Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, “Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu” wa Lebanon, kwa kutoa tamko lao, umelaani vikali mauaji ya halaiki yaliyofanywa na adui Myahudi katika kambi ya Ayn al-Hilwah, na kusisitiza kuwa: Adui Myahudi hakuhitaji kufanya mauaji mapya ili kuthibitisha mwelekeo wake endelevu wa kuamua kuangamiza taifa la Palestina.
Umoja huo umeongeza kwamba: Lakini katika jinai yake ya karibuni iliyo ya kuchukiza, hakutofautisha kati ya shabaha ya kijeshi – kama anavyodai – na taasisi ya kijamii–kimichezo iliyokuwa na jukumu la kuwatunza watoto na vijana wa Kipalestina waliotawanywa. Vijana ambao wamelazimishwa kuondoka katika ardhi yao na kusubiri kurejea wakiwa katika makambi ya wakimbizi.
Umoja huo wa Wanazuoni umeeleza: Adui, kwa kutekeleza mauaji ya kutisha katika kambi ya Aynu al-Hilwah, alilenga uwanja wa michezo ambapo vijana wa kambi hiyo walikuwa wamekusanyika, na makumi ya watu kati yao wameuawa shahidi na kujeruhiwa. Vilevile, adui hakuzingatia kwamba uwanja huo wa michezo ulikuwa karibu na Msikiti wa Khalid bin Walid, ambako waumini walikuwa wamekusanyika wakati huo; na katika wakati uleule ambao mashine ya mauaji ya Kizayuni ilipolenga uwanja, msikiti pia uliathirika.
Madai ya uongo ya adui Myahudi
Tamko hilo limeongeza kuwa: Imebainika kuwa mashahidi wengi na majeruhi ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18; jambo hili linathibitisha uongo wa madai ya adui Myahudi aliyedai kuwa shabaha yake ilikuwa kikao cha viongozi wa makundi mbalimbali ya Kipalestina ndani ya uwanja huo wa michezo, au mkusanyiko wa wahusika wa kigaidi katika eneo ambalo alilipa jina la “Kituo cha Elimu cha Hamas”.
Umoja wa Wanazuoni Waislamu ukaendelea kusema: Adui Myahudi, kutokana na kukosa hazina mpya za kulenga, ameanza kulenga maeneo ya kidini, na ili kuhalalisha mashambulizi haya hutumia uwongo wa kudai kulenga shabaha za kijeshi.
Tamko hilo limeashiria kuwa mashambulizi ya awali kama vile kulenga manispaa ya Blida na uvamizi wa jana dhidi ya manispaa ya Al-Tayri vinathibitisha kuwa adui hana tena malengo ya kijeshi. Hivyo basi, ili kuleta hofu miongoni mwa wakazi, amegeukia kuwalenga raia wasiopigana wanaojaribu kujenga upya; kwa dhana kwamba ujenzi upya unavuruga mipango yake ya upanuzi ndani ya Lebanon.
Ombi la kuchukuliwa kwa hatua muafaka
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu umesisitiza: Mauaji ya halaiki yaliyofanywa na adui Myahudi katika Aynu al-Hilwah yanahitaji jibu muafaka kutoka kwa muqawama wa Kipalestina, na jinai hii haitasalia bila hisabu na adhabu – lakini kwa njia ya hikima itakayochaguliwa na uongozi wa muqawama. Vivyo hivyo, mauaji haya yanahitaji msimamo wa serikali ya Lebanon ambayo inapaswa kuwasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama na kuomba kuitishwa kwa dharura kwa Kamati ya Utaratibu (mekanizimu) ili kulaani kitendo hiki cha woga na uhalifu.
Umoja huo umekumbushia kwamba suala la Palestina litaendelea kuwa suala kuu la Umma, na kusisitiza: Hatutaliacha.
Mwishoni, Umoja huo umesifu kikao kilichofanyika katika kituo cha Dar al-Ifta’ mjini Sidon, kilichohudhuriwa na wanaharakati wa kisiasa na kidini, na ukaunga mkono yaliyotolewa kwenye kikao hicho, hususan juu ya kutoshindwa na kuendelea kushikamana na dhana ya Palestina hadi kufikiwa kwa lengo tukufu la Umma – ambalo ni kuikomboa Palestina yote, kuanzia baharini hadi mtoni, na kuangamizwa kwa utawala haramu wa Kizayuni.
Maoni yako