Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Baraza la Mkoa wa Najaf Tukufu limeidhinisha kwa kauli moja ya wajumbe wake pendekezo la kuinua hadhi ya kiutawala ya wilaya ya kihistoria na kidini ya Kufa na kuifanya kuwa mkoa mpya wenye jina rasmi la “Kufa Tukufu”.
Kwa mujibu wa maelezo ya pendekezo hilo, ambalo awali liliwasilishwa na wajumbe wa Baraza la Mkoa, akiwemo Dkt. Sobhi Wahid al-Hiyawi na wawakilishi wengine, uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia nafasi kubwa ya kidini, kihistoria na kistaarabu ya mji wa Kufa. Mji huo unachukuliwa kuwa mji mkuu wa kwanza wa utawala wa Kiislamu baada ya Madina Tukufu, chini ya uongozi wa Amirul Muuminina Imam Ali bin Abi Talib (a.s.). Aidha, uamuzi huo unalenga kuheshimu na kuthamini msimamo wa muqawama na uvumilivu ulioonyeshwa na wakazi wa mji huo katika mazingira magumu ambayo Iraq imepitia.
Sababu nyingine zilizotolewa kuunga mkono pendekezo hilo ni pamoja na uwepo wa misikiti na makaburi matukufu katika mji huo, kupokea mamilioni ya mazuwari katika kipindi chote cha mwaka, upanuzi mkubwa wa shughuli za ujenzi na maendeleo ya miji, pamoja na ongezeko endelevu la idadi ya wakazi wa Kufa na maeneo yanayoizunguka. Mambo hayo yameongeza zaidi umuhimu wa kuwa na usimamizi huru wa kiutawala na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Uamuzi huo, baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria na kiutawala zinazohitajika, unachukuliwa kuwa hatua muhimu kuelekea maendeleo yenye uwiano, pamoja na kuthamini na kuenzi nafasi ya kidini ya mji huu wa Kiislamu.
Maoni yako