Jumapili 6 Aprili 2025 - 23:31
Wafanyakazi wa Microsoft wavuruga sherehe, wasema AI ya shirika imechangia mauaji ya kimbari Gaza

Wafanyakazi wa shirika la Microsoft la Marekani wameandamana wakati wa tukio la sherehe ya miaka 50 ya kuanzisha kampuni hiyo, wakitangaza upinzani wao dhidi ya kutumiwa teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence-AI-) ya kampuni hiyo na utawala wa Israel katika vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza.

 Shirika la Habari la Hawza - Ijumaa, wakati wa tukio hilo lililohudhuriwa na watu mashuhuri kama mwanzilishi mwenza Bill Gates na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Steve Ballmer, waandamanaji wanaoitetea Palestina walikatisha hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kitengo cha Akili Mnemba cha Microsoft, Mustafa Suleyman, wakati alipokuwa anawasilisha mpango wa kuboresha programu ya Akili Mnemba ya kompyuta za Microsoft inayojulikana kama Copilot.

Mmoja wa waandamanaji aliyetambuliwa kama Ibtihal Aboussad ambaye ni mfanyakazi wa Microsoft alisikika akipiga mayowe na kusema: “Mustafa, aibu kwako,” huku akielekea jukwaani. Tukio hilo lilimfanya Suleyman aache hotuba yake.

Aliendelea kusema, “Wewe ni mfanyabiashara anayefaidika na vita. Acha kutumia Akili Mnemba kufanya mauaji.”

Bi. Aboussad akiwa amevalia Hijabu aliendelea kusema: “Unadai kwamba Akili Mnemba inatumiwa kwa ajili ya malengo mema, laakini Microsoft inaliuzia jeshi la Israel silaha za Akili Mnemba. Watu elfu hamsini wameuawa Gaza na Microsoft inashiriki katika mauaji hayo.”

Aboussad aliendelea kutoa nara dhidi ya Microsoft kwa kusema: "Suleyman na Microsoft yote” wana damu mikononi mwao. Kisha alirusha skafu ya Kipalestina ya keffiyeh jukwaani kabla ya walinzi kumuondoa kwa nguvu kwenye kikao hicho.

Microsoft imekabiliwa na ukosoaji unaoongezeka kuhusiana na mikataba yake na jeshi la Israel, kwani ripoti zinaonyesha kuwa teknolojia ya Akili Mnemba za kampuni hiyo hutumika kuchagua maeneo yanayolengwa kwa mabomu katika Ukanda Gaza, na kusababisha mauaji ya maelfu Wapalestina hasa wanawake na Watoto..

Baadaye, mfanyakazi mwingine wa Microsoft, Vaniya Agrawal, alikatisha sherehe hiyo huko Redmond, Washington, wakati Gates, Ballmer, na Mkurugenzi Mtendaji wa sasa Satya Nadella walipokuwa jukwaani .

Wafanyakazi wengine pia walikusanyika na kuandamana nje ya ukumbi wa mkutano.

Microsoft siyo shirika pekee lililokabiliwa na maandamano kutokana na uhusiano wake na utawala katili wa Israel. Mwezi Aprili mwaka uliopita, Google iliwafukuza wafanyakazi 28 kufuatia maandamano dhidi ya mkataba wa kampuni hiyo na utawala haramu wa Israel kuhusiana na data za kivita.

Chanzo: Pars Today

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha