Jumanne 25 Novemba 2025 - 20:18
Iran Yalaani Vikali Mauaji ya Kamanda Mkubwa wa Muqawama

Hawza/ Wizara ya Mambo ya Nje na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa wamelaani vikali uhalifu wa kigaidi uliofanywa na utawala wa Kizayuni katika shambulio dhidi ya maeneo ya makazi huko Beirut na mauaji ya kamanda mkubwa wa muqawama, Haitham Ali Tabatabai.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Wizara ya Mambo ya Nje kupitia tamko ililolitoa imelaani vikali uhalifu wa kigaidi wa utawala wa Kizayuni katika shambulio dhidi ya maeneo ya makazi huko Beirut na mauaji ya kamanda mkubwa wa muqawama, Haitham Ali Tabatabai.

Maudhui ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inalilaani vikali shambulio la alasiri ya Jumapili lililofanywa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo la makazi huko Dhahiyya Beirut na kuuwawa kishujaa ya kamanda mwandamizi wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon, Shahid Haitham Ali Tabatabai; shambulio ambalo ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2024 na ni uvamizi wa kinyama dhidi ya ukamilifu wa ardhi na mamlaka ya kitaifa ya Lebanon, na limesababisha kuuwawa na kujeruhiwa makumi ya raia wa kawaida wa Lebanoni wakiwemo wanawake na watoto wasio hatia. Wizara hii inalilaani vikali tukio hili na kusisitiza ulazima wa kuwafikisha mahakamani na kuwaadhibu viongozi wa utawala huu kwa kutenda kitendo hiki cha kigaidi na jinai ya kivita.

Wizara ya Mambo ya Nje, sambamba na kutoa heshima kwa daraja tukufu la Shahid Haitham Ali Tabatabai ambae maisha yake yenye baraka aliyatumia katika kuilinda Lebanon na kuupigania muqawama dhidi ya adui Mzayuni, sambamba na kuwapa mkono wa pole viongozi na wapiganaji wa Hizbullah Lebanon na familia za mashahidi, imesisitiza kwamba; kuendelea kwa uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni ni sababu kuu ya uendelezaji wa uvunjaji sheria na uvamizi wa utawala huo. Aidha imesisitiza wajibu wa moja kwa moja wa wadhamini wa kusitisha mapigano katika suala hili.

Wizara ya Mambo ya Nje, kwa kukumbushia uvunjaji wa mara kwa mara wa kusitisha mapigano na utawala wa Kizayuni, imetaja kutofanyiwa kazi na ukimya wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja huo mbele ya uvamizi unaoendelea na jinai nyingi za utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Lebanon kuwa ni jambo la kusikitisha na lisilokubalika, na imeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na ugaidi ulioratibiwa na uchochezi wa vita unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na mataifa mengine ya eneo hili. Bila shaka yoyote, vitimbi vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia ya Magharibi ni tishio kubwa kabisa si kwa amani na uthabiti wa eneo hili tu bali pia kwa amani na usalama wa kimataifa, na hivyo basi kukabiliana na tishio hili ni jukumu la dunia nzima.

Dkt. Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, naye katika ujumbe wake ametoa mkono wa pole kwa ajili ya shahada ya Haitham Ali Tabatabai, na aliandika:

“Katika usiku wa shahada ya Fatimah Zahra (a.s.), mmoja wa wafuasi wa kweli wa bibi huyu mtukufu wa wanawake ulimwenguni, shahidi Haitham Ali Tabatabai, miongoni mwa makamanda wakuu wa Hizbullah, pamoja na baadhi ya wenzake amefikishwa kwenye shahada kwa mkono wa Wazayuni wahalifu.

Wao wamefikia matamanio yao, lakini Netanyahu ataendelea na vitimbi vyake hadi dunia nzima ijue kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kukabiliana na utawala huu bandia.

Ninatoa mkono wa pole kwa kiongozi mtukufu wa Hizbullah na mujahidin wake.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha