Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Abduljabbar Fahdawi, Mkuu wa Bodi ya Utawala ya Baraza la Riba't Muhammadi nchini Iraq, aliyasema hayo katika kikao cha sita cha kimataifa cha “Mwamko wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w.)”, kilichofanyika Jumatano, tarehe 29 Mehr 1405 Hijria ya Shamsi, kikiandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun.
Akisisitiza umuhimu wa umoja wa Umma wa Kiislamu, kuimarisha nguvu ya ulimwengu wa Kiislamu na kukabiliana na njama za maadui alieleza kuwa; umoja wa Waislamu ni suala la hatima katika kulinda heshima na utambulisho wa Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Katika hotuba yake, Sheikh Abduljabbar Fahdawi alirejelea mafundisho ya Qur’ani Tukufu na kueleza kuwa umoja wa Umma wa Kiislamu haupaswi kuchukuliwa kuwa ni kaulimbiu tu, bali ni ulazima wa msingi kwa ajili ya kulinda heshima, nguvu na misingi ya Kiislamu.
Akirejelea aya za Qur’ani Tukufu zinazozungumzia umoja wa Umma na umuhimu wa kujiandaa kukabiliana na maadui alisisitiza kuwa; Waislamu wanapaswa kukusanyika chini ya bendera ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), licha ya tofauti zao za kimadhehebu na kimtazamo. Alieleza kuwa wanapaswa kuimarisha uhusiano wa kindugu baina yao na kujiepusha na mifarakano na migawanyiko.
Mkuu wa Bodi ya Utawala ya Baraza la Riba't Muhammadi nchini Iraq, akirejelea hadithi ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) kuhusu kuhurumiana na kushirikiana katika maumivu baina ya Waumini, aliufananisha Umma wa Kiislamu na mwili mmoja, ambapo maumivu na matatizo yanayoikumba sehemu yoyote ya mwili huo yanapaswa kuwa jambo linalozigusa na kuzihangaisha sehemu nyingine zote.
Aidha, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo na nguvu za ulimwengu wa Kiislamu, alizungumzia uwezo uliopo katika nchi za Kiislamu wa kuutetea Uislamu na ardhi za Waislamu. Alizitaja Iraq, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Lebanon na Yemen kuwa ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza wajibu muhimu katika uwanja huo. Fahdawi alisisitiza umuhimu wa mshikamano na kuunga mkono uwezo uliopo katika ulimwengu wa Kiislamu ili kukabiliana na vitisho.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, mwanazuoni huyo wa Iraq aliashiria uanzishaji wa mahusiano ya kawaida na utawala wa Kizayuni, ushawishi wa kiutamaduni na kimawasiliano kutoka Magharibi, pamoja na mipango ambayo, kwa mujibu wa mtazamo wake, kunalenga kudhoofisha utambulisho wa Kiislamu, kuwa ni miongoni mwa mambo yanayotishia umoja wa Umma wa Kiislamu. Hivyo, alitoa wito kwa Waislamu kuwa macho na makini wanapokabiliana na mwenendo huo.
Akieleza kuwa Umma wa Kiislamu unakabiliwa na matukio yenye athari kubwa kwa hatima yake, alisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kuwa na msimamo wa pamoja, kuimarisha umoja wao na kuongeza uwezo wao wa kujilinda ili kuhifadhi misingi na tunu za Kiislamu.
Mwisho, Sheikh Abduljabbar Fahdawi alieleza kuwa; ushindi wa Uislamu na Waislamu unategemea mshikamano, nguvu na msimamo thabiti wa Umma wa Kiislamu. Alisisitiza umuhimu wa kuugeuza umoja kutoka kuwa kaulimbiu ya maneno pekee na kuufanya kuwa hatua za vitendo kwa ajili ya kulinda heshima na mustakabali wa Umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Maoni yako