Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, likinukuu ukurasa wa Ofisi ya Sayyid Ibrahim Zakzaky, Sheikh Ibrahim Zakzaky, alitoa hotuba katika hafla ya kufunga Kongamano la Vyombo vya Habari la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (Media Forum), lililofanyika jijini Abuja, siku ya Jumapili, tarehe 12 Jumada al-Akhira 1448 Hijria, sawa na tarehe 1 Azar 1405 Hijria Shamsia (22 Novemba 2026).
Katika hafla hiyo, alizitaja shughuli za kutoa taarifa na kufikisha ujumbe kuwa ni juhudi muhimu na zenye thamani kubwa. Akizungumzia nafasi ya kufikisha ujumbe katika zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w), alisema kuwa juhudi za kufikisha ujumbe wa dini katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) zilikuwa na mchango mkubwa katika kuenea kwa Uislamu.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, akizungumzia pia mabadiliko yaliyotokea katika nyenzo za mawasiliano na maendeleo ya teknolojia katika zama za sasa, aliitaja mitandao ya kijamii kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu zaidi za kufikisha ujumbe katika dunia ya leo. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutumia vizuri na kwa malengo maalumu fursa hiyo.
Sheikh Zakzaky alionya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hususan kutoa matusi, lugha chafu na kutowaheshimu wengine, huku akisisitiza: “Tunataka kushuhudia mageuzi na mabadiliko katika namna ya kutumia mitandao ya kijamii.”
Katika kuendelea kusisitiza umuhimu wa tabia na mwenendo wa kihabari wa wanachama wa Harakati ya Kiislamu kuwa tofauti na wa watu wengine, alibainisha: “Lazima kuwe na tofauti ya wazi kati ya yale tunayoyafanya sisi na yale yanayofanywa na wengine.”
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia nafasi ya kielimu na kiakili ya wafuasi wa harakati hiyo, alisema: “Ni sisi tunaopaswa kuwa walimu wa wengine, nao wanapaswa kujifunza kutoka kwetu.”
Mwisho wa hotuba yake, alizitaja hekima, busara, elimu na kujiepusha na matusi pamoja na kumvunjia mwingine heshima kuwa ni miongoni mwa misingi muhimu ya kufikisha ujumbe na kuwasiliana na wengine kupitia mitandao ya kijamii. Pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia tunu hizo katika utekelezaji wa shughuli za kihabari.
Kongamano hilo lilifanyika kwa muda wa siku mbili, likiwa na lengo la kuchunguza uwezo na fursa zilizopo katika nyanja ya vyombo vya habari, pamoja na kuinua kiwango cha shughuli za utoaji wa taarifa za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Kongamano hilo lilihitimishwa kwa hotuba ya Kiongozi wa harakati hiyo.
Maoni yako