Alhamisi 29 Oktoba 2026 - 23:00
Jumuia ya Wanazuoni wa Iraq, Yatoa Onyo Kali kwa Watawala wa Kuwait

Hawza/ «Jumuia ya Wanazuoni wa Iraq» imelaani, kupitia taarifa yenye lugha kali, kukamatwa idadi ya wawakilishi, wanazuoni wa dini, wahutubu na watu mashuhuri wa kijamii wa Kishia nchini Kuwait.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, «Jumuia ya Wanazuoni wa Iraq» imelaani, kupitia taarifa yenye lugha kali, kukamatwa idadi ya wawakilishi, wanazuoni wa dini, wahutubu na watu mashuhuri wa kijamii wa Kishia nchini Kuwait. Taasisi hiyo ya kidini, huku ikieleza wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo ya hatua hizi imeonya kwamba; kuwalenga raia kwa misingi ya mwelekeo wao wa kidini, mbali na kukiuka haki za kiraia na kisiasa, kunatishia utulivu wa kijamii na kupanua zaidi ufa kati ya utawala na wananchi.

Maandishi ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Taarifa ya kulaani iliyotolewa na «Jumuia ya Wanazuoni wa Iraq» kuhusu hali wanayokabiliana nayo wafuasi wa madhehebu ya Kishia nchini Kuwait

Kwa maneno makali kabisa, tunalaani kukamatwa idadi ya wawakilishi, wanazuoni wa dini, wahutubu, wasomi na watu mashuhuri wa kijamii wa Kishia nchini Kuwait, pamoja na hatua za ukandamizaji zinazoambatana na matukio hayo, ambazo zimechukuliwa kwa misingi ya ubaguzi wa kimadhehebu unaochukiwa.

Tunaeleza wasiwasi na huzuni yetu kubwa kuhusu matokeo yanayoweza kusababishwa na hatua hizi, ikiwemo ukiukaji wa haki za kisiasa, kiraia na kidini, pamoja na kutishia misingi ya usawa wa uraia, uhuru wa itikadi na ushiriki katika maisha ya kijamii.

Kumchukulia hatua raia yeyote kwa sababu ya uhusiano wake wa kimadhehebu iwapo jambo hilo litathibitishwa, ni ukiukaji mkubwa wa misingi ya haki na usawa. Hatua za aina hii hazitatui tatizo lolote, bali zinazidisha mvutano, zinapanua zaidi ufa kati ya utawala na wananchi, na zinapingana na muundo wa kijamii wa nchi.

Tunatoa onyo dhidi ya vitendo vya mateso na unyanyasaji vinavyotokana na misingi ya kidini, kwa sababu vina matokeo hatari kwenye umoja na utulivu wa jamii.

Tunasisitiza kwamba «kuwa Shia» si tuhuma, «kuwaamini Ahlul-Bayt (as)» si uhalifu, na «kudai haki halali zinazotambuliwa na sheria na katiba» si kwenda kinyume na sheria.

Kuwepo wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (as), wanazuoni, wahutubu, pamoja na haki yao ya kuendesha shughuli za kidini, kueleza itikadi zao na kushiriki katika maisha ya kijamii, ni haki za msingi ambazo hazipaswi kuvamiwa wala kupunguzwa.

Tunatoa wito wa kuwepo  dhamana za kisheria zilizo za haki, kupinga ukamataji wa kiholela na tuhuma zisizo na ushahidi ulio wazi. Vilevile, tunasisitiza umuhimu wa kuhakikisha haki na uhuru wa waliokamatwa, pamoja na kuwaachilia huru wote ambao mashtaka dhidi yao hayajathibitishwa katika kesi ya haki inayofanyika kwa kufuata taratibu za kisheria zilizo za haki.

Tunasisitiza kwamba; msimamo wa Hawza, wanafunzi wa elimu za kidini na wanazuoni kuhusu kukataa dhuluma na ubaguzi uko wazi. Tunaonya pia kuhusu matokeo hatari ya hatua hizi kwa tabaka la kijamii na utulivu wa kitaifa.

Aidha, tunaziomba mamlaka za Kuwait kuzingatia nafasi muhimu, yenye heshima na ya kizalendo ya Mashia, hususan kujitolea kwao na misimamo yao katika kutetea ardhi ya Kuwait na kusimama pamoja na nchi yao wakati wa uvamizi wa Saddam.

Historia inatufundisha mafunzo ambayo hayapaswi kupuuzwa. Miongoni mwa mafunzo hayo ni hatima ya dhalimu kama Saddam, aliyewatesa wafuasi wa taifa la Iraq, hususan Mashia, na kuwakandamiza wapinzani wake mpaka mambo yalipofikia hatima ile inayojulikana.

Dhuluma haidumu, na matokeo yake hayawaathiri tu wale wanaodhulumiwa, bali pia huwafikia madhalimu wenyewe, jamii na nchi. Vilevile, tunawaomba wanazuoni wa Kiislamu, taasisi za kidini na za haki za binadamu, wananchi na serikali kutekeleza wajibu wao wa kisheria, kimaadili na kibinadamu katika kuwasaidia wanaodhulumiwa, kutetea haki za raia wa Kishia na kupinga kila aina ya ubaguzi na ukandamizaji wa kidini, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyosema:

«كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّهِ»

«Kuweni wenye kusimamia uadilifu na mashahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.»

Je, utukufu wa Muumini na heshima yake haviashirii kwamba dhamiri ya Kiislamu inapaswa kuchochewa ili imsaidie?

Je, si jambo la lazima kwa wanazuoni na taasisi za haki za binadamu kusimama dhidi ya dhuluma, na kuwasadia wanaodhulumiwa kuwa wajibu wa kisheria na kibinadamu usiotambua mipaka ya kijiografia wala tofauti za madhehebu?!

Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba kwa haki ya Muhammad na Aali Muhammad uwalinde wafuasi wa Amirul-Muuminina (as) nchini Kuwait na katika ardhi nyingine za Waislamu; uwaokoe kutokana na matatizo yanayowakabili; uondoe dhuluma dhidi ya wanaodhulumiwa; uharibu hila za madhalimu; ulipandishe juu neno la haki na usimamishe uadilifu. Hakika Wewe ni Mwenye kusikia na Mwenye kuitikia maombi.

Jumuia ya Wanazuoni wa Iraq

16 Jumada al-Ula 1448 Hijria

27 Oktoba 2026 Miladia

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha