Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Ali al-Gharawi, mhadhiri wa sheria nchini Iraq, katika mahojiano na tovuti ya habari ya Al-Ahd, alisema kuwa; iwapo Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel watafanya tena uchokozi dhidi ya Iran, Iraq inapaswa kuchukua hatua kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa.
Alifafanua kuwa; jambo hilo halimaanishi kujiunga na madola ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kinyume chake, Iraq haipaswi kuruhusu ardhi wala anga yake kutumiwa kwa ajili ya kufanya uchokozi dhidi ya nchi yoyote jirani, kwa kuzingatia Katiba yake inayokataza ardhi na anga ya Iraq kutumiwa kama kituo au jukwaa la kufanyia mashambulizi dhidi ya nchi jirani.
Al-Gharawi aliongeza kuwa; Iraq inapaswa pia kutumia nafasi na umuhimu wake wa kimkakati katika kuhamasisha nchi zinazozunguka eneo hilo ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya amani.
Aliendelea kusema kuwa, kwa upande wa wananchi wa Iraq, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wananchi watakuwa na nafasi hai na yenye ushawishi, kama walivyofanya wakati wa uchokozi uliopita.
Alieleza kuwa wito wa Ayatullah al-Udhma Sayyid Sistani ulikuwa na athari kubwa katika kuunga mkono muungano wa ndani wa Iran na kuulinda dhidi ya mifarakano na migawanyiko. Aidha, wafuasi wa Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao) nchini Iraq walionesha msimamo wa kujivunia kwa kushirikiana na wananchi wa Iran katika kukabiliana na mateso na machungu waliyokuwa wakiyapitia.
Maoni yako