Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hafla ya kuadhimisha usiku wa saba tangu kufariki Marji' Mkuu wa Taqlidi, Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), iliandaliwa na Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi, huku yeye mwenyewe akihudhuria hafla hiyo. Mkusanyiko huo ulifanyika Jumanne usiku, tarehe 3 Azar 1405 Hijria Shamsia, baada ya Swala ya Magharibi na Isha, katika Msikiti Mkuu wa Qum.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Hawza, wawakilishi wa ofisi za Maraji' wakuu wa Taqlidi, wajumbe wa Ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wajumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi, Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Kielimu ya Qum, Baraza Kuu la Hawza za Kielimu na Baraza la Walinzi wa Katiba. Aidha, walihudhuria kundi la wanazuoni na wasomi wa Hawza, viongozi wa kitaifa na kimkoa, makamanda wa vikosi vya kijeshi na vyombo vya usalama, wabunge pamoja na wananchi kutoka makundi mbalimbali waliokuwa wamehudhuria kwa ajili ya kuomboleza.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hussein Mu’mini, mwalimu wa Hawza ya Kielimu ya Qum na mzungumzaji mkuu wa hafla hiyo, alisimulia baadhi ya kumbukumbu zake za kipindi alipokuwa mwanafunzi wa marehemu. Alizungumzia namna marehemu alivyoishi, mwenendo wake wa kielimu na jinsi alivyokuwa akitoa umuhimu mkubwa kwenye majlisi za kuomboleza misiba ya Ahlul-Bayt (a.s.).
Ili kuwatambua wanazuoni wakubwa, tuangalie njia walizozipitia
Mwanzoni mwa hotuba yake, mwalimu huyo wa Hawza alieleza kuwa kupanga mambo ni msingi wa kuwa na utaratibu, na utaratibu huo huimarisha azma ya mwanadamu katika kufikia malengo yake.
Alisema: “Mwanadamu, pamoja na kuwa na mipango, anahitaji pia kuwa na mifano ya kuigwa. Baada ya Maasumina (a.s.), ambao tunaweza kuwaiga katika nyanja zote za maisha, tunapaswa kuangalia mwenendo wa wanazuoni walioifuata njia ya Ahlul-Bayt (a.s.), wakasimama imara katika njia hiyo na ambao katika mienendo yao hakukuwa na dalili yoyote ya kujifungamanisha na asiyekuwa Mwenyezi Mungu.”
Akigusia ukweli kwamba wanazuoni wengi wamewahi kufundisha katika Msikiti Mkuu wa Qum, lakini leo hii hata baadhi ya wanafunzi vijana wa Hawza hawafahamu majina ya baadhi yao, aliongeza: “Lengo la kuwaenzi wanazuoni si kuendeleza majina na umaarufu wao pekee, bali ni lazima tuangalie ni njia gani waliyoipitia ambayo iliwawezesha kuwa na athari kwa wengine walipokuwa hai, na hata baada ya kufariki kwao, watu wengine wakaweza kuifanya mienendo yao ya maisha kuwa mfano wa kuigwa katika kuifuata njia hiyo hiyo.”
Katika kufafanua jambo hilo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini alimzungumzia Shahidi wa Kwanza (Shahid Awwal), aliyeandika kitabu cha Fiqhi kinachoitwa Al-Lum’ah akiwa gerezani. Baada ya kuuawa kwake, hata alama ya kaburi lake haikuachwa. Hata hivyo, licha ya kuandikwa vitabu vingi baada yake, kitabu chake bado kinasomwa katika Hawza, na jina lake limeendelea kuhusishwa na utetezi wa Fiqhi ya Ahlul-Bayt (a.s.).
Mwalimu huyo wa Hawza pia alizungumzia nafasi ya marehemu Akhund Khorasani (q.s.), akisema kuwa anafahamika zaidi kupitia kitabu chake Kifayat al-Usul, ambacho ni kitabu madhubuti na kigumu. Ugumu wa matini yake pia humsaidia mwanafunzi wa Hawza kujenga uwezo wa kuelewa maandishi na riwaya zenye utata na ugumu.

Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani alikuwa katika kilele cha unyenyekevu
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini, akimwelezea Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), alisema kuwa; marehemu alikuwa katika kilele cha unyenyekevu.
Alisema: “Daraja lake la kielimu linafahamika miongoni mwa watu wa Hawza. Hata hivyo, jambo ambalo wanafunzi wake walikuwa wakilishuhudia walipokuwa pamoja naye, mbali na uwezo wake mkubwa wa kielimu, ni utumwa wake kwa Mwenyezi Mungu, nidhamu, mipango na juhudi zake za kudumu. Mambo hayo yalikuwa yakimfanya asiruhusu hata dakika moja ya maisha yake ipotee bure.”
Aliwausia wanafunzi wa Hawza kutafuta kupata usikivu wa Imam Mahdi (a.j.)
Akieleza kwamba alihudhuria masomo ya Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.) katika Msikiti Mkuu wa Qum kwa kipindi cha takribani miaka kumi hadi kumi na moja, Mu’mini alikumbuka siku ambayo kaka yake na watoto wa dada yake walivishwa mavazi ya wanazuoni mbele ya Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.).
Alisema: “Jambo nililolisikia kutoka katika kinywa chake mwenyewe, na ambalo kila ninapolikumbuka bado linanigusa moyo, ni pale alipowaambia: ‘Fanyeni mambo yatakayowafanya muonekane mbele ya macho ya Hujjat bin Hassan (a.j.).’
“Nasaha hiyo ilikuwa inaendana kikamilifu na mwenendo wa maisha yake mwenyewe, kwani hakuwa akitafuta kufanya mambo ili aonekane na watu wengine.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini pia alipataja mahali alipozikwa Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.) kuwa ni mfano mwingine unaoendana na roho hiyo ya unyenyekevu.
Aliongeza kuwa marehemu alikuwa akisema anataka kuzikwa chini ya miguu ya Imam Ridha (a.s.). Hata sasa, kaburi lake halipo katika upande wa wanaume ya Haram Tukufu, lakini jambo lililokuwa muhimu kwake ni kutimia kwa matakwa yake ya kupumzishwa chini ya miguu ya Imam Ridha (a.s.).
Riwaya aliyokuwa akiijua kwa moyo katika nusu ya mwezi wa Shaaban, lakini aliisoma kutoka kitabuni
Mwalimu huyo wa Hawza ya Kielimu ya Qum, akirejelea hotuba za Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.) katika maadhimisho ya nusu ya mwezi wa Shaaban yaliyokuwa yakifanyika katika Msikiti Mkuu wa Qum, alisema: “Ninakumbuka waziwazi angalau miaka miwili au mitatu ambapo alikuwa akiwasomea watu riwaya ya dua ya Bani Israil kutoka katika juzuu ya pili ya kitabu Tafsir al-Ayyashi. Licha ya kuwa alikuwa ameihifadhi riwaya hiyo kwa moyo, alikuwa akiweka kitabu mbele yake na kuisoma. Wakati akisoma, alikuwa akishindwa kujizuia kutokana na hisia kali, sauti yake ikitetemeka na machozi yakimtoka.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini, akifafanua riwaya hiyo ambayo marehemu alikuwa akiitumia, alisema: “Kwa mujibu wa tafsiri hiyo, mateso ya Bani Israil yalitakiwa kuendelea kwa miaka 400. Hata hivyo, baada ya kupita miaka 230, walitumia siku 40 usiku na mchana wakimwomba Mwenyezi Mungu kwa kilio na majonzi ili awaondolee mateso yao.
“Ndipo Mwenyezi Mungu alipowasamehe miaka 170 iliyokuwa imebaki na akawaamuru Mitume wake, Nabii Musa na Nabii Harun (a.s.), wawaokoe watu hao kutoka katika makucha ya Firauni.”
Akieleza kuwa lengo la Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.) kuisoma riwaya hiyo katika maadhimisho ya nusu ya mwezi wa Shaaban lilikuwa ni kuwafahamisha watu umuhimu wa dua katika kuomba kuja faraja na kufunguliwa mambo, aliendelea kusema: “Baada ya kusimulia kisa cha Bani Israil, alikuwa akisoma sehemu ya mwisho ya riwaya hiyo, ambapo Imam (a.s.) anasema kwamba lau Mashia nao wataomba na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa namna hiyo hiyo, basi Mwenyezi Mungu ataleta Faraja (Dhuhoor) ya Imam Mahdi (a.j.).”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini aliendelea kusisitiza kuwa Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), pamoja na masomo na mijadala yake ya kielimu, alikuwa akizipa umuhimu wa pekee majlisi za kuomboleza msiba wa Imam Hussein (a.s.). Katika siku za Fatimiyyah, aliona kwenda Haram ya Bibi Ma’sumah (s.a.) kuwa sehemu ya maombolezo
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mu’mini, akigusia kwamba mwaka huu nafasi ya Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.) ilikosekana katika hafla za maombolezo na matembezi ya miguu ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Bibi Fatimah Zahraa (s.a.), alisema: “Marehemu alikuwa akiwausia watu kwa kusema: ‘Zungumzeni kuhusu Fatimah.’ Yeye mwenyewe, katika siku ya kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Bibi Fatimah (s.a.), alikuwa akivua kilemba chake, akiliondoa joho lake mabegani, akifungua vifungo vya kanzu yake kama ishara ya maombolezo, kisha akienda kwa miguu mitupu katika Haram ya Bibi Ma’sumah (s.a.) ili kutoa rambirambi za kuuawa shahidi Bibi Bibi Fatimah (s.a.) kwa Mkarimu wa Ahlul-Bayt (s.a.).”
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi, pamoja na ushiriki wake katika majlisi ya maombolezo ya Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), ilifanyika kwa lengo la kuienzi nafasi yake ya kielimu na huduma zake kwenye Hawza za kielimu na Madh-hab ya Ahlul-Bayt (a.s.).
Awali, baada ya kufariki Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi alikuwa ametoa ujumbe wa rambirambi, akieleza masikitiko yake kutokana na msiba huo na kuenzi huduma za kielimu na kidini za mwanazuoni huyo mashuhuri.
Ikumbukwe kwamba: Hafla nyingine ya kumuenzi Ayatollah al-Udhma Waheed Khorasani (q.s.), iliyoandaliwa na Ayatollah al-Udhma Jawadi Amuli (Mwenyezi Mungu amuhifadhi), itafanyika siku ya Ijumaa baada ya Swala ya Magharibi na Isha katika ofisi ya Marji' huyo wa Taqlidi, iliyopo katika Mtaa wa Safaiyeh, Qum, Iran.
Maoni yako