Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Mahdi Takht-Firuzeh, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Msikiti Mkuu wa Dar al-Ihsan mjini Sanandaj na mwakilishi wa wananchi wa Sanandaj katika Baraza la Kiislamu la Jiji hilo kwa vipindi vitatu, alitoa matamshi hayo katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa “Mwamko wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w.)”, uliofanyika Jumatano, tarehe 29 Mehr 1405, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun.
Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa umoja wa Umma wa Kiislamu na kueleza kuwa msimamo thabiti wa taifa la Iran dhidi ya shinikizo na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni ni miongoni mwa dhihirisho muhimu za mapambano na kushikamana na tunu za Kiislamu.
Takht-Firuzeh aliutaja umoja miongoni mwa Waislamu kuwa ni wajibu wa kidini na mkakati muhimu. Akirejelea msisitizo wa Qur’ani Tukufu kuhusu kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu, alisema kuwa mshikamano wa Umma wa Kiislamu unaweza kuweka mazingira ya kukabiliana na njama mbalimbali na kuhifadhi heshima pamoja na uhuru wa nchi za Kiislamu.
Akizungumzia mashambulizi na uharibifu uliosababishwa kwa miundombinu, kuuawa shahidi kwa makamanda na wanasayansi, pamoja na kuuawa kwa watoto, aliituhumu Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kuiwekea Iran shinikizo na kuchukua hatua za uhasama dhidi yake. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa macho na kujiandaa kukabiliana na mabadiliko na matukio hayo.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Masayyid wa Mkoa wa Kurdistan alieleza kuwa; taifa la Iran linataka kuishi kwa uhuru na kuhifadhi uhuru wake wa kujitawala, alisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kusimama imara dhidi ya shinikizo kutoka nje kwa kudumisha umoja na mshikamano, na kutoruhusu tofauti baina yao kudhoofisha nguvu na mshikamano wao.
Aidha, Takht-Firuzeh alirejelea mafundisho ya Kiislamu kuhusu kuwaheshimu Mitume na dini za Mwenyezi Mungu, akisisitiza kuwa Uislamu unawaelekeza wafuasi wake kuhifadhi heshima ya Mitume na kuheshimu mambo matakatifu, alibainisha kuwa umoja wa Umma wa Kiislamu unapaswa kuimarishwa kwa kuzingatia tunu za kidini na kujiepusha na mifarakano.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, mwanaharakati huyo wa masuala ya utamaduni na kijamii alieleza kuwa shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran linakumbusha namna Waislamu walivyozingirwa kiuchumi katika zama za mwanzo za Uislamu. Akirejelea matatizo aliyokabiliana nayo Mtume Muhammad (s.a.w.w.), Ahlul-Bayt (a.s.) na maswahaba wake, alisisitiza umuhimu wa subira, ustahimilivu na kudumisha matumaini wakati wa kukabiliwa na changamoto.
Mwisho wa hotuba yake, Takht-Firuzeh aliashiria umoja wa Waislamu, kushikamana na mafundisho ya Qur’ani Tukufu na kupambana na shinikizo kutoka nje kuwa ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya mwamko wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w.). Alieleza matumaini yake kuwa taifa la Iran na Umma wa Kiislamu, kwa kudumisha mshikamano na msimamo thabiti, vitaendelea na safari ya kuelekea kwenye heshima na mafanikio.
Maoni yako