Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka mjini Mashhad, shughuli za mazishi na maziko ya mwili wa marehemu Ayatullah Wahid Khorasani zimeanza masaa machache yaliyopita katika Shule ya Ayatullah Khoei, mjini Mashhad, zikihudhuriwa na umati mkubwa wa wanazuoni, wawakilishi wa Maraji' Wakuu wa Taqilidi, wanafunzi na walimu wa Hawza ya Kielimu ya Khorasan, pamoja na wananchi wanaopenda na kuthamini nafasi ya Maraji' wa Kidini.
Kwa mujibu wa taarifa hii, shughuli za kusindikiza mwili wake mtakatifu zilianza leo, Alhamisi, kuanzia saa 9:00 asubuhi katika mji mtakatifu wa Mashhad. Shughuli hizo zilianzia katika Shule ya Ayatullah Al-Udhma Khoei, kisha msafara wa mazishi ukaingia katika Haram Tukufu ya Imamu Ridha (as) kupitia lango la Bab al-Jawad, na kuelekea katika eneo la Bast Shirazi. Baadaye, msafara huo ulipitia katika ukumbi wa Sahni Inqilab, Sahni Kauthar na Sahni Payambar A'zam (saww).

Hatimaye, mwili wa marehemu marji' huyu mkuu wa kidini ulihamishiwa katika ukumbi wa Dar al-Sa'adah kwa ajili ya kuzikwa.
Aidha, shughuli ya kuomboleza kifo cha marehemu Ayatullah Wahid Khorasani itafanyika leo Alhamisi, tarehe 28 mwezi wa Aban, baada ya Swala ya Magharibi na Isha, kwa niaba ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hafla hiyo itafanyika kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 2:00 usiku katika ukumbi wa Imam Khomeini (ra), ndani ya Haram Tukufu ya Imamu Ridha (as).
Kwa lengo la kuwezesha kufanyika shughuli za mazishi na maziko ya mwili mtakatifu wa Ayatullah Wahid Khorasani, vizuizi vya kupita kwa magari binafsi vimewekwa katika barabara ya Shirazi na barabara ya Shahid Andarzgoo, zinazoelekea kwenye Haram Tukufu.

Mwili wake utazikwa katika ukumbi wa Dar al-Sa'adah, eneo lililopo upande wa chini wa miguu ya kaburi tukufu la Imamu Ridha (as), katika sehemu maalumu ya wanawake.
Mahali pa kuzikwa marehemu huyu pamechaguliwa kwa kuzingatia wosia wake pamoja na ombi la familia yake.

Maoni yako