Jumanne 25 Machi 2025 - 11:29
Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa ya Umma kufungamana na Palestina

Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa ya kuonyesha msaada wa umma kwa taifa la Palestina na ukombozi wa al-Quds, amesema afisa mwandamizi nchini Iran.

Shirika la Habari la Hawza - Kiongozi wa Makao Makuu ya Intifada na Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran, Brigedia Jenerali Ramezan Sharif, ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani (IQNA) kabla ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya mwaka huu, ambayo itakuwa tarehe 28 Machi.

Siku ya Kimataifa ya Quds ni mojawapo ya urithi wa hayati mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu), ambaye anaheshimiwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote.

Mji wa al-Quds (Jerusalem) unachukuliwa kuwa nembo ya ukombozi wa Palestina kwani unatazamiwa kuwa mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.

Katika ujumbe wake wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa "Siku ya Kimataifa ya Quds", Imam Khomeini aliwataka Waislamu na wapenda haki kote ulimwenguni kujitokeza kila mwaka katika siku hii kwa ajili ya kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina na kuungana kwa ajili ya kukata mikono ya utawala haramu wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina huku ukitenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimpindua mtawala wa kiimla, Shah, aliyeungwa mkono na Marekani pamja na Israel, Imam Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa Quds ili Waislamu na wapenda haki kote duniani waweze kujitokeza katika siku hiyo katika maandamano na mijumuiko ya kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina sambamba na kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel unaokoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yatakuwa na ujumbe wa msaada wa walimwengu na hasa harakati za Muqawama kwa Wapalestina wanaokandamizwa katika Ukanda wa Gaza, Brigedia Jenerali Sharif aliiambia IQNA. 

Amesisitiza kuwa mwaka huu Siku ya Quds itakuwa ujumbe wenye maana kwa utawala wa Kizayuni na waitifaki wake ambao ni kuwataka wasitishe mauaji ya watu wa Palestina na sambamba na kuwaruhusu warejee katika ardhi yao na kuishi kwa amani, alisisitiza. 

Aliongeza kuwa umati mkubwa wa watu wa Iran katika mikutano ya Siku ya Quds kwa miaka mingi umedhihirisha uthabiti wao katika kuunga mkono Palestina na kukemea utawala wa Kizayuni.

Ameongeza kuwa hatua ya Imam Khomeini ya kutangaza Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ilisambaratisha mkakati wa utawala wa Israeli wa kuondoa suala la Palestina katika fikra za walimwengu.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Brigedia Jenerali Sharif amesema taifa la Palestina, ambalo lilianza mapambano yake dhidi ya wavamizi wa Kizayuni kwa mawe, sasa limekuwa na nguvu, kama ilivyoonyeshwa katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyofanywa na vikosi vya Muqawama au mapambano ya Kiislamu dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 2023. 

Afisa huyo ameelezea matumaini kwamba kuna siku watu wa dunia watashuhudia jiji takatifu la al-Quds likiwa limekombolewa na taifa la Palestina litaishi katika ardhi hii kwa amani na usalama tena.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha