Alhamisi 19 Novemba 2026 - 15:05
Wapenzi wa Ahlul-Bayt (as) waandika historia katika kuiaga nguzo ya elimu ya Fiqhi yenye msimamo wa Kiwilaya

Wakazi wa mji wa Qum, wanaoshikamana na Wilaya na wenye kuthamini mchango wa viongozi wao, walijitokeza kwa wingi katika mitaa inayoelekea kwenye Haram ya Bibi Fatimah Ma'asumah (as), si tu kwa ajili ya kusindikiza mwili mtakatifu wa mwanachuoni mmoja wa Fiqhi, bali pia kumuaga mwanazuoni aliyekuwa kielelezo cha Fiqhi yenye msimamo wa Kiwilaya. Ayatullah Wahid Khorasani alikuwa mfano halisi wa Fiqhi hiyo, huku mwenendo wake wa maisha ukidhihirisha ufuasi wa kweli wa dini katika zama zetu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, jana umati mkubwa wa wakazi wa Qum, hususan wanazuoni na wapenzi wa mafundisho ya Ahlul-Bayt wa Utume (as), walimsindikiza kwa mabega yao marji' mkuu wa kidini na mwanazuoni mahiri wa Fiqhi, ambaye kwa hakika alikuwa miongoni mwa watu adimu wa zama zake katika medani ya kiroho na elimu ya Fiqhi.

Kwa hakika, inapaswa kusemwa kwamba kufariki watu wa haki na wanazuoni mahiri wa Fiqhi wenye mchango mkubwa kama huyu katika jamii ya Kiislamu na Kishia si pengo la kawaida la kuondokewa na mtu tu. Bali, tunapotafakari kwa kina, ni pengo katika uwepo na mfumo wa maisha ya kiroho na kielimu. Ni kwa mtazamo huu hasa tunapopaswa kutafsiri kauli hii yenye thamani kubwa ya Mtume Mkuu (saw), aliposema:

«Mwanazuoni mwenye elimu ya kina ya Fiqhi anapofariki, hutokea ufa katika Uislamu ambao hakuna kitu kitakachoweza kuuziba mpaka Siku ya Kiyama.»

Kielelezo cha kudumu kwa wanaofuata njia ya elimu ya Fiqhi

Bila shaka, Ayatullah Al-Udhma Hussein Wahid Khorasani alikuwa miongoni mwa nguzo imara za elimu ya Fiqhi na mmoja wa vinara katika kufafanua na kueneza utamaduni safi wa Ahlul-Bayt (as).

Hakuna shaka kwamba juhudi zake imara na zisizoyumba katika kufafanua hukumu za Mwenyezi Mungu, pamoja na umakini wake wa kipekee katika kutoa hitimisho la hukumu za Fiqhi, ni tegemeo imara kwa Hawza za kielimu na kielelezo cha kudumu kwa wote wanaofuata njia ya elimu ya Fiqhi.

Jana, wakazi wa Qum wanaoshikamana na Wilaya na wenye kuthamini mchango wa viongozi wao, katika mitaa inayoelekea kwenye Haram ya Bibi Fatimah Ma'asumah (as), hawakusindikiza tu mwili mtakatifu wa mwanachuoni wa Fiqhi, hii ni kwa sababu marehemu Ayatullah Wahid Khorasani alikuwa kielelezo cha Fiqhi yenye msimamo wa Kiwilaya, huku mwenendo wake wa maisha ukidhihirisha ufuasi wa kweli wa dini katika zama zetu.

Wapenzi wa Ahlul-Bayt (as) waandika historia katika kuiaga nguzo ya elimu ya Fiqhi yenye msimamo wa Kiwilaya

Mafuriko ya wanafunzi katika mazishi ya mwalimu wa kipekee

Wanafunzi wengi ambao jana walihudhuria katika safu zilizoungana na zenye mshikamano, wakiwa wamejaa huzuni na machozi katika hafla hiyo adhimu ya mazishi ya mwili mtakatifu wa mwanazuoni huyu mkubwa, bila shaka wanathibitisha kwamba katika maisha yake, elimu ya Fiqhi ilikuwa nyenzo ya kuelewa yale yanayohitajika katika njia ya kumtumikia Mwenyezi Mungu, na baadaye katika kuonesha upendo na mapenzi kwa mafundisho ya Ahlul-Bayt (as). Kwa mtazamo huu, huduma zake za dhati na zenye kudumu zinapaswa kupimwa kwa mizani ya upendo kwa Maimamu Maasumu (as).

Upendo na mapenzi ya marehemu Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani kwa Familia Tukufu ya Mtume (saww), hususan Bibi Fatimah Zahraa (as), hayakuwa madai ya maneno tu, bali yalikuwa sehemu ya uwepo wake wa kiroho, ambayo yalijidhihirisha na kutiririka katika kila tendo na kila mtazamo wake.

Kuagwa kihistoria kwa sauti za “Ya Hussein (as)” na “Ya Zahraa (as)”

Umati mkubwa wa waombolezaji waliofurika katika mitaa ya katikati ya mji mtakatifu wa Qum, hususan maeneo yanayozunguka Haram tukufu ya Bibi wa Ahlul-Bayt (as), katika shughuli za mazishi ya jana, uliambatana na maombolezo na hasa sauti na nyimbo za huzuni za “Ya Hussein (as)” na “Ya Zahraa (as)”.

Hali hiyo ilifufua kumbukumbu muhimu za nyakati ambazo marehemu Ayatullah Wahid Khorasani, pamoja na kundi kubwa la wanazuoni, walikuwa wakishiriki katika shughuli za kuomboleza siku za kumbukumbu za shahada za Maimamu Maasumu (as), hususan katika siku za Fatimiyyah.

Kwa mapenzi na hisia zisizoweza kuelezeka, walikuwa wakitembea kutoka Mtaa wa Mashuhadaa (Safaiyeh), mjini Qum, kuelekea kwenye Haram tukufu ya Bibi wa Ahlul-Bayt (as), ili kuwasilisha rambirambi zao kwa Bibi Fatimah Ma'asumah (as), shangazi wa Maimamu Maasumu, kutokana na misiba iliyowapata Ahlul-Bayt (as).

Marehemu Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani alidhihirisha upendo na mapenzi yake kwa mafundisho ya Muhammad (saww) na Familia ya Muhammad (saww) kupitia uhusiano wa kina kati ya Fiqhi yenye msimamo wa Kiwilaya na mafundisho ya Ahlul-Bayt, pamoja na huduma kwa Umma.

Kwa hakika, mwenendo na historia hii yake yenye nuru ni funzo la hali ya juu kwa wote wanaofuata njia ya haki na ukweli, hususan wale ambao mioyo yao imefungamana na upendo wa Maimamu Watoharifu (as).

Utumishi mbele ya Ahlul-Bayt (as): Kutoka darasani hadi safu za waombolezaji

Pamoja na nafasi yake kubwa ya kielimu na daraja lake la juu katika elimu ya Fiqhi, miongoni mwa sifa muhimu na za kipekee za shakhsia ya Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani ilikuwa ni upendo wake wa dhati na utumishi wake wa kujitolea mbele ya Ahlul-Bayt wa Utume na Utakasifu (as).

Kwa sababu hiyo, alikuwa na hisia na uangalifu mkubwa kuhusu kuadhimisha alama na nembo za kidini zinazohusiana na Maimamu Maasumu (as), na alilichukulia jambo hilo kuwa jukumu la kudumu lililokuwa juu yake.

Marji' huyu wa kidini aliyefariki dunia na mwanazuoni huyu mpambanaji, miongoni mwa matukio yote ya kidini, alikuwa na juhudi na mapenzi ya pekee katika kuhuisha maombolezo ya Bibi Fatimah Zahraa (as).

Aidha, katika kipindi cha uhai wake, alisisitiza kwa namna ya pekee umuhimu wa kuifanya shughuli ya maombolezo ya Fatimiyyah (as) kuwa ya jumla na kuwahusisha waumini wengi zaidi, sambamba na uwepo wa vikundi na jumuiya za kidini katika njia na mitaa ya umma.

Kuadhimisha siku za Fatimiyyah (as): Wajibu ulio juu ya wapenzi wa Maimamu Watoharifu (as)

Wanachama wa vikundi vya maombolezo hawatasahau kwamba mwaka 1398 Hijria Shamsia, katika kuelekea siku za Fatimiyyah (as), Ayatullah Wahid Khorasani aliwaomba wanachama wa vikundi vya kidini, katika mojawapo ya hotuba zake, kujitokeza mitaani na kuandaa maandamano ya maombolezo, ili kutoa na kuonesha rambirambi zao kwa Amirul-Muuminina (as) na Ahlul-Bayt wengine (as).

Msisitizo wake ulikuwa kwamba maombolezo hayo yafanyike kwa namna inayoonesha wazi huzuni na rambirambi zao.

Hata mwaka 1399 Hijria Shamsia, wakati wa kilele cha kuenea kwa virusi vya Corona, alipoulizwa kuhusu namna ya kuendesha shughuli za maombolezo ya Fatimiyyah, alisisitiza kwamba shughuli za Fatimiyyah (as) hazipaswi kusimamishwa. Badala yake, zinapaswa kuendelezwa kwa namna bora zaidi, huku zikizingatiwa kanuni za afya na ushauri wa wataalamu.

Leo, siku chache tu baada ya shahada ya Ummu Abiha (Mama wa Baba yake) (as), umati mkubwa wa wapenzi wa Bibi Zahraa (as) ulikusanyika ili kumsindikiza hadi kwenye makazi yake ya milele mmoja wa watu waliokuwa na mapenzi ya dhati na ya kweli kwake.

Kwa hakika, wakazi wa Qum wanaoshikamana na Wilaya, pamoja na watu waliotoka maeneo mbalimbali, walitekeleza utaratibu huu mzuri kwa namna bora na kwa fahari kubwa. Hivyo, tarehe 27 mwezi wa Aban mwaka 1405 Hijria Shamsia (18 Novemba 2026 Miladia) nayo itaendelea kung'aa na kubaki katika historia ya Kishia na elimu ya Fiqhi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha