Alhamisi 23 Julai 2026 - 11:13
Mwandishi wa Habari Aliyemrushia Bush Kiatu: Ushirikiano wa Muqawama Kati ya Mashia na Masunni Ulishinda Uvamizi wa Marekani Nchini Iraq

Hawza/ Muntadhar al-Zaidi, mwandishi wa habari wa Iraq ambaye aligeuka kuwa alama ya kimataifa ya muqawama dhidi ya ukoloni baada ya kumrushia George Bush kiatu mwaka 2008, ameeleza undani wa nyuma ya pazia kuhusu uvamizi wa Iraq na kusisitiza kuwa; kuondoka kwa jeshi la Marekani kulitokana na muqawama wa pamoja wa Mashia na Ahlus-Sunnah wa Iraq, ingawa Washington bado inaendelea kuitawala Baghdad kupitia ushawishi wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Islami Analysis, Muntadhar al-Zaidi, mwandishi wa habari wa Iraq ambaye aligeuka kuwa mmoja wa alama za kimataifa za kupambana na ubeberu baada ya kumrushia kiatu George W. Bush, aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, katika mahojiano alieleza kwa kina sura zilizofichika za uvamizi wa Iraq, nafasi ya Marekani katika mabadiliko ya kisiasa ya nchi hiyo, hali ya sasa ya Eneo la Kijani la Baghdad, pamoja na athari za Operesheni "Tufani al-Aqsa".

Kumrushia Bush kiatu kulikuwa matokeo ya miaka mingi ya muqawama dhidi ya uvamizi

Al-Zaidi alisema kuwa kitendo chake cha kihistoria dhidi ya Bush hakikuwa jambo la papo kwa papo, bali kilikuwa matokeo ya miaka mingi ya maandalizi na hasira zilizojengeka kutokana na uvamizi wa Iraq.

Alisema: "Kitendo hicho hakikuwa jaribio langu la kwanza la kupambana na uvamizi. Kama mwandishi wa habari, katika kipindi cha uvamizi haramu na usio wa haki wa Iraq uliofanywa na Marekani, nilifanya kila juhudi kufichua ukweli. Mwanadamu ana wajibu wa kuitetea nchi yake, ardhi yake na historia yake dhidi ya uvamizi wa aina hiyo. Iraq haikustahili kuvamiwa na mataifa mengine kwa kisingizio cha kuleta demokrasia. Uvamizi huo ulisababisha kufanyika kwa uhalifu ambao ni mifano ya uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, mabomu dhidi ya maeneo ya makazi na sehemu salama, uharibifu wa miundombinu, pamoja na kuvunjwa kwa jeshi na vikosi vya usalama vya Iraq."

Ukumbi ulikuwa umejaa maafisa wa ujasusi na wanamaji wa Marekani

Al-Zaidi akielezea mazingira ya ukumbi uliokuwa ukitumika kwa mkutano wa waandishi wa habari wa Bush alisema: "Ndani ya ukumbi huo hawakuwepo waandishi wa habari pekee, bali maafisa wa ujasusi wa Marekani walikuwa kila mahali. Wanamaji wa Marekani pia walikuwepo, hata watu waliokuwa wakisimamia taa na kugawa kamera walikuwa wanajeshi. Walikuwa wameudhibiti kabisa ukumbi huo, huku waandishi wa habari wa Iraq na wa kigeni wakiwa wamezungukwa nao."

Aliongeza kuwa Bush alifika Iraq siku hiyo kwa madai ya kusaini "Mkataba wa Mfumo wa Kimkakati" au mkataba wa usalama, lakini lengo lake halisi lilikuwa kutangaza ushindi wa Marekani nchini Iraq.

Alisema: "Kwa hakika alikuja kuwaaga wanajeshi wake na kukabidhi madaraka kwa Barack Obama kwa madai ya uongo kwamba ameikomboa Iraq na kuiletea amani. Kwa hiyo, mimi pia, kama raia wa Iraq ambaye nilikuwa nikiwakilisha madhila ya wananchi wa Iraq na zaidi ya waandishi wa habari 127 waliouawa, nilimpatia busu la kuaga kutoka kwa wananchi wa Iraq."

Al-Zaidi pia alisema kuwa kwa miaka mingi alikuwa akiwaza kutekeleza kitendo hicho na alijitahidi kila alipopata nafasi kumlenga Bush ili kuonesha kwamba wananchi wa Iraq hawakuwapokea wavamizi kwa maua.

Kuondoka kwa jeshi la Marekani ni ushindi wa upinzani, lakini ulinzi wa kisiasa bado unaendelea

Al-Zaidi alisisitiza kuwa; kuondoka kwa jeshi la Marekani nchini Iraq kulitokana na mapambano ya wananchi wa nchi hiyo. Alisema: "Tuliondokana na tatizo kubwa lililoitwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani, na jambo hilo lisingewezekana bila juhudi za muqawama wa Iraq, wa Mashia na Masunni, tangu mwaka 2003 hadi sasa, Wamarekani waliondoka Iraq kijeshi lakini hawakuondoka kisiasa. Maamuzi ya Iraq bado yako mikononi mwa Ubalozi wa Marekani, ingawa Ukanda wa Kijani kwa sura ya nje limekabidhiwa serikali ya Iraq, kwa vitendo ni Ubalozi wa Marekani unaosimamia mchezo wa kisiasa katika eneo hilo."

Akieleza kuwa; Iraq imekuwa mateka wa sera za serikali za Marekani tangu miaka ya 1990, aliongeza: "Uamuzi wa Iraq ni uamuzi wa Marekani. Hata uteuzi wa Waziri Mkuu katika dakika za mwisho hufanyika kwa uamuzi wa Marekani, katiba ya sasa ya Iraq pia ni katiba iliyowekwa na Wamarekani, na hadi leo tunaendelea kulipa gharama ya katiba hii iliyojaa mitego ya kisiasa."

Tufani al-Aqsa ni mwanzo wa mfumo mpya wa dunia

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Al-Zaidi, akichambua maendeleo yaliyotokea baada ya Operesheni "Tufani al-Aqsa" ya tarehe 7 Oktoba, alilinganisha utendaji wa Marekani na utawala wa Kizayuni na tawala za kifashisti za Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Alisema: "Jumuiya ya kimataifa ya sasa haina ufanisi. Umoja wa Mataifa umeshindwa kutekeleza wajibu wake na Baraza la Usalama limepooza, Jumuiya ya kimataifa imekumbwa na hofu na kutokuwa na hatua, hali hii inafanana kabisa na mazingira ya kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia au wakati wa vita hivyo, ambapo ufashisti, Unazi na Dola ya Kijeshi ya Japan zilikuwa katika kilele cha uhalifu wao, lakini miaka michache baadaye nini kilitokea? Ufashisti ulitoweka, Unazi uliangamizwa na Dola ya Japan nayo ikafikia mwisho, leo hata majina ya tawala hizo hayatamkwi tena kwa hadhi ile ya zamani, ninaamini kwamba Marekani, utawala wa Kizayuni na mikondo yote inayohusiana nayo pia kwa sasa inapitia kipindi chake cha mwisho cha uhai."
Serikali ziko upande wa Marekani, lakini mataifa yako upande wa Palestina

Mwishoni mwa mazungumzo yake, Al-Zaidi alisisitiza kuwa hadi pale suala la Palestina litakapopatiwa ufumbuzi, dunia haitarejea kamwe katika hali yake ya kawaida. Alisema: "Baada ya tarehe 7 Oktoba, dunia imegawanyika katika sehemu mbili; upande mmoja zipo serikali za Magharibi zinazoiunga mkono Marekani, na upande mwingine zipo mataifa yaliyosimama pamoja na harakati ya Palestina. Kwa maneno mengine, Ikulu ya White House iko upande mmoja na wananchi wa Marekani wako upande mwingine. Serikali ya Uingereza imesimama pamoja na Marekani na utawala wa Kizayuni, lakini wananchi wa Uingereza wako pamoja na harakati yetu. Ninaamini kwamba wimbi hili la wananchi litaathiri bara zima la Ulaya, na wale wanaopinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Ghaza watakuwa na nafasi muhimu katika kuunda serikali za baadaye za Ulaya."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha