Jumapili 6 Aprili 2025 - 00:33
Wanazuoni wa Kiislamu Watoa Fatwa ya Jihad Dhidi ya Israel

Kamati ya Ijtihad na Fatwa ya taasisi moja ya kimataifa ya wanazuoni Kiislamu imesisitiza kuwa kuanzisha Jihad dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Isarel unaoendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza ni wajibu wa Kiislamu.

 Shirika la Habari la Hawza - Kulingana na IQNA, katika taarifa, Kamati ya Ijtihad na Fatwa ya Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) imetoa Fatwa ikisisitiza kuwa kuanzisha Jihad dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni wajibu wa Kiislamu (Wajib), kufuatia kile ilichokitaja kuwa mauaji ya kimbari yanayoendelea dhidi ya wananchi wa Gaza.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa IUMS, Sheikh Ali al-Qaradaghi, umoja huo umezitaka nchi zote za Kiislamu pamoja na zile zenye Waislamu wengi kuchukua hatua madhubuti—kijeshi, kiuchumi na kisiasa—ili kukomesha kile alichokiita "mauaji ya halaiki na uharibifu mkubwa unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina."

“Kushindwa kwa serikali za Kiarabu na Kiislamu kuiunga mkono Gaza wakati ikiteketezwa ni jinai kubwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu dhidi ya ndugu zetu wanaoonewa,” alisema Sheikh Qaradaghi katika waraka huo maalum uliosheheni vipengele 15.

Sheikh Qaradaghi, anayehesabiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, alisisitiza kuwa ni haramu kwa Muislamu yeyote kuisaidia Israel kwa namna yoyote ile katika operesheni zake dhidi ya Gaza.

Alisema: “Hairuhusiwi kuuza silaha kwa Israel, wala kuruhusu usafiri wake kupitia bandari au njia za kimataifa kama Mfereji wa Suez, Bab al-Mandab, Mlango wa Hormuz, au njia nyingine yoyote ya ardhini, angani au majini.”

Katika fatwa hiyo, IUMS pia imetoa mwito wa kuanzishwa kwa vikwazo vya anga, baharini na nchi kavu dhidi ya Israel, kama ishara ya mshikamano na watu wa Gaza.

Wanazuoni wengine 14 mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali pia waliunga mkono tamko hilo, wakitoa wito kwa nchi za Kiislamu kufanyia mapitio upya mikataba yao ya amani na Israel. Pia waliwataka Waislamu wanaoishi Marekani kutumia ushawishi wao kisiasa kumshinikiza Rais Donald Trump kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni zake – ikiwa ni pamoja na kusitisha mashambulizi na kusaidia kuleta amani ya kudumu.

Vita vya kinyama vya mauaji ya kimbari na halaiki vinavyoendeshwa na utawala wa Israel huko Gaza, vilivyoanza mwezi Oktoba 2023 kufuatia shambulio la kulipiza kisasi lililoongozwa na Hamas dhidi ya utawala huo, vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 50,609 hadi sasa.

Mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa masuala ya kijeshi, Yoav Gallant, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaotekelezwa huko Gaza.

Fatwa ni tamko au uamuzi wa kisheria unaotolewa na mwanazuoni wa Kiislamu, unaotegemea Qur’an na Sunna (mafundisho na matendo ya Mtume Muhammad – Amani -SAW-). Ingawa si lazima kufuatwa kisheria, fatwa hubeba uzito mkubwa katika jamii za Kiislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha