Jumatatu 28 Septemba 2026 - 17:52
Iran Haitarejea Katika Kipindi Ambacho Adui Anakitamani

Hawza/ Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Kwa neno moja; Iran haitarejea katika kipindi ambacho adui anakitamani.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husayni Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Mkuu wa Majeshi yote, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku za mwanzo za vita vya kwanza vya kulazimishwa na maadhimisho ya siku tukufu za ulinzi wa miaka nane uliofanywa na kudumishwa na wananchi wa Iran, huku akizungumzia juhudi za madola yenye kutawala ulimwengu za kuirejesha Iran katika kipindi cha kudumaa, “udhalilifu na unyonge”, utegemezi na sifa mbaya, kupitia kulazimisha vita katika muongo wa kwanza wa Mapinduzi, amesisitiza kwamba: Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa, mfumo wa Kiislamu uliinuka ukiwa na nguvu na ustawi zaidi kuliko hapo awali, ukiwa na sauti yenye kusikika zaidi na kuruka juu zaidi, kama Phoenix; na hii ikawa tabia endelevu ya mfumo huu katika matukio yaliyofuata yaliyotengenezwa na maadui. Na sasa Phoenix huyo, kutokana na mashinikizo ya maadui, hususan vita viwili vya hivi karibuni vilivyolazimishwa, amekuwa mkubwa kiasi kwamba kivuli cha safari yake ya angani kimeenea hadi juu ya ardhi za maadui.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, huku akiitukuza kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa kishahidi Amir wa Kiarabu shujaa na alama kubwa ya Muqawama, Sayyid Hassan Nasrullah, na kutoa heshima kwa Muqawama na jihadi ya Kiashura ya Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu, pamoja na wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon, amesema: “Siku hizi za Lebanon ni siku mashuhuri na za fahari kwa wapiganaji wote wa Muqawama, na ni siku za udhalilifu na hatimaye aibu kwa wale ambao mbele ya adui Mzayuni wameweka matumaini yao katika ahadi za uongo za watawala wa dunia na watu wao wenye nia mbaya.”

Matini ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

“Na kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na ishara zetu, tukamwambia: Watoe watu wako kutoka gizani uwapeleke kwenye nuru, na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu.”

Surat Ibrahim, Aya: 5

Siku za mwanzo za mwezi wa Mehr zinakumbusha Siku za Mwenyezi Mungu na tukio kubwa na la kudumu la ulinzi wa kishujaa wa miaka nane wa wananchi wa Iran katika vita vya kwanza vya kulazimishwa. Katika siku hizo, mwangaza wa joto wa jua la Mapinduzi katika anga ya ardhi ya Iran ulikuwa ukieneza hisia nzuri ya mshikamano wa kitaifa na uaminifu kwa madhehebu na mwenendo wa Uislamu wa kimapinduzi; jambo ambalo kutokana na athari yake, barafu za utawala wa kibeberu na ukoloni wa zamani na mpya zilikuwa zikiyeyuka. Katika siku hizo, baadhi ya wananchi wa Iran walikuwa wakikumbuka kumbukumbu za miaka zaidi ya ishirini iliyotangulia kuhusu uadui wa wakoloni na matukio yaliyohusiana na kutaifishwa sekta ya mafuta na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani.

Wengine walikuwa wamesikia habari hizo, na wengi wao walikuwa wameishuhudia kwa karibu hali halisi ya kile ambacho utawala wa wageni juu ya masuala ya nchi yetu ulikuwa umekileta juu yake. Lakini siku zilizotangulia zilikuwa siku zenye giza na huzuni, ambapo mabalozi wa serikali za kibabe walikuwa wakimfikishia mfalme wa nchi masharti ya mambo ya kufanya na kutofanya, naye kwa hiari au bila hiari alikuwa akiyatekeleza, hadi Mapinduzi makubwa ya wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini (ra) yalipovuruga mfumo huo.

Siku hizo za giza, kutokana na Mapinduzi haya, ziligeuka kuwa siku zenye nuru za kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jambo hili liliwakasirisha sana watawala wa kibeberu waliokuwa wameelekeza tamaa zao kwenye utajiri wa nchi hii, na ambao kwa miaka mingi walikuwa wamewafanyia watu wake aina mbalimbali za maovu ili kuumiliki utajiri huo.

Kwa hiyo, tangu wakati huo walielekeza juhudi zao zote katika kuugeuza mkondo wa mto mkubwa wa wananchi wanamapinduzi na kuurudisha katika mwelekeo wa awali; na vita vya kwanza vya kulazimishwa vilikuwa hatua yao muhimu zaidi katika muongo wa kwanza wa maisha yenye baraka ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kutoka ndani ya moto wa vita hivyo, uliowashwa na Chama cha Baath kilichokuwa dhidi ya wananchi, kwa dhana kwamba vita vingedumu siku chache na kwamba ushindi ungepatikana kwa urahisi, mfumo wa Kiislamu uliinuka ukiwa na ustawi na nguvu zaidi kuliko hapo awali, kama Phoenix, ukiwa na sauti yenye nguvu zaidi na safari ya juu zaidi kuliko zamani; na hali hii ikawa tabia endelevu ya mfumo huu katika matukio yaliyofuata yaliyotengenezwa na maadui.

Siku zile ambapo adui alikuwa amewatawala wananchi hawa kupitia vibaraka wake na kutumia aina mpya ya ukoloni, kwa baraka za Mapinduzi na kuinuliwa bendera ya Uislamu na jihadi katika mazingira ya vita vya kulazimishwa, ziligeuka kuwa siku za fahari ambazo hata baada ya kupita miaka 38 tangu kumalizika kwake, tunapotafakari tukio baada ya tukio na simulizi za kweli za walionusurika, mifano ambayo kila mmoja wao ni funzo la ibada, ushujaa, upinzani, maadili na utu, hujitokeza kama nyota zinazong’aa katika kilele cha historia ya nchi yetu.

Siku zile ambazo mwanzoni mwa mashambulizi ya wafuasi wa mfumo wa utawala wa kibeberu, nchi yetu kwa ajili ya kujilinda dhidi ya vitisho vingi ilikuwa imerithi mikono mitupu kutoka katika mfumo wa kitwa'ghuti, kwa baraka za kusimamisha haki na msaada wa Mwenyezi Mungu, sasa zimefikia siku ambazo watawala wenyewe wa kibeberu wanaofanya mashambulizi, na si wafuasi wao, wanatafuta hifadhi mbele ya mashambulizi ya wapiganaji wa Kiislamu na kunyoosha mikono ya kuomba vita visitishe.

Siku ambazo wao wanatamani kuirejesha nchi yetu kwenye siku hizo, siku ambazo zilikuwa siku zilizojaa kudumaa, udhalilifu na unyonge, utegemezi na sifa mbaya ya Iran katika ulimwengu wa Kiislamu; lakini siku hizi tunazoishi zimejaa maendeleo, heshima, uhuru na kiwango cha juu kabisa cha hadhi katika ulimwengu wa Kiislamu, bali katika ulimwengu mzima. Leo, baadhi ya watu wanatuchukulia kuwa dola kuu ya nne duniani. Bila shaka, wao wanasema hivyo kwa mujibu wa hesabu za kidunia; lakini kwa mujibu wa hesabu za Mwenyezi Mungu, nchi inayojiona kuwa ni ya Ahlul-Bayt watoharifu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote, na ambayo wananchi wake wengi wamejifunga na watu hao watukufu, na hawaogopi katika kusimamisha haki, ndiyo inayochukuliwa kuwa nguvu ya kwanza duniani.

Siku zile, bahari mbili za kusini mwa Iran zilikuwa uwanja wa kutembea majeshi ya adui, lakini katika siku hizi wao hawasongi mbele zaidi ya Bahari ya Arabia kutokana na mashambulizi yenye maumivu waliyopokea kutoka kwa wapiganaji mashujaa na walinzi wa Mlango wa Hormuz; na kila walipothubutu kujihatarisha kwa jambo hilo, wamejisababishia madhara wao wenyewe; na si muda mrefu kabla Bahari ya Arabia nayo kujitakasa kutokana na uwepo wao.

Kulikuwa na siku ambazo watawala wa kibeberu, kupitia operesheni za kisaikolojia na kuunda mazingira ya vitisho, waliifanya mitaa ya mji mkuu kuwa mitupu na kuanzisha mapinduzi ya kijeshi dhidi ya harakati ya wananchi hii ya kutafuta uhuru, na baada ya hapo wakapora utajiri wa nchi hii kwa miaka 25; lakini katika siku hizi, kwa muda wa miezi saba, wananchi wenzetu wamezipamba viwanja na mitaa katika sehemu mbalimbali za nchi kwa uwepo wao wenye uwajibikaji na shauku, ili kuwapa moyo wapiganaji wa Kiislamu na kumtia hofu adui. Kadhalika, zaidi ya Wairani milioni 30 wametangaza kujitolea kwao kujitoa muhanga, na ilipohitajika kuwepo aina fulani ya kujiandikisha tena, katika dakika 100 tu za mwanzo, zaidi ya watu 500,000 walikamilisha idadi iliyohitajika. Kwa sasa, katika maeneo yote ya Iran, ambayo yamepambwa na uwepo wa Wairani kutoka makabila mbalimbali, kuna matangazo mbalimbali ya utayari, hususan utayari wa kijeshi, ili kujenga uwanja wa mapambano ambao utawapa wao jina la heshima na kumpa adui yao fedheha.

Kulikuwa na siku ambazo ushujaa wa watu wa nchi hii ulitambulishwa kupitia wanaume wake; lakini sasa tuko katika siku ambazo wanawake katika baadhi ya nyanja za ushiriki wa kishujaa wanawazidi wanaume kwa ujasiri.

Kulikuwa na siku ambazo adui alijaribu kuendelea kuudhoofisha msingi wa kijamii wa mfumo; lakini katika siku hizi, matabaka mbalimbali ya jamii, licha ya tofauti zao zilizo wazi, yanasisitiza kulinda misimamo yao ya haki, miongoni mwao ikiwa ni kulinda Mlango wa Hormuz wenye baraka na manufaa.

Ulinganisho huu kati ya siku zilizopita na siku za sasa bado unaweza kupanuliwa na kuelezwa zaidi, lakini kwa neno moja, mimi, kama mtumishi wa wananchi wapendwa wa Iran, natangaza kwamba; siku zile za zamani ambazo adui yetu anatamani zirejee zimepita, na hazitarudi tena kamwe. Bila shaka, kwa uchungu na huzuni, lazima nikumbuke kwamba katika siku hizi tunamkosa sana Khomeini Mkuu na Khamenei mwenye heshima kubwa, mashahidi—Mwenyezi Mungu ainue daraja zao—ambao heshima ya leo ya nchi inadaiwa na uongozi wao. Lakini kwa baraka za hazina yenye thamani waliyowaachia wafuasi wao kutokana na matendo yao na maneno yao yenye kung’aa na yenye kutoa mwongozo, siku zijazo zitakuwa zenye utukufu mkubwa zaidi kuliko siku hizi. Kwa sababu Phoenix aliyetokea kutoka katika lundo la moto wa vita vya kwanza vilivyolazimishwa, sasa kutokana na mashinikizo ya maadui, hususan vita viwili vya hivi karibuni vilivyolazimishwa, amekuwa mkubwa kiasi kwamba kivuli cha safari yake ya angani kimeangukia juu ya ardhi za maadui.

Katika fursa hii, inafaa sana, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuwawa kishahidi Amir shujaa wa Kiarabu na alama kubwa ya Muqawama, shahidi mwenye daraja kubwa, Sayyid Hassan Nasrullah [Mwenyezi Mungu autakase moyo wake]. Yeye alikuwa mtu mwenye nia njema ya dhati kwa watu wake na kwa madhehebu yake, ambaye khutba zake za kweli na zenye utamu, pamoja na hatua zake za kishujaa, zilikuwa zikiimarisha nyoyo za watu wake na hata za watu huru duniani. Alikuwa mtu aliyeliinua jina la Lebanon, nchi ndogo ambayo kwa miaka mingi ilikuwa imekuwa uwanja wa nyuma kwa baadhi ya madola, na kulifikisha katika utukufu, alikuwa mtu ambaye nusra na ushindi vilikuwa masahaba wake wa kudumu; na bila shaka katika historia yote ya Miji ya Sham hadi sasa, baada ya Mitume na Mawasii wao, hakukuinuka katika eneo hilo la kale mtu mwenye ukubwa kama yeye. Na kwa sasa, bendera yake yenye fahari iko mikononi mwa Sheikh Naim Qassem—Mwenyezi Mungu amhifadhi—ambaye kwa ushujaa, akiwa mbele ya safu imara na ya Kiashura ya Hizbullah, anaendelea kufuata njia yake.

Siku hizi za Lebanon, mbele ya historia na hata kuanzia sasa, ni siku mashuhuri na za fahari kwake yeye na wapiganaji wote wa Muqawama; na ni siku za kuleta udhalili na hatimaye aibu kwa wale ambao mbele ya adui Mzayuni wameweka matumaini yao katika ahadi za uongo za watawala wa kibeberu na watu wao wenye nia mbaya, watu ambao, tofauti na Sayyid shahidi wa Muqawama, Sayyid Hashim Safi al-Din, na wapiganaji wa sasa wa Muqawama ambao wataendelea kung’aa kama nyota zenye mwanga katika mwendelezo wa historia na kuwaongoza watafutaji wa njia waliobaki katika mshangao, wao watazikwa na kusahaulika haraka sana katika kurasa za mwanzo kabisa za historia; na kila watakapokumbukwa katika siku zijazo, watakuwa ukumbusho wa uovu, kutokuwa na busara na hata, pengine, usaliti.

Mwisho, ninatumaini kwamba kwa kuendelea fadhila za Mwenyezi Mungu na dua maalumu ya Bwana wetu—Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake—na kwa ajili yake roho zetu ziwe fidia, wananchi wa Iran na wafuasi wote wa Muqawama wasikabiliane na chochote isipokuwa nusra, ushindi na heshima, na maadui zao wasikabiliane na chochote isipokuwa kushindwa na udhalilifu; kwa fadhila na ukarimu wa Mwenyezi Mungu.

Sayyid Mojtaba Husayni Khamenei
6 Mehr 1405

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha