Jumatano 25 Novemba 2026 - 13:50
Ikhlasi ya Allamah Tabatabai; Shahidi Mutahhari Anukuu Similizi kutoka kwa Mwalimu Wake

Hawza/ Inawezekanaje mwanachuoni kutumia miaka thelathini katika juhudi za kielimu na kuandika tafsiri yenye thamani kubwa, lakini hata kwa kazi hiyo kubwa asijione kuwa anastahili kupata thawabu? Shahidi Mutahhari, kwa kunukuu simulizi kutoka kwa Allamah Tabatabai, anasimulia mfano wa kushangaza wa ikhlasi na kuichunga nafsi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Shahidi Murtadha Mutahhari, aliponukuu simulizi kutoka kwa mwalimu wake, Allamah Tabatabai, alizungumzia kiwango cha juu cha ikhlasi aliyokuwa nayo. Alisema kuwa Allamah, katika tukio lililofanana na ndoto, alimwona baba yake akiwa hamridhii, na sababu ya kutoridhika kwake ilikuwa kwamba hakumshirikisha katika thawabu za uandishi wa tafsiri yake.

Shahidi Mutahhari aliendelea kueleza kuwa Allamah hakujiona kuwa anastahili kupata thawabu kwa kazi hiyo. Akasisitiza kwamba: Mwenyezi Mungu anapopata nafasi ndani ya moyo wa mwanadamu, huingia na kutawala ndani yake kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hata tendo kubwa sana huliona kuwa dogo, na nafsi ya mwanadamu hutawaliwa na kushindwa mbele Yake. Hii ndiyo maana na athari ya mafundisho ya Mitume yanapopenya ndani ya mwanadamu.

Katika kikao cha mmoja wa wanazuoni wakubwa, ambaye ana nafasi ya kuwa mwalimu wangu na ambaye nimefaidika na elimu yake, alikuwa akisimulia tukio lililofanana na ndoto. Alikuwa akizungumzia jambo hili kwamba katika ndoto hiyo inayofanana na hali ya kuota, alimwona baba yake akiwa hamridhii.

Alikuwa amemuuliza sababu ya kutoridhika kwake, naye akajibiwa kwamba: Mwanangu huyu, katika kitabu fulani alichokiandika — ambacho kwa hakika ni kitabu chenye thamani kubwa sana na manufaa mengi — ametumia miaka thelathini ya juhudi, na matokeo yake ni kitabu hiki chenye manufaa makubwa katika taaluma ya tafsiri, ambacho amekiacha kama urithi kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Je, kuna huduma nyingine iliyo bora na kubwa zaidi kuliko hii?! Hayo yote ameyafanya huku akivumilia matatizo na kunyimwa mambo mengi, ambayo mimi ninayafahamu; kwa sababu ninajua kwamba kama mtu huyu angetumia nguvu na uwezo wake katika kuandika vitabu vinavyoingiza kipato, hali yake ya kifedha na nafasi yake vingekuwa bora zaidi, tena kwa kiwango kikubwa sana.

Pamoja na hayo yote, baba katika ndoto hiyo analalamika kwamba mwanangu huyu hakunishirikisha katika thawabu za kitabu chake hiki alichokiandika.

Baada ya hapo, yeye mwenyewe alianza kuzungumza kwa hali ya kawaida kabisa, akasema: «Wallahi, mimi sielewi! Kwa kweli, sikuwa hata nimeipa kazi hii thawabu yoyote ili nianze kufikiria kwamba thawabu yake iwe yangu, au ya baba yangu, au ya kaka yangu. Sikuwahi hata kufikiria kwamba kazi hii kimsingi inastahili kuwa na thawabu.»

Sasa, kwa nini sisi tunapokuwa katika hali hii, tunasisimka na kufurahi mno tunaposikia mtu akisema: «Mashaallah» au «Barakallah»?! Mtu akituambia «Mashaallah» au «Barakallah», tunajaa furaha na kujiona wakubwa kiasi hiki!

Basi, thawabu ya kazi hii ni nini?!

Wakati huo huo, nilitafakari kwa kina na kusema: Tazameni, Mwenyezi Mungu anapopata nafasi ndani ya moyo wa mwanadamu, huingia na kutawala ndani ya nafsi yake kwa kiwango gani! Hali huwa hivi kiasi kwamba mtu huyu, licha ya kufanya tendo kubwa namna hii, huliona tendo hilo kuwa dogo sana machoni pake mwenyewe. Aidha, huichunga nafsi yake kwa umakini mkubwa kiasi kwamba hata anazingatia jambo hili na kusema: «Ikiwa siku moja nitajikuta nikifikiria kwamba mtu fulani anaweza kuja na kunisifu, akaniambia: Mtukufu, tafsiri hii uliyoandika, hongera! Hii ndiyo tafsiri bora kuliko zote; basi wakati huo nitahisi kiburi na kujiona mkubwa moyoni mwangu, na nitajivunia nafsi yangu. Kwa hiyo, thawabu ya kazi hii ni nini?!»

Kimsingi, yeye mwenyewe haipi kazi hii thawabu yoyote ndani ya moyo wake.

Hii ndiyo maana ya mafundisho ya Mitume. Hii ndiyo athari ya mafundisho ya Mitume yanapopenya ndani ya kina cha dhamiri ya mwanadamu, yanatawala uwepo wake na kuifanya nafsi yake itawaliwe na kushindwa mbele yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha