhihiri na mapinduzi ya kimataifa ya Imam Mahdi (as) ni mambo manne, ambayo kila moja litafanyiwa uchambuzi kivyake:

A) Mpango na Mtaala

Ni wazi kuwa kila harakati ya mabadiliko inahitaji kuwa na mipango miwili:

1. Mpango kamili wa kupambana na hali zilizopotoka kwa njia ya kuandaa na kupanga nguvu kazi.

2. Sheria kamili na inayolingana na mahitaji yote ya jamii ambayo ihakikishe haki zote za mtu mmoja mmoja na jamii kwa jumla, ndani ya mfumo wa dola ya haki, na ambayo iielekeze jamii katika mwelekeo wa maendeleo kuelekea hali ya kiideali.

Mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Sunnah ya Maimamu watoharifu (as) — yaani Uislamu halisi — ndiyo sheria bora kabisa na mpango ambao upo mikononi mwa Imam wa Zama (as), na atatekeleza mapinduzi yake kwa mujibu wa waraka huu wa milele wa Kiungu. Kitabu ambacho aya zake zimeshushwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ana elimu kamili juu ya nyanja zote za maisha ya mwanadamu na mahitaji yake ya kimwili na kiroho. Kwa hiyo, mapinduzi yake ya kimataifa yatakuwa na uungwaji mkono wa kipekee katika suala la sheria na mpango wa serikali, na hayawezi kulinganishwa na harakati nyingine yoyote ya mageuzi.

Ushahidi wa dai hili ni kwamba dunia ya leo, baada ya kujaribu sheria za kibinadamu, imeshuhudia udhaifu na mapungufu yake na sasa polepole inakuwa tayari kuukubali mfumo wa sheria za mbinguni.

B) Uongozi

Katika kila harakati ya mabadiliko, kuwepo kwa kiongozi ni sharti la lazima. Kadiri harakati inavyokuwa kubwa na malengo yake kuwa ya juu, ndivyo inavyohitaji zaidi kiongozi mwenye uwezo wa kulingana na malengo hayo.

Katika mapambano ya kimataifa dhidi ya dhulma na katika kueneza haki na usawa duniani, uwepo wa kiongozi mwenye elimu, uwezo na huruma, ambaye ana ujuzi wa uongozi bora, na ni nguzo kuu na ya msingi ya mapinduzi. Imam Mahdi (as), ambaye ni muhtasari wa Mitume na Mawalii, ndiye kiongozi wa mapinduzi haya makubwa. Yuko hai na yupo hadhir. Yeye ndiye kiongozi pekee ambaye kwa sababu ya uhusiano wake na ulimwengu wa ghaibu, ana uelewa kamili wa kila kilichopo, na ndiye mwanadamu mwenye elimu zaidi katika zama zake.

Mtume Mtukufu (saw) amesema:

«أَلَا إِنَّهُ وَارِثُ کُلِّ عِلْمٍ وَ الْمُحِیطُ بِکُلِّ فَهْمٍ.»
 

Fahamuni! Yeye (Mahdi) ni mrithi wa elimu yote na ana uelewa na maarifa yote kwa ukamilifu. (Khutbah ya Ghadīr)

C) Wasaidizi

Sharti jingine muhimu kwa kudhihiri ni kuwepo kwa wasaidizi waaminifu na stahiki watakaosaidia harakati hiyo na kutekeleza majukumu ya serikali ya kimataifa. Ni jambo la wazi kuwa mapinduzi ya kimataifa yatakayoongozwa na kiongozi wa mbinguni yanahitaji wasaidizi wanaolingana na hadhi hiyo. Si kila mtu anayejidai kuwa msaidizi anaweza kushiriki katika uwanja huu.

D) Utayari wa Umma

Katika nyakati mbalimbali za historia ya Maimamu watoharifu (as), tunaona ukweli huu kwamba watu hawakuwa na utayari wa kutosha wa kunufaika kwa kiwango cha juu na uwepo wa Imamu. Wakati wa kuwepo kwao, watu hawakuthamini kikamilifu neema ya kuwa karibu nao, wala hawakuchota ipasavyo kutoka katika chemchemi ya mwongozo wao. Mwenyezi Mungu Mtukufu alimficha Hujjah wa mwisho hadi wakati ambapo utayari wa umma wa kumkubali utakapopatikana, ndipo atadhihiri na kuwanywesha watu wote kutoka katika chemchemi ya maarifa ya Kimungu.

Hivyo basi, uwepo wa utayari wa jumla ni sharti muhimu sana la kudhihiri kwa Mkombozi aliyeahidiwa, na kwa kupitia sharti hili ndipo harakati yake ya marekebisho itazaa matunda yanayotarajiwa. Kudhihiri kutatokea pale ambapo wote kwa pamoja, kwa undani wa nafsi zao, watatamani haki katika jamii, usalama wa kimaadili na kiakili, pamoja na ustawi na maendeleo ya kiroho.

Ni wazi kuwa hamu ya kushuhudia uwepo wa Imamu hufikia kilele pale binadamu anapopitia uzoefu wa serikali mbalimbali na mifumo ya kibinadamu, na hatimaye kufikia hitimisho kuwa mkombozi pekee wa ulimwengu huu kutokana na ufisadi na maangamizi ni Khalifa na Mrithi wa Mwenyezi Mungu ardhini — yaani Imam Mahdi (as) — na kwamba mpango pekee wa kuleta maisha safi na matakatifu kwa wanadamu ni sheria za Kimungu. Hivyo basi, wanadamu huielewa kwa kina haja yao kwa Imamu, na baada ya kufikia uelewa huo, huanza kujitahidi kutengeneza mazingira ya kudhihiri kwake na kuondoa vizingiti vilivyopo mbele yake. Ni wakati huo ndipo "faraja" na mwangaza wa matumaini huwasili.

Mtume Mtukufu (saww) amesema:

«... حَتَّی لاَ یَجِدُ اَلرَّجُلُ مَلْجَأً یَلْجَأُ إِلَیْهِ مِنَ اَلظُّلْمِ، فَیَبْعَثُ اَللَّهُ رَجُلاً مِنْ عِتْرَتِی... .»


[Wakati utafika] ambapo mtu muumini hataweza kupata hifadhi yoyote ya kujikinga na dhulma; basi [katika wakati huo], Mwenyezi Mungu atamleta mtu kutoka katika kizazi changu... . (Ithbāt al-Hudā, j.5, uk.244)

Utafiti huu unaendelea...

Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Negin-e Āfarinish” huku ikifanyiwa marekebisho kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha