Jumamosi 24 Oktoba 2026 - 11:38
Maombolezo ya Bibi Fatima Zahra (sa) ni Kuifanya Upya Ahadi ya Kushikamana na Malengo ya Ahlul-Bayt (as)

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Muhammad Hassan Jaafari, huku akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu ya dhuluma alizofanyiwa Bibi Fatima Zahra (sa), amesema kuwa; kushiriki katika majlisi za maombolezo ya Bibi huyo mtukufu ni dhihirisho la mapenzi yanayoonekana kwa vitendo na uhusiano wa moyo na Ahlul-Bayt (as).

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Muhammad Hassan Jaafari, mwanazuoni mashuhuri wa Pakistani, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa mji wa Skardu, eneo la Baltistan nchini Pakistan, alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu ya dhuluma alizofanyiwa Bibi Fatima Zahra (sa). Alieleza kuwa kushiriki katika majlisi za maombolezo ya Bibi huyo mtukufu ni dhihirisho la mapenzi yanayoonekana kwa vitendo na uhusiano wa moyo na Ahlul-Bayt (as).

Umuhimu wa kuheshimu siku za Fatimiyya na kushiriki katika huzuni ya Ahlul-Bayt (as)

Akizungumzia kufika siku za Fatimiyya, aliwaomba waumini watambue nafasi tukufu ya Bibi Fatima Zahra (sa) na kuzingatia misiba iliyowapata Ahlul-Bayt (as). Aliwataka kujiepusha na kufanya sherehe za furaha katika siku hizo, zikiwemo sherehe za harusi, na iwapo itawezekana waziahirishe hadi baada ya kumalizika kwa siku za Fatimiyya.

Alisema: “Katika siku hizi, familia ya Mtume Mkuu wa Mwenyezi Mungu (saww) iko katika maombolezo ya Bibi Fatima Zahra (sa). Kwa hiyo, inatupasa nasi kukumbuka dhuluma alizofanyiwa Bibi huyo mtukufu, kushiriki katika majlisi za huzuni na maombolezo, na kuonesha kwa vitendo mapenzi yetu na uhusiano wa moyo wetu na Ahlul-Bayt (as).”

Imam wa Swala ya Ijumaa wa mji wa Skardu alieleza matumaini yake kwamba, kuheshimu siku za Fatimiyya na kushiriki katika huzuni ya Ahlul-Bayt (as) kutakuwa sababu ya waumini kupata wokovu na kunufaika na uombezi wa Bibi Fatima Zahra (sa).

Nafasi yenye kuamua ya watu mashuhuri katika kuirekebisha au kuipotosha jamii

Katika kuendelea na hotuba zake, akifafanua nafasi ya watu mashuhuri na wenye ushawishi katika hatima ya jamii, alibainisha kwamba wanazuoni wa dini, wenye mamlaka, wanafikra na shakhsia nyingine zenye ushawishi wanaweza, kupitia maamuzi na tabia zao, kubadilisha mwelekeo wa jamii na kuielekeza kwenye marekebisho na maendeleo au kwenye upotovu na uharibifu.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hassan Jaafari, aliongeza kusema kwamba; watu mashuhuri walio katika safu ya haki wanaweza, kwa kuwa na utambuzi sahihi, kutenda kwa uwajibikaji na kufanya juhudi za pamoja, kuweka mazingira ya amani, umoja na marekebisho ya kijamii. Kinyume chake, mwenendo mbaya wa watu mashuhuri walio katika safu ya batili hueneza tofauti, migawanyiko na ufisadi katika jamii.

Akizungumzia hali ya kihistoria ya Madina kabla ya Hijra ya Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saww), alisema: “Yathrib, kabla ya kuwasili Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), ilikuwa imekumbwa na migogoro ya kikabila, uadui wa muda mrefu na umwagaji damu. Hata hivyo, uwepo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) na mafundisho yake ya Mwenyezi Mungu viliweka mazingira ya kuugeuza mji huo kuwa kitovu cha amani, udugu na umoja.”

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Pakistani alisisitiza kwamba kila mtu anapaswa, kabla ya jambo jingine lolote, kufanya tathmini ya nafsi yake na kuchunguza mwenendo na utendaji wake. Aidha, anapaswa kujiunga na safu ya watu mashuhuri walio katika upande wa haki na kupiga hatua katika njia ya kusimamisha uadilifu, kurekebisha jamii, kuimarisha umoja na kuhakikisha manufaa ya umma.

Akizungumzia vitisho na shinikizo zinazoweza kutolewa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, alisema kuwa; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipuuzi vitisho hivyo na inaendelea kufanya juhudi za kuimarisha uwezo wake wa kujilinda, hususan katika nyanja za teknolojia ya makombora na ndege zisizo na rubani.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa mji wa Skardu, akizungumzia matatizo ya kiuchumi na kuongezeka gharama za maisha nchini Iran, aliongeza kusema kwamba; licha ya changamoto za kimaisha, wananchi wa Iran wamehifadhi moyo wao wa umoja, subira na ustahimilivu, na wanaendelea kusimama imara na kwa mshikamano mbele ya maadui.

Alieleza kwamba, moyo huu wa kitaifa umetokana na kujitolea kwa mashahidi, hususan Kiongozi Shahidi, Ayatullah Al-Udhma Sayyid Ali Khamenei. Alimuomba Mwenyezi Mungu awape wananchi wa Iran ushindi na heshima, awanusuru kwa msaada Wake, na akomeshe uchokozi wa utawala wa Kizayuni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha