Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hashim Mousavi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Quetta, katika khutuba za Swala ya Ijumaa, amelaani uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza, ukandamizaji wa waumini nchini Bahrain na mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Amesisitiza kuwa mwenendo wa watawala wengi wa nchi za Kiislamu mbele ya mateso na dhuluma wanazofanyiwa wananchi wa Kiislamu unaonyesha kuwa wameshindwa katika mtihani wa Mwenyezi Mungu.
Akizungumzia hali ngumu wanayopitia wananchi wa Ghaza, hususan watoto, amesema: “Wananchi wanaodhulumiwa wa eneo hili wanakabiliwa na matatizo na mateso mengi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya adui pamoja na hali ngumu ya hewa. Hali yao ya kusikitisha na dhuluma wanazofanyiwa ni mtihani mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wanadamu wote, hususan watawala wa nchi za Kiislamu.”
Imam wa Swala ya Ijumaa wa Quetta ameongeza kuwa: “Kwa masikitiko, watawala wengi wa Kiislamu wameshindwa katika mtihani huu wa Mwenyezi Mungu. Msimamo na mwenendo wao mbele ya mateso na majanga yanayowakumba wananchi wa Palestina unastahili kutafakariwa na kuhojiwa kwa uzito.”
Aidha, akilaani ukandamizaji na mashinikizo yanayofanywa dhidi ya waumini nchini Bahrain, amesema: “Dhuluma na uonevu haviwezi kudumu milele. Madhalimu wanapaswa kufahamu kuwa matendo yao haya ya kidhalimu ndiyo yanayotayarisha mazingira ya kuanguka na kuangamia kwao, na hatimaye kufuta majina yao katika kurasa za historia.”
Hujjatul-Islam Sayyid Hashim Mousavi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, amelaani mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, akisema: “Utawala wa Aal Saud, ambao umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Yemen katika medani ya vita, unajaribu kuonyesha nguvu zake kwa kuwalenga wananchi wasio na ulinzi. Huu ni mwenendo unaodhihirisha dhuluma na woga.”
Maoni yako