Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Mufti Sayyid Ashiq Hussein, mwanazuoni wa Ahlu Sunna kutoka Pakistan, ambaye alisafiri kwenda Iran kushiriki katika mazishi ya Kiongozi Shahidi, alisema katika mahojiano na Shirika la Habari la Hawza kwamba, akielezea aliyoyaona katika safari yake ya Iran na ushiriki wake katika hafla ya mazishi ya Kiongozi Shahidi, aliitaja hafla hiyo kuwa ni dhihirisho la umoja wa Umma wa Kiislamu na uhusiano wa kina kati ya mataifa ya Iran na Pakistan.
Mwanzoni mwa mazungumzo yake, alimshukuru Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Iftikhar Hussein Naqvi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Imam Khomeini (qs), pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Nyumba ya Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisema: "Kwa baraka za juhudi za watu hawa wema, nilipata fursa ya kushiriki katika hafla hii ya kihistoria na kushuhudia kwa macho yangu mapenzi na uaminifu wa watu kwa Kiongozi Shahidi."
Mufti Sayyid Ashiq Hussein, akizungumzia mazingira ya urafiki yaliyotawala nchini Iran, alisema: "Tangu nilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Tehran hadi nilipotembelea miji ya Tehran, Qom na maeneo mengine, wananchi wa Iran walinipokea kwa upendo, heshima na ukarimu wa kipekee. Kila nilipoonekana nikiwa nimevaa mavazi ya Kipakistan, watu walinipokea kwa tabasamu na kuonesha mapenzi yao kwa kaulimbiu za ‘Urafiki kati ya Iran na Pakistan uendelee daima’ na ‘Iran na Pakistan ni ndugu.’”
Shahada ya Kiongozi Shahidi; msiba kwa Umma mzima wa Kiislamu
Alisisitiza: "Shahada ya Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei haikuwa msiba kwa Iran pekee, bali ni huzuni ya pamoja kwa Umma wa Kiislamu na kwa watu wote huru duniani. Yeye alikuwa shahidi wa Umma wa Mtume Mtukufu (saww) na mmoja wa viongozi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu ambaye kwa ustahimilivu na msimamo wake alitekeleza jukumu la kihistoria katika kulinda matukufu ya Uislamu na heshima ya Waislamu."
Msimamo thabiti wa Iran uliharibu mipango ya maadui
Mwanazuoni huyo wa kidini aliongeza: "Viongozi wa utawala wa Kizayuni walidai wakati wa vita kwamba Iran ndiyo kikwazo kikubwa zaidi katika kufanikisha malengo yao na kwamba baada ya kuishinda Iran, wangeelekeza mashambulizi yao dhidi ya Makkah Tukufu na Madina Munawwara. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutegemea imani, Muqawama na ustahimilivu, ilivunja mipango hiyo yote na kumshinda adui katika kufikia malengo yake."
Mkurugenzi wa Jamiat Zainabiyya Pakistan alisema kuwa; ushiriki wa wajumbe wa ngazi za juu wa Pakistan katika mazishi ya Kiongozi Shahidi unaonyesha kina cha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, akisema: "Ushiriki wa Waziri Mkuu wa Pakistan Muhammad Shehbaz Sharif, Field Marshal Sayyid Asim Munir, Bilawal Bhutto Zardari na Sayyid Mohsin Naqvi katika hafla hii umeonesha kwamba Iran na Pakistan hushirikiana katika huzuni na furaha, na kwamba uhusiano wa mataifa haya mawili umejengwa juu ya msingi wa undugu na kuheshimiana."
Vituo vya kielimu vya Qom vinasisitiza umoja wa Kiislamu
Aidha, akizungumzia programu za kielimu za safari yake, alisema: "Katika kipindi cha siku nane nilichokaa Iran, nilikutana na Ayatullah Alireza A'rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, manaibu wake, viongozi wa Chuo Kikuu cha Qom na kundi la wanazuoni pamoja na viongozi wa Hawza. Mada kuu ya mikutano hiyo ilikuwa kuimarisha umoja wa Kiislamu na kukuza upendo na kuheshimiana kati ya Mashia na Ahlu Sunna. Nilichokiona katika mikutano hiyo kinaonyesha dhamira ya dhati ya taasisi za kielimu za Iran katika kuimarisha mshikamano wa Umma wa Kiislamu."
Mufti Sayyid Ashiq Hussein aliendelea kwa kusema: "Nilipata heshima ya kushiriki katika Swala ya maiti na mazishi ya Kiongozi Shahidi yaliyohudhuriwa na mamilioni ya watu, nikiwa mwakilishi wa Pakistan katika safu za mbele za washiriki. Pia walikuwepo wanazuoni, mabalozi na shakhsia mashuhuri kutoka nchi mbalimbali. Heshima hii ni kielelezo cha uhusiano wa kina wa kindugu na kirafiki kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan."
Uhusiano wa kindugu kati ya Iran na Pakistan ni mtaji wenye thamani kubwa
Mwenyekiti wa Jamiat Bayt al-Qur'an Pakistan alisema kuwa; katika safari yake yote alipokelewa kwa upendo na heshima kubwa na wananchi wa Iran, akieleza: "Mapokezi haya mazuri ni matokeo ya uhusiano wa kirafiki na sera ya ushirikiano na ujirani mwema kati ya Iran na Pakistan. Kwa mtazamo wangu, roho ya kujitolea, utamaduni wa ushahidi, ujasiri na ustahimilivu wa taifa la Iran ndio mtaji mkubwa zaidi na chanzo cha nguvu ya nchi hiyo katika kukabiliana na changamoto na vitisho vyote."
Akisifu namna hafla ya mazishi ilivyoandaliwa, alisema: "Katika hafla yote, vijana, wazee, wanawake na hata watoto walikuwa wakiwahudumia mazuwari na washiriki kwa kuwapatia maji, chakula na mahitaji mengine kwa moyo wa kujitolea wa mfano wa kuigwa. Aidha, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia mipango madhubuti, maandalizi ya huduma muhimu, mfumo mzuri wa sauti na usimamizi makini wa hafla, waliwezesha kufanyika kwa tukio hili la kihistoria kwa mafanikio makubwa, jambo linalostahili pongezi."
Mufti Sayyid Ashiq Hussein alihitimisha kwa kulitakia taifa la Iran mafanikio na kusema: "Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aijaalie Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iendelee kuwa na heshima, nguvu, usalama na maendeleo yanayozidi kuongezeka. Kama alivyosema Allama Muhammad Iqbal Lahori, iwapo Tehran itakuwa ‘Geneva ya Mashariki’, inaweza kuwa na nafasi ya kuamua mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu na hata ulimwengu mzima.”
Maoni yako