Ijumaa 23 Oktoba 2026 - 07:29
Utamaduni wa Ahlul-Bayt (as) Una Wafuasi Wengi Duniani/ Tuwasilishe Maarifa ya Dini kwa Lugha na Mtindo wa Kisasa

Hawza/ Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini (ra), huku akisisitiza kuwa uzuri wa utamaduni tajiri wa Uislamu na Ahlul-Bayt (as), kutokana na kuafikiana kwake kikamilifu na akili na maumbile ya asili ya mwanadamu, una mvuto mkubwa kwa watu katika pembe mbalimbali za dunia, amesema: Wajibu wa tablighi ya kimataifa hutimia pale ujumbe wa dini unapojikita ndani kabisa ya nafsi na fikra za walengwa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mahmoud Rajabi aliyasema hayo katika mkutano wake na mkuu pamoja na viongozi wa ofisi ya uwakilishi wa Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu mjini Qum Iran, pamoja na wajumbe wa Kongamano la Tuzo ya Kimataifa ya Shahidi Sadr, uliofanyika katika Taasisi ya Imam Khomeini (ra).

Alisema: “Uislamu umeteremshwa ili kuwaita wanadamu waielekee tamaduni ya Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa matini za riwaya za Maimamu Maasumina (as), iwapo mataifa ya dunia yatafahamu uzuri wa maneno na mvuto wa utamaduni wa Ahlul-Bayt (as), yatauelekea kwa shauku kubwa. Hii ni kwa sababu mafundisho haya yanaafikiana kikamilifu na maumbile ya asili ya mwanadamu pamoja na mantiki ya kiakili. Kwa msingi huo, uwekezaji wowote wa kifedha, maandalizi ya vifaa na rasilimali watu, pamoja na kuwatumia wataalamu mahiri katika njia hii, hauwezi kusemwa kuwa ni mwingi kupita kiasi. Ufanisi wa juhudi hizi unategemea moja kwa moja aina ya mipango inayowekwa na kiwango cha ulinganifu wa uwezo wa watu wanaopelekwa katika maeneo ya utekelezaji.”

Mkuu huyo wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini (ra), akizungumzia yale aliyojionea mwenyewe katika safari za nje za tablighi, aliongeza: “Uzoefu unaonesha kuwa kila mahali ambapo mtu mwenye uelewa, fikra pana na ufahamu wa utamaduni tajiri wa Kiislamu pamoja na undani wa kazi za kiutamaduni alipokuwepo, mtu huyo amekuwa chanzo cha baraka nyingi na athari za kudumu. Ameweza kufikisha ujumbe halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika mizani yote ya shughuli hizi jambo la kwanza na lenye nafasi muhimu zaidi ni rasilimali watu wenye sifa zinazostahili. Hii ni kwa sababu mtu mwenye ufanisi anaweza kufidia na kurekebisha upungufu wa vifaa na mifumo ya kiutendaji, lakini mtu asiye na sifa zinazohitajika hupoteza fursa bora kabisa.”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu za Kidini nchini humo aliongeza: “Katika mojawapo ya safari zilizofanyika nchini Thailand mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kutokana na kutokuwepo mshauri wa utamaduni, kaimu wa ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu alikuwa amechapisha kitabu cha kuyatambulisha madhehebu ya haki ya Shia. Hata hivyo, katika utangulizi wa kitabu hicho bila kukusudia, alithibitisha na kusambaza shubha ya zamani na batili iliyobuniwa na Wayahudi, ambayo ni madai kwamba kuasisiwa Ushia kunatokana na Abdullah bin Saba. Hilo lilikuwa kosa kubwa lililoonesha matokeo mabaya na yenye madhara yanayoweza kusababishwa na kutokuwa na ujuzi kwa wale wanaosimamia masuala hayo.”

Alisisitiza umuhimu wa kuweka mfumo maalumu wa kuandaa na kuwafundisha washauri wa utamaduni katika Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu, akasema: “Shirika lolote lenye majukumu maalumu linapaswa angalau kuandaa kozi fupi za mafunzo na stadi zinazolingana na malengo yake. Katika kipindi fulani, Bw. Mostafavi, aliyekuwa mkuu wa shirika hilo wakati huo, alikwenda kukutana na Allamah Misbah Yazdi (ra), Katika kikao hicho Allamah alitangaza rasmi kuwa sisi katika taasisi yetu tuko tayari kubuni na kutekeleza kozi za kitaaluma na za kuandaa watumishi wenye uwezo, kulingana na majukumu ya shirika hilo.”

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisema: “Hata leo, kuna ulazima wa kuwaandaa watu wenye imani thabiti, wanaofahamu mifumo na taratibu za kiutamaduni, waliobobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na wenye uelewa mpana wa misingi ya Kiislamu.

Watu hao wanapaswa kuwa na nyaraka zilizopangwa na zenye taarifa za kina kuhusu hali ya nchi wanayolenga, ili waanze shughuli za tablighi katika hatua ya maendeleo iliyofikiwa tayari, badala ya kuanza kwa kutegemea majaribio na makosa.”

Ayatullah Rajabi, aliashiria aya tukufu ya Qur’ani isemayo:

«فَذَكِّرْ إِنَّ الذِّكْرَیٰ تَنْفَعُ الْمُؤْمِنِینَ»

“Basi kumbusha, kwani hakika ukumbusho huwanufaisha Waumini.”

Aliashiria kanuni ya kuzingatia uzalishaji wa “kazi bora na zenye thamani ya juu” kuwa ni jambo la kimkakati, akafafanua: “Kutengeneza kazi moja iliyo imara, madhubuti na inayokidhi viwango ni jambo lenye ufanisi mkubwa zaidi kuliko kuchapisha vitabu vingi dhaifu na visivyokuwa na mvuto kwa wasomaji. Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika safari yake ya mwisho mjini Qum, alipokutana na wajumbe wa Baraza Kuu la Hawza, alisisitiza wazi kwamba kazi ya mtafiti haikamiliki kwa kuandika kitabu tu, Badala yake jukumu lake humalizika pale maudhui hayo yanapojikita ndani kabisa ya nafsi, moyo na fikra za msomaji.”

Aliongeza: “Ufuatiliaji endelevu wa maoni na mwitikio wa walengwa, pamoja na tathmini ya moja kwa moja ya kiwango cha ufanisi wa kazi ni nguzo muhimu sana katika shughuli za kiutamaduni. Imam Khomeini (ra) na Kiongozi Shahidi pia walikuwa wakisisitiza daima uwezo mkubwa wa utamaduni wa kupenya ndani ya jamii na kuathiri watu, tukiwawasilishia watu maarifa ya dini kwa fasihi inayofaa na lugha ya kisasa, umma utaweza kujinasua kutokana na mvuto wa juu juu wa tamaduni potovu na tupu za kimaada.”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alirejelea mpango wa kihistoria wa Ayatullah Misbah Yazdi (ra) wa kuutambulisha Uislamu na madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) duniani, akakumbushia: “Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kitabu Kuitambua Dini ya Uislamu, kilichoandikwa na Shahidi Beheshti na Shahidi Bahonar, kilikuwa tayari kimeandaliwa. Hata hivyo, Allamah Misbah alibuni mpango mpya ili mfumo mzima na kamili wa mafundisho ya Uislamu uandikwe si katika juzuu nyingi, ndefu na zinazochosha, bali katika matini madhubuti zinazotegemea vyanzo vinavyokubaliwa kwa pamoja na Waislamu na wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu.”

Utamaduni wa Ahlul-Bayt (as) Una Wafuasi Wengi Duniani/ Tuwasilishe Maarifa ya Dini kwa Lugha na Mtindo wa Kisasa

Ayatullah Rajabi aliongeza: “Mpango huo ulijumuisha miundo 14 ya kitaalamu na ya jumla, iliyokusudiwa kwa makundi manne ya walengwa: umma kwa ujumla, vijana balehe, wanafunzi wa vyuo vikuu, pamoja na wasomi na wahadhiri wa vyuo vikuu. Kwa kila kundi, maudhui yalipaswa kuandaliwa katika maeneo manne ya kimadhehebu na kidini: maudhui yanayokubaliwa na Waislamu wote bila kujali madhehebu yao; maudhui mahsusi yanayohusu madhehebu ya Shia; maudhui yanayolingana na mahitaji ya wafuasi wa dini zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu; na maudhui yanayowalenga wafuasi wa falsafa na dini zisizotokana na wahyi.

“Ingawa baadhi ya sehemu za maarifa ya Qur’ani za Allamah zilichapishwa katika mitandao ya kijamii na kupokelewa kwa mwitikio mkubwa na wanazuoni wa Ahlus-Sunna, bado kuna umuhimu wa kuupitia upya mfumo huu wa vipengele 12 na kuutekeleza kwa kushirikiana na Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu.”

Mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza mjini Qum, akieleza uwezo wa kitaaluma wa Taasisi ya Imam Khomeini (ra) katika kuzalisha nadharia za Kiislamu katika nyanja za sayansi za kibinadamu na sayansi za Kiislamu, alisema: “Katika eneo la falsafa za taaluma mbalimbali, takribani juzuu 16 za vitabu vyenye thamani kubwa kuhusu falsafa ya sayansi, falsafa ya sayansi za kijamii na falsafa za taaluma mbalimbali za sayansi za kibinadamu kwa mtazamo wa Kiislamu zimefikia hatua ya mwisho ya maandalizi au zimekwishaandikwa.

“Vilevile, tafsiri za Kiarabu na Kiingereza za kazi za Allamah Misbah katika nyanja za maarifa ya Qur’ani, falsafa ya Kiislamu na ‘irfani ya Kiislamu’ zina uwezo wa kipekee wa kutumika katika taasisi za kitaaluma za Magharibi. Kazi hizi zinawasilisha nadharia iliyosafishwa na iliyoandaliwa kwa umakini, iliyoepushwa na upotovu, misimamo ya kupitiliza mipaka na uzembe, huku ikiegemezwa katika mafundisho ya Ahlul-Bayt (as).”

Ayatullah Rajabi aliendelea kusema: “Vilevile, ‘Waraka wa Uzalishaji wa Sayansi za Kibinadamu za Kiislamu’, ulioandaliwa na taasisi hii na kuwa msingi wa kuanzishwa kituo maalumu cha sayansi za kibinadamu za Kiislamu, umeandaa fursa nzuri kwa ajili ya kushiriki katika majukwaa ya kimataifa ya mijadala ya kitaaluma na kiakili.”

Alielezea utajiri wa kielimu na ubunifu uliomo katika matini za Kiislamu kuwa ni wa kipekee, akiongeza: “Tafiti zilizofanywa katika mojawapo ya vituo vya Hawza mjini Qum kuhusu matatizo ya kijamii na sosholojia ya upotovu zilithibitisha kuwa aya za Qur’ani na riwaya zina nadharia bunifu ambazo bado hazijajitokeza katika tafiti za kisasa za kibinadamu.

“Kwa mfano, katika kuchambua nadharia ya ‘ushirikiano wa karibu unaochochea uhalifu’ (differential association theory), kwa kulinganisha riwaya na aya za Qur’ani, tuligundua mambo ya kushangaza na yenye umuhimu mkubwa. Baadhi ya mambo hayo yamefafanuliwa wazi katika kitabu Maadili katika Qur’ani.”

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisema: “Kiongozi Shahidi alikuwa akikumbushia kwamba ni kiasi gani wanadamu hulazimika kufanya juhudi nyingi, kujaribu na kurekebisha makosa yao kabla ya kufikia sehemu ndogo tu ya maarifa, ilhali sisi tumeketi kando ya bahari isiyo na mipaka ya elimu za Qur’ani bila kunufaika nayo ipasavyo. Kushikamana na chanzo hiki kitakatifu ndio kichocheo muhimu zaidi cha maendeleo ya kielimu, kuondoa kutoelewana na kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu.”

Mwisho, Ayatullah Rajabi alisifu uamuzi wa kuitaja Tuzo ya Sadr kwa jina la mwanazuoni na mwanafikra mashuhuri, Shahidi Ayatullah Sayyid Muhammad Baqir Sadr (quddisa sirruh), akimtaja kuwa alikuwa mwasisi wa nadharia za kipekee na mwenye mchango mkubwa katika kufungua njia za kielimu.

Alisema: “Kwa mujibu wa mfumo wa malezi ya kielimu wa Allamah Misbah Yazdi, kila tunapokuwa na uwezo wa kutekeleza jukumu fulani lakini tukalipuuza, hatutakuwa na udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huo, Taasisi ya Imam Khomeini (ra) iko tayari kushirikiana na Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha